Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania < dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akiwa katika majadiliano kuhusu utengamano wa Afrika na Fursa za
biashara na Uwekezaji, na baadhi ya viongozi, Katibu Jumuiya ya Afrika
Mashariki, Balozi Richard Sezibera (katika) na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa wa Ghana, Hanna Tetteh, wakati wakihojiwa na
Mwandishi wa habari wa Kimataifa na Mkurugenzi wa Kampuni ya ‘Eddo
Media’, Mark Eddo (kushoto).
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal
(wa nne kutoka kulia) akijumuika na baadhi ya viongozi wakati
alipohudhuria Mkutano wa GBF, uliofanyika kwenye Hoteli ya Atlantis
jijini Dubai.
Mo Dewji, akijumuika na washiriki wa Kongamano hilo....
Baadhi
ya Washiriki wa kongamano hilo kutoka Tanzania, Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Nehemiah Mchechu (wa tatu kutoka kulia)
akijadiliana jambo na Prof. Ahmada Ktahib kutoka Tume ya Utalii
Zanzibar wakati walipohudhuria mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya
Atlantis nchini Dubai.
Mfanyabiashara
mwenye ukwasi mkubwa Afrika Aliko Dangote katika mazungumzo na Makamu
wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal kuhusu uwekezaji wake katika kiwanda
cha simenti mkoani Mtwara. Dangote alisema kazi ya ujenzi inakwenda kama
ilivyopangwa na kwamba kiwanda hicho kitakuwa kikubwa kabisa kwa
uzalishaji simenti katika ukanda wa Afrika Mashariki. Kulia ni Balozi wa
Tanzania, Nchini Dubai, Mbarouk
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiagana na baadhi ya Viongozi na wawekezaji baada ya kumalizika kwa
Kongamano hilo.
**************************************
MAKAMU WA RAIS AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA KONGAMANO LA PILI LA KIMATAIFA LA BIASHARA KWA NCHI ZA AFRIKA JIJINI DUBAI
OKTOBA 03, 2014
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
Oktoba Mosi, 2014 ameiwakilisha Tanzania katika kongamano la pili la
Kimataifa la Biashara kwa nchi za Afrika lililofanyika katika jiji la
Dubai, Farme za Kiarabu.
Kongamano
hili limehudhuriwa na washiriki wapatao 800 kutoka nchi mbalimbali
duniani na limelenga katika kukuza uwekezaji katika nchi za Farme za
Kiarabu na kufungua fursa za kibiashara barani Afrika. Kongamano la
kwanza la namna hii lilifanyika pia jijini hapa mwaka jana na
kushirikisha washiriki wapatao 3000 kutoka nchi mbalimbali duniani.
Baadhi
ya Viongozi wa Afrika waliohudhuria kongamano hilo ni pamoja na Rais
Paul Kagame wa Rwanda, Rais John Dramani Mahama wa Ghana na Rais Mulatu
Teshone Watu wa Ethiopia.
Viongozi
hawa kwa nyakati tofauti walizungumzia umuhimu wa utengamano barani
Afrika na wakaeleza kuwa hiyo ndiyo fimbo pekee ya kukuza uwekezaji
wenye tija Afrika.
Pia
walizungumzia mabadiliko makubwa ya Afrika huku wakiwakumbusha
wawekezaji na wafanyabiashara waliohudhuria kongamano hilo kuwa Afrika
ya sasa siyo bara la giza na kwamba ni bara linalokuwa kimaendeleo kwa
kasi huku likiwa na fursa ya kukuza maendeleo yake kwa haraka. Kongamano
hili pia lilihudhuriwa na Mfalme Sheikh Mohammed Bin Rashid Al-Makhtoum
ambaye alialikwa na wenyeji wa kongamano hili yaani Kituo cha Biashara
cha Dubai.
Sambamba
na hao pia kulikuwa na wafanyabiashara wakubwa akiwemo Aliko Dangote,
ambaye sambamba na kuwa na uwekezaji mkubwa katika Afrika pia anawekeza
mkoani Mtwara katika ujenzi wa kiwanda kikubwa cha simenti kuliko vyote
Afrika Mashariki.
Mfanyabiashara
huyo mara baada ya mijadala ya ufunguzi wa kongamano hilo, pia alipata
nafasi ya kukutana na mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Bilal na
kubadilishana naye mawazo kuhusu uwekezaji wake Tanzania ambapo aligusia
nia ya kutumia mkaa wa mawe uliopo Mbinga katika uzalishaji wa nishati
kiwandani kwake pamoja na kutanua sekta ya usafirishaji ili kumudu
kusafirisha saruji kwa matumizi ya nje ya nchi.
Mfanyabiashara
huyo alifafanua kuwa, katika sekta ya usafirishaji pekee anatarajia
kuchangia ajira zipatazo 3000 na pia anakusudia kuwapa mafunzo
wafanyakazi wa kiwanda chake nchini Nigeria ili waendane na teknolojia
ya sasa katika uzalishaji.
Uwekezaji
wa Aliko Dangote katika Tanzania unatokana na nchi yetu kuwa na sera
nzuri za uwekezaji na anafafanua kuwa maendeleo ya ujenzi wa kiwanda
chake yanakwenda kama alivyopanga na ujenzi utakapokamilika na
uzalishaji kuanza, ni wazi eneo la Kusini mwa Tanzania litaanza
kubadilika kiuchumi kufuatia uwekezaji huo mkubwa.
Mheshimiwa
Makamu wa Rais akichangia katika mjadala ambao pia ulimshirikisha
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Balozi Richard Sezibera,
alisema nchi za Afrika na hususani Tanzania zimepiga hatua katika kuweka
mazingira ya uwekezaji licha ya kuwa changamoto ya uduni wa miundombinu
na urasimu.
Mheshimiwa
Makamu wa Rais alisema, Tanzania imeunganika katika mtandao wa barabara
hivyo kwa wawekezaji ni rahisi kwao kuwekeza huku pia nchi yetu
inategemea kuwa na ziada ya umeme katika miaka michache ijayo hali
itakayohakikishia uhakika katika uzalishaji hasa wa viwanda vikubwa
vinavyohitaji nishati kubwa ya umeme ili kuzalisha.
Pia
alisisitiza kuhusu umuhimu wa nchi za Afrika kuungana ili kurahisisha
matumizi ya miundombinu sambamba na kutanua masoko katika nchi za Afrika
na akaeleza kuwa Tanzania iko mstari wa mbele kuhakikisha inachangia
uwezo wake katika kuhamasisha nchi kuungana kwa lengo la kukuza
mahusiano, kuimarisha amani na kutanua fursa za uwekezaji.
“Sisi
Tanzania tupo katika uhusiano na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
sambamba na zile za Kusini mwa Afrika. Ushiriki wetu katika jumuiya hizi
unasaidia pia hasa sasa ambapo tunazungumzia kuweka mashirikiano na
nchi za Magharibi ya Afrika na hivyo kuwa na mfumo mmoja wa biashara
barani Afrika,” Mheshimiwa Makamu wa Rais anasisitiza.
Katika
hatua nyingine Mheshimiwa Makamu wa Rais alikutana na Makamu wa Rais wa
Sychelles Mheshimiwa Danny Faure ambaye alimuelezea Mheshimiwa Dkt
Bilal kuwa, Sychelles inakusudia kuanza safari ya ndege zake kuleta
watalii Tanzania sambamba na kununua mazao ya kilimo na ufugaji na hivyo
kuwa fursa mpya kwa wakulima wa mbogamboga, vitunguu na wafugaji wa
ng’ombe.
Mheshimiwa
Faure alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa, uhusiano baina ya
Tanzania ni Sychelles ni mkubwa na hivyo ili kuuwekea msingi imara upo
umuhimu wa kushirikiana katika biashara hasa kwa bidhaa ambazo
hazipatikani Sychellles.
Mheshimiwa
Makamu wa Rais Dkt. Bilal alipokea taarifa hiyo na kumueleza Makamu wa
Rais Faure kuwa, Tanzania itatoa taarifa kwa wafanyabiashara wake ili
waweze kuchangamkia fursa hiyo kupitia Bodi ya Biashara za Nje
(Tantrade).
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Oktoba 3, 2014 Dubai, UAE
No comments:
Post a Comment