Betty Ndejembi ni msichana mrembo na mwanamitindo ambaye
anatumia sana huduma za mitandao ya kijamii kwa ajili ya shughuli zake
mbalimbali za kujiingizia kipato na kujitangaza zaidi.
Siku moja alibakwa mpaka akapoteza fahamu,
akaokotwa na watu akapelekwa hospitali. Alipofika hospitali aliendelea
kutumia mitandao ya kijamii, kwa ajili ya kufahamisha wenzake
anavyoendelea kwa nia nzuri kabisa.
Jinsi alivyokuwa anafahamisha umma kuhusu
maendeleo yake, baadhi yao walitumia fursa hiyo kumtukana, kumnyanyapaa,
kutumiana picha zake na dhihaka nyingine nyingi kwa njia ya mitandao
hiyo hiyo.
Betty alifariki dunia baadaye wakati anaendelea na
matibabu, lakini matusi aliyovurumishiwa, maneno aliyoambiwa na
unyanyasaji mwingine, umeleta historia mpya katika matumizi salama ya
mitandao ya mawasiliano.
Jijini Arusha kijana mmoja alikutwa na mke wa mtu,
akadhalilishwa huku akipigwa picha. Zile picha zikawekwa kwenye
mitandao kadhaa ya kijamii, baada ya siku chache yule kijana alionekana
amejinyonga chini ya daraja.
Huko Marekani dada mmoja anayeitwa Rebecca Ann Sedwick aliamua kujitoa uhai baada ya kudhalilishwa kupitia mtandao wa kijamii.
Kitendo alichofanyiwa Betty, kijana wa Arusha na
huyo mwanadada wa Kiingereza, kinaitwa kitaalamu kwa jina la
cyberbulling, yaani mtu kutumia njia za mawasiliano kwa nia ya kuumiza,
kudanganya au kumdhalilisha mwingine.
Vitendo hivi ni kama kutumia picha ambayo mwenyewe
hajaruhusu, kuandika habari za uongo hasa za udaku, kuandika au kutoa
maoni ambayo si ya kweli kwa nia ya kudhalilisha au kuumiza, kudanganya
kuhusu bidhaa au huduma fulani kwa nia hiyo hiyo.
Mimi binafsi niliwahi kukumbana na sakata kama
hili, lakini lilimkuta rafiki wa rafiki yangu mmoja. Yeye alikuwa na
mpenzi wake, kumbe wakiwa kwenye starehe yule mwanaume alikuwa na tabia
za kumpiga picha.
Siku ikafika hawakuelewana ikabidi kila mtu
aendelee na maisha yake, yule kijana akaingia katika mtandao wa kijamii
wa facebook akatengeneza jina bandia akaweka picha za yule binti na
kuwarushia watu wa karibu wa binti halafu akafuta lile jina.
Binti alienda kituo cha polisi kutoa taarifa,
polisi wakaomba ushahidi wa picha, lakini ndiyo hivyo jamaa alikuwa
ameshafuta mpaka jina, kwa hiyo wakaomba msaada, nikawapeleka polisi
makao makuu kitengo cha uhalifu wa mtandao.
Polisi waliweza kupata taarifa zote zinazohusu
yule kijana kwenye mitandao ya kijamii na wakaenda kumkamata alipokuwa
anaishi wakakagua simu zake, kompyuta na nyaraka nyingine wakapata picha
zote kama ushahidi na sasa hivi huyu kijana yuko jela.
Huko mitaani kuna kina Betty wengi wamezushiwa, wamedhalilishwa,
wamepakaziwa na kutengenezewa habari nyingi mbaya na za kuumizwa na
watu wanaowajua au kutowajua, lakini wanakaa kimya. Madhara yake ni
makubwa.
Ieleweke kuwa kukaa kwao kimya hakumaanishi
kitendo hiki kinakubalika. La hasha hili ni kosa kubwa la jinai ambalo
hapa nchini linaanza kuota mizizi. Watu wanatumia mitandao ndivyo sivyo.
Unachotakiwa kujua ni kwamba mawasiliano yote
kuanzia simu na mitandao ya kijamii, hata kama mtu alifuta, kampuni
inayotoa huduma husika huwa ina sehemu yake ya kuhifadhi mawasiliano
yote.
Tushirikiane pamoja ili kuweza kumaliza au
kupunguza tatizo hili la unyanyasaji, kwa kutumia vyombo vya mawasiliano
ili tuweze kuwa na jamii iliyostaarabika.
MAKALA: MWANANCHI
MAKALA: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment