Kwako mheshimiwa Samuel Sitta.
Ni
matumaini yangu kwamba sasa unajipongeza kwa kufanikisha kazi uliyopewa
ya kuliongoza Bunge Maalum la Katiba ya kuhakikisha akidi inatimia ili
kupitisha rasimu ya katiba inayopendekezwa.
Najua
una furaha sana kwa hilo, upo kwenye karamu ya kufurahia ushindi kiasi
kwamba itakuwa vigumu sana kwa lofa kama mimi kukutana na wewe hasa
katika kipindi hiki ambacho unaamini kasi na viwango vyako
vimedhihirika. Hata hivyo, hilo halinizuii kufikisha ujumbe wangu kwako.
Mimi
si Mbunge wa Urambo Mashariki kama wewe, sikuzaliwa Desemba 18, 1942
wala sijamuoa mwanamke mwanasiasa, Magreth Sitta aliyewahi kushika
nyadhifa mbalimbali serikali kama wewe. Mimi ni mwananchi wa kawaida tu,
lofa, hohehahe nisiye na mbele wala nyuma.
Sijawahi
kuwa spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wala sijawahi
kujipatia umaarufu mkubwa na kupendwa na wengi kutokana na kuruhusu
mijadala ya ufisadi bungeni kama ulivyo wewe. Sijawahi kuibua kashfa
kubwa kama ya Richmond na kusababisha baadhi ya vigogo wang’atuke kwenye
nyadhifa zao.
Sina
nia wala sitegemei kuja kugombea urais wa nchi hii kama wewe, mimi ni
mwananchi wa kawaida kabisa. Sijawahi kujisifu kwamba mimi ni mtu wa
viwango na kasi, mimi ni mlala hoi tu.
Sijawahi
kuitumia nchi hii katika nyadhifa mbalimbali kuanzia nilipokuwa shule,
kwa zaidi ya miaka 40 nikigusa karibu awamu zote za uongozi kama wewe,
mimi si Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wala sijawahi kuota
ndoto kwamba nitakuja kuwa Spika wa Bunge Maalum la Katiba! Narudia
tena, mimi ni mwananchi wa kawaida kabisa, hohehahe nisiye na ndoto za
kuja kuwa mwanasiasa.
Hata
hivyo, ningekuwa mimi ndiyo nipo kwenye nafasi yako, hakika nakuapia
nisingeshiriki kwenye karamu ya wenye dhambi kama wewe. Nisingeshiriki
hata kidogo kuchakachua maoni ya mwenyekiti wa tume ya kukusanya maoni
kuhusu katiba mpya, Jaji Joseph Warioba kama wewe.
Nisingerudia
kukusanya upya maoni kwa wananchi wakati nikijua fika kuwa hiyo siyo
kazi yangu. Nisingebadilika ghafla kama wewe, kutoka kuwa shujaa wa
kutegemewa kama ulivyokuwa kipindi ulipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano na kuwa adui wa demokrasia kama ulivyo sasa.
Nakuhakikishia
nisingeshiriki kabisa karamu ya wenye dhambi, kwa kulazimisha wajumbe
wa bunge maalum la katiba, hata kwa vitisho waipigie kura ya ndiyo
rasimu ya katiba inayopendekezwa huku nikijua waziwazi kwamba
nimeshiriki kunyofoa vipengele vyote muhimu ambavyo wananchi
walivipendekeza ili kupata katiba bora.
Nisingefikia
hatua ya kuwatusi viongozi wa dini ambao walikuwa wakinionesha waziwazi
kwamba nilichokuwa nakifanya kwenye bunge maalum la katiba hayakuwa
matakwa ya Mungu bali ya watu wachache wenye dhambi.
Kwa
kuwa najua kwamba katiba ndiyo ‘injini’ ya maendeleo ya taifa lolote,
ningekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba maoni ya wananchi ndiyo
yanayoingia kwenye katiba bila kuchakachuliwa. Ningethibitisha kwa
vitendo kwamba mimi ni mtu wa kasi na viwango!
Nisingekubali
kuongozwa na tamaa ya kuja kuwa rais wa nchi hii kiasi cha kulipua
mchakato mzima wa kupata katiba kwa maslahi yangu na chama changu kwa
sababu ningejua kwamba umri umeshanitupa mkono (Una miaka 71 sasa)
lakini wapo wanangu, wajukuu na ndugu zangu wengi na watu wanaoniamini
ambao wanaisubiri kwa hamu katiba mpya itakayowakomboa, baada ya ile ya
awali kushindwa kuwatatulia kero zao kwa zaidi ya miaka hamsini sasa.
Narudia
tena, nisingeongozwa na tamaa ya madaraka, upendeleo kwa chama changu
wala maslhai ya mtu au watu fulani, la hasha! Ningesimamia haki katika
ukamilifu wake na rasimu ambayo ingepatikana, ingekuwa ni mawazo ya
wananchi wote na siyo uhuni kama uliofanyika sasa kupata rasimu ya
katiba inayopendekezwa.
Ningeongozwa
na hofu ya Mungu na nisingewaangusha wananchi ambao kwa kipindi kirefu
waliniona mpiganaji ninayesimamia maslahi yao na taifa kwa jumla na
kamwe nisingeshiriki karamu ya wenye dhambi kama ilivyotokea kwenye
Bunge Maalum la Katiba.
Kwa
bahati mbaya mimi nitabaki kuwa mimi na sitaweza kuwa wewe lakini kama
ningekuwa mimi kwenye nafasi yako, kwa jinsi hali ilivyo sasa, narudia
tena kusema bila kumung’unya maneno kwamba nisingeshiriki kwenye karamu
ya wenye dhambi kama wewe, ningesimamia ukweli, haki na demokrasia bila
kumpendelea wala kumkandamiza mtu yeyote.
No comments:
Post a Comment