Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu,
Mhe. Benjamini Wiliam Mkapa akiwahutubia Wajumbe waliohudhuria mkutano
wa Jiolojia uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa J.K Nyerere Jijini
Dar es Salaam
Baadhi wa Wajumbe
waliohudhuria mkutano wa Jiolojia wakifuatilia kwa makini hotuba
iliyokuwa ikitolewa na mgeni rasmi katika Ukumbi wa Kimataifa wa J.K
Nyerere Jijini Dar es Salaam.Wanasayansi
Vijana wakifuatilia mada wakati wa mkutano wa tatu wa Wanasayansi
Vijana Duniani wenye lengo la kuhakikisha kuwa vijana wanashiriki vyema
katika rasilimali za duniani kwa ajili ya maendeleo na ukuaji wa uchumi
thabiti. (Picha na Makala na Benedict Liwenga,
Vijana nchini hawanabudi kupenda kujifunza masomo ya Sayansi na
teknolojia ili waweze kupata ujuzi na mitazamo katika sekta ya gesi
ambayo inakuwa kwa kasi kubwa hapa nchini na Duniani kwa ujumla.
Kiukweli sayansi na teknolojia inasadikiwa kuwa mihimili mikubwa ya
sasa katika kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali kwani mambo mengi
yenye kuhitaji haraka hutegemea sayansi na teknolojia kwa kiasi kikubwa.
Licha ya kuwepo kwa changamoto zinazozikabili baadhi ya nchi nyingi
za Afrika katika kupata maendeleo ikiwa ni pamoja na kutowekeza katika
sayansi na teknolojia, hali inayopelekea baadhi ya nchi nyingi kukosa
Wataalam wa kutosha katika mambo ya sayansi na teknolojia, hivyo nchi za
Afrika zinahitaji kujikwamua na changamoto hiyo kwa kuhakikisha kuwa
zinawekeza katika sayansi ili kubadilisha uchumi wa Afrika.
Sayansi na teknolojia hapa duniani huleta maendeleo makubwa hivyo
Vijana wanatakiwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujituma katika
mambo ya sayansi na teknolojia ili kuweza kuleta uchumi endelevu.
Sambamba na hilo, katika Kongamano liloandaliwa hivi karibuni na
Wizara ya Nishati na Madini nchini Tanzania ambao ulifunguliwa rasmi na
Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe.
Dkt Mohammed Gharib Bilal ambao ulikuwa ni mkutano wa tatu wa
Wanasayansi Vijana Duniani wenye lengo la kuhakikisha kuwa vijana
wanashiriki vyema katika rasilimali za duniani kwa ajili ya maendeleo na
ukuaji wa uchumi thabiti, Wakala wa Jiolojia nchini, Profesa Mruma
alisema kuwa Mkutano huo una lengo la kurithisha taaluma ya jiolojia
inayohusisha madini, rasilimali, gesi na mafuta kutoka kizazi kimoja
hadi kizazi kingine.
Kongamano hilo la Vijana liliwakutanisha vijana toka nchi zaidi ya 42
zikiwemo baadhi ya nchi za Afrika Tanzania ikiwemo na ambaye ndiyo
alikuwa mwenyeji wa Kongamano hilo.
Katika kongamano hilo, Naibu
Waziri wa Wizara ya Nishati na madini, Mhe. Masele alisema kuwa
Serikali ya Tanzania imewekeza nguvu zake kwa katika kuendeleza sayansi
ya mambo ya gesi na mafuta pamoja na afya kwa kuanzisha Vyuo mbalimbali
na kuwapeleka baadhi ya Watanzania kwenda kusoma nje ya nchi ili waweze
kupata ujuzi na kuwa wataalam na wakaguzi katika sekta ya gesi, mafuta
na afya kwa lengo la kuja kuisaidia nchi.
Aidha, Mhe. Masele alisisitiza kuwa wajibu wa Serikali kuamua kwa
makusudi kusomesha vijana katika nchi mbalimbali ni kuwawezesha vijana
waweze kupata elimu juu ya sayansi na teknolojia hasa katika masuala ya
gesi ili kupata wataalam na wakaguzi wa kutosha nchini ambao
watalisaidia taifa kuinua uchumi wake.
“Hivi sasa Serikali imeanzisha vyuo mbalimbali nchini, programu
mbalimbali za mafunzo kwa watanzania, imetoa ufadhili wa masomo kwa
watanzania na imedhamini makongamano ya vijana ili wapate fursa ya
kujiendeleza’, alisema Masele.
Mhe. Masele pia aliyataka Makampuni ambayo ndiyo yalikuwa Wadhamini
wa kongamano hilo kuendelea kuwekeza nchini pamoja na kuendelea kulipa
kodi ili serikali iweze kukusanya mapato na wananchi wapate kunufaika na
mapato hayo.
Halikadharika, katika mkutano mwingine uliohusiana na mambo ya
Jiolojia uliowakutanisha Wataalam mbalimbali wa mambo ya jiolojia
ulimwenguni jijini Dar es Salaam, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mhe.
Benjamini William Mkapa ambaye alikuwa ndiye mgeni rasmi wa mkutano huo
aliziasa jamii hizo za Kiafrika kuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na
mambo ya sayansi na teknolojia ili ziweze kujikwamua kimaendeleo.
Mhe. Mkapa alisema kuwa jamii nyingi za kiafrika hazijaelewa mchango
mkubwa wa sayansi na teknolojia katika kuleta maendeleo licha ya ukweli
wa kwamba maendeleo daima yanatokana na rasilimaliwatu iliyopo juu ya
ardhi na chini ya ardhi, mchango wake huo hauthaminiwi na wengi lakini
wanaoweza kufanya hivyo ni Wanasayansi.
“Serikali licha ya kudhamini mafunzo mbalimbali na masomo kwa vijana
nje na ndani ya nchi, fedha za kutosha bado zinahitajika katika
kuhakikisha kuwa kazi hiyo inakuwa endelevu”, alisema Mhe. Mkapa.
Bila shaka kuna haja ya kizazi kilichopo na kijacho kurithishwa
uelewa mzuri kuhusiana na mambo ya jiolojia ya jamii, jiolojia ya
madini, mazingira na mabadiliko ya tabianchi, vyanzo vya nishati,
matatizo yanayotokana na milipuko kama jiolojia na kuunganisha elimu ya
Tehama na jiolojia kwani hii itawasaidia vijana wengi kuelimika vya
kutosha kuhusiana na mambo ya jiolojia na pamoja na maendeleo kwa
manufaa yao wenyewe.
Naye Mwenyekiti wa Mtandao huo kwa upande wa Tanzania Bw. Stephen
Joseph Nyagonde alitaja kauli mbiu ya mkutano huo kuwa ni ”Kuhakikisha
ushiriki wa vijana katika rasilimali za duniani kwa ajili ya maendeleo
endelevu na ukuaji wa uchumi imara”.
Katika mikutano hii yote, wadau mbalimbali wakiwemo Wanasayansi
Vijana walipata fursa ya kujadiliana kwa kina na kutoa mapendekezo ya
kisayansi ya namna ya dunia inavyotakiwa kupiga hatua za kimaendeleo na
kuboresha maisha ya wakazi.
Jamii nyingi za Kiafrika kiuhalisia hazina uelewa wa kutosha
kuhusiana na mchango wa sayansi na teknolojia katika kuleta maendeleo
nchini hali inayopelekea kuzorota kwa maendeleo ya nchi nyingi za
Kiafrika.
Hivyo Wanasayansi ulimwenguni wanatakiwa kujenga utamaduni wa
kukutana mara kwa mara na kujadili mambo yanayohusu Sayansi na
teknolojia ili kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii hizo.
Endapo vijana nao wakichangamkia fursa mbalimbali za masomo
yanayohusiana na mambo ya rasilimali zipatikanazo nchini mwao kama vile
gesi asilia, mafuta na madini mengine wataweza kutatua kitendawili cha
umasikini Barani Afrika na nchini mwao, hasa vijana wa kike kujenga
utamaduni wa kujikita katika masomo ya sayansi ili waweze kuwa wabunifu
na kujikwamua na maisha yao.
No comments:
Post a Comment