MMOJA kati
ya wasanii ninaowa-heshimu sana katika muziki wa kizazi kipya kutokana
na uwezo wao, ni Judith Wambura Mbibo, mwenye majina mengi ya kisanii,
lakini maarufu zaidi Lady Jaydee au Jide.
Ni bonge la msanii, anajua kuimba, anajua mashairi yanayogusa na anakwenda na wakati.
Tokea
alipojiingiza katika muziki huo zaidi ya miaka 13 iliyopita, siku zote
amekuwa mtu anayepanda juu. Wamekuja wasanii wengi vijana wa kike,
wamejaribu lakini hakuna kati yao aliyeweza kufikia levo zake, achilia
mbali ndoto za kumpita.
Ni
kupoteza nafasi kuanza kutaja kazi za Lady Jaydee, kwa sababu
zinaeleweka sana. Lakini kubwa, pengine ni kuwakumbusha tu wasomaji
kwamba dada huyu aliwahi kufanya kolabo na mtu wa ndoto zake, Oliver
Mtukudzi, mwanamuziki anayetamba Afrika, raia wa Zimbabwe.
Aina ya
muziki anaoufanya, Afro Pop, hauchoshi na unabadilika kadiri anavyotaka.
Kwa uwezo na ubunifu wake, anaweza kuimba hata katika umri kama
aliokuwa nao Bi. Kidude. Lakini kuna jambo moja ambalo kwa mtazamo
wangu, ni la msingi sana kwake kulifanya kwa sasa, wakati ambao watu
wanaanza kumtazama kwa jicho la maswali yanayokosa majibu. Katika
maisha, siku zote binadamu ni watu wa kujifunza kwa sababu kila mmoja
hufanya makosa.
Jide
anatakiwa kutazama upya nyendo zake. Ni kuhusu uhusiano na watu wake wa
karibu. Nimewahi kufanya naye kazi kwa ukaribu kidogo, ni mtu mzuri,
hana roho mbaya, ni mwenye kupenda kusaidia anapoweza, ni muungwana na
kwa kweli, ni mwenye kupenda ushirikiano na kujituma.
Tatizo la
Jide ana hasira, kisasi na asiye makini katika matamshi yake, hasa kwa
kuzingatia nafasi yake katika jamii. Historia inaonyesha ni mtu mwenye
kupenda bifu zinazodumu na asiye tayari kuweka tofauti mezani kwa ajili
ya mjadala wenye lengo la mapatano.
Nina
mifano kadhaa, lakini nizungumzie michache ili kushibisha hoja. Kwa
tunaofuatilia Bongo Fleva kitambo, tunafahamu kwamba Jide alikuwa ‘mtoto
wa Ruge’ kwa miaka mingi. Wakati wasanii wengi walikuwa wakimlalamikia
Rugemalila Mutahaba, yeye alikuwa naye karibu kiasi cha wenzake kumuona
kama msaliti.
Sitaki
kujua kilichosababisha wakakorofishana, lakini kauli aliyoitoa Jide
kuhitimisha ugomvi wao ni kubwa na mbaya, kwamba ikitokea yeye
akatangulia kufa, basi Ruge na Joseph Kusaga (Mkurugenzi, Clouds Media
Group) wasifike kwenye msiba wake na endapo watakaidi, mashabiki wake
wawapige mawe.
Mtu
mwenye busara, kama ambavyo Jide anastahili kuwa, hawezi kutoa kauli
kama hii hadharani. Ujumbe mmoja unaoweza kuupata kwa maneno haya ni
kwamba amefuta kabisa uwezekano wa suluhu, kitu ambacho siyo kizuri.
Sugu
huenda ndiye msanii aliyevutana zaidi na Ruge pengine kuliko mwingine
yeyote, tena kwa miaka mingi. Tofauti kati yao zikaongezeka zaidi
walipokutana tena katika ishu ya Malaria No More, lakini pamoja na
machungu yote, Sugu hakuwahi kutoa kauli kali kama hii, akiamini wakati
wowote mambo yanaweza kubadilika.
Hivi
karibuni Jide alitofautiana na mumewe, Gardner G Habash. Magazeti ya
Global yalipoanza kuripoti juu ya kuvunjika kwa ndoa hiyo, aliyaponda
sana akitoa maneno mengi ya kejeli, kitu kilichomaanisha ndoa yao
ilikuwa salama. Lakini hatimaye, mwenyewe amekiri kwamba mchezo
umekwisha!
Hata
hivyo, kauli yake haikuwa imekaa vizuri, pale alipokiambia kituo kimoja
cha redio kwamba ‘amemuacha’ Gardner. Nia ya kauli hii ni kutaka
kuuonyesha umma kwamba ni yeye ndiye aliyeamua kumtema mwenzake. Na bila
shaka alifanya hivi makusudi ili kuziaminisha hisia za wengi kuwa
Gardner alikuwa akimtegemea yeye, pasipo kutambua kwamba amechangia kwa
kiwango kikubwa mafanikio aliyonayo.
Na mara
kadhaa amekuwa pia akitupia vijembe na kejeli kupitia mitandao ya
kijamii na hata kwenye blog yake. Ninafahamiana na wasanii
wanaoheshimiana naye, wanakuambia dada ni mtata!
Najua,
wote sisi kama binadamu tuna mapungufu, lakini siyo jambo baya kujiuliza
na kujirudi. Kitu cha msingi sana ni kuweka akiba ya maneno, ndiyo
maana hata Mfalme Suleiman alipotakiwa na Mungu kusema kitu anachohitaji
kutoka kwake, aliomba apewe hekima.
No comments:
Post a Comment