Mwalimu Galus Focus Nguruwe akiwa amefungwa mnyororo
Ndugu wa mtu anayedaiwa kuwa ni mlemavu wa akili, Galus Focus Nguruwe
(35) ambaye ni mwalimu wa sekondari moja mjini Morogoro, wamelituhumu
Kanisa la House of Prayer Shield of Faith Christian Fellowship lililopo
Boko Magengeni jijini Dar kuwa wamemfunga mnyororo ndugu yao huyo kwa
miezi nane mfululizo.
Kwa mujibu wa dada wa Galus, Piencia Focus, ndugu yao huyo
alichukuliwa na mke wa mtoto wa dada yao waliyemtaja kwa jina la Doreen
kutoka Songea mkoani Ruvuma Januari, mwaka huu bila kuwataarifu ndugu,
jambo lililowafanya wamfuatilie na kugundua alipelekwa kwenye kanisa
hilo kwa madai ya kufanyiwa maombi.
Dada wa Galus, Piencia Focus akiwa kanisani hapo
Dada huyo alisema kuwa aliamua kumtafuta ndugu yake hasa baada ya
kupata taarifa kuwa aliko amekuwa akishinda huku amefungwa mnyororo
mguuni, hali inayomfanya ajisaidie na kula papohapo.
“Japokuwa alikuwa na matatizo ya akili tangu zamani, lakini alikuwa
akitumia dawa zake na alipata nafuu na kufanya kazi yake ya ualimu kwani
alikuwa akifundisha shule moja ya sekondari Morogoro,”
alisema Piencia Focus.
Kaka
wa Galus,Peter Focus akizungumza na waandishi wa habari. Naye kaka wa
Galus, aliyejitambulisha kwa jina la Peter alisema baada ya kupata
taarifa kwamba mdogo wake yupo kwenye kanisa hilo aliamua kufika kwa
ajili ya kumchukuwa kistaarabu lakini cha kushangaza alijikuta
akiangukia kwenye mikono ya waumini hao wakidai yeye ni gaidi na
wakamkwapulia fedha zake.
Peter alisema alipoachiwa alikimbilia Kituo cha Polisi Wazo Hill
ambapo alifungua jalada lenye Namba za Kumbukumbu WH/RB/6364/14 WIZI
TOKA MAUNGONI. Waumini
wa kanisa hilo wakijibizana na ndugu wa Galus kanisani hapo. Peter
alisema alilazimika kuungana na dada yake kwa kushirikisha na vyombo vya
usalama ambapo walifika kanisani hapo kwa mara nyingine ili kumkomboa
ndugu yao na kuwatia mikononi waumini waliomwibia fedha zake. Waandishi
wetu waliokuwa karibu na eneo hilo walizinyaka taarifa hizo na kufika
kanisani hapo ambapo waliwashuhudia ndugu hao wakiwa na polisi
wakimchukuwa mmoja wa watuhumiwa waliodaiwa kumshambulia Peter na
kuondoka naye.
Kanisa
la House of Prayer Shield of Faith Christian Fellowship kwa muonekano
wa mbele. Hata hivyo, jambo la kushangaza ni kitendo cha polisi hao
kumwacha Galus akiwa bado amefungwa kwenye nguzo na mnyororo kanisani
hapo wakidai watamfuata baada ya kumpeleka mtuhumiwa wa unyang’anyi
kituoni, jambo ambalo halikuwa la kweli kwani hawakufika kwa siku hiyo.
Waandishi wetu walishuhudia timbwili la aina yake kanisani hapo kati
ya waumini wa kanisa hilo na ndugu wa Galus waliorejea kwa lengo la
kumchukuwa ndugu yao baada ya awali kumpeleka kituoni mtuhumiwa wa
kumshambulia Peter.
Waandishi wetu walipoomba kuzungumza na uongozi wa kanisa hilo
ilishindikana na kujikuta wakishambuliwa kwa maneno huku wakitakiwa
kuondoka mara moja katika eneo la kanisa hilo.
No comments:
Post a Comment