Habari ya mjini kwa sasa ni bethidei ya Miss Tanzania 2006, Wema
Sepetu kutimiza miaka 26 tangu kuzaliwa, lakini ndani ya tukio hilo,
mengine yameibuka!
Staa katika tasnia ya filamu Bongo, Kajala Masanja. Miongoni mwa
yaliyoibuka kwenye sherehe hiyo iliyofanyika Jumapili iliyopita nyumbani
kwa Wema, Mtaa wa Bwawani, Kijitonyama jijini Dar es Salaam ni madai ya
mama Wema, Mariam Sepetu kudaiwa kupewa nafasi ya kutoa ‘neno la
hekima’ lakini akaitumia kumvurumishia mitusi aliyekuwa shosti wa Wema,
Kajala Masanja.
Baada ya sherehe hiyo, Jumatatu na Jumanne, mitandao mingi ya kijamii
ilitumbukiza video yenye sauti ikimuonesha mama Wema akimrushia matusi
Kajala kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kutokana na kukorofishana kwa
mwanaye na Kajala aliyewahi kumfadhili mahakamani kwa kumlipia faini ya
shilingi milioni 13 asiende jela kwa kesi ya kuuza nyumba iliyokuwa na
zuio la kisheria.
Wema Sepetu akiwa na mama yake. KAJALA AAMUA ZITO
Katika kufuatilia sakata hilo, Amani lilinyetishiwa kwamba Kajala
baada ya kushindwa kuvumilia, ameamua kumshitaki mahakamani mama Wema.
Chanzo chetu kinadai kuwa Kajala alifikia uamuzi huo baada ya kushauriwa
na familia sanjari na wafuasi wake (Timu Kajala) ambapo sasa, timu hiyo
na Timu Wema wameingia vitani tena.
“Kajala ameshawasiliana na wanasheria wawili na kutoa maelezo yake,
wao wanaandaa faili ili mashitaka yafike mahakamani, amekasirika
sana.“Amesema mama Wema ametumia nafasi ya kukutana na watu
kumdhalilisha bila kumpa nafasi ya kujitetea, ameona si sawa hata
kidogo,” kilisema chanzo hicho ambacho ni jirani na Kajala.
Wema Sepetu akiwa na Kajala Masanja. MATUSI YENYEWE
Katika sauti, mama Wema anasikika akitamka matusi (hayaandikiki
gazetini) huku Wema naye anasikika akimsihi mama yake asimtaje jina
Kajala kwa kuwa kufanya hivyo ni kumpaisha. Hapa inamaanisha kwamba,
Wema alitaka mama yake afunguke lakini bila kutamka jina la mtu.
AGUNDUA TIMU KAJALA IMO NDANI YA BETHIDEI
Katika hatua nyingine, mama Wema alisema kauli iliyoashiria kwamba
Timu Kajala ilikuwemo ndani ya bethidei ya mwanaye. “Nasema haya huku
najua humu ndani kuna Timu Kajala, lakini nasema….(matusi mazito)”
KAJALA SASA
Baada ya madai hayo yote, juzi, Amani lilimsaka Kajala kwa njia ya
simu ili kumuuliza ukweli wa madai hayo. Licha ya kutopokea simu ya
paparazi wetu, alitumiwa ujumbe mfupi wa maneno ‘SMS’ na kuulizwa kila
kitu.
Hata hivyo, badala ya kujibu alikaa kimya, baada ya dakika kama kumi
na tano alimrushia kwa simu mwandishi wetu video hiyo ambayo anadai
kutukanwa na mama Wema bila kusema chochote hali iliyotafsiriwa kuwa
kama alisema; ‘hebu oneni wenyewe jamani, nimemkosea nini mama Wema?’
Mama yake Wema Sepetu. ALICHOKIFANYA MARTIN KADINDA
Katika hatua nyingine siku hiyo, meneja wa Wema, Martin Kadinda
alikuwa na kazi ya ziada kuhakikisha, mama Wema na mama Diamond, Sanura
Kasim ‘Sandra’ hawakai jirani au meza moja licha ya kwamba watoto wao
wamependana.
“Kadinda ana kazi ngumu sana, unajua anatakiwa kuhakikisha kwamba
mama Wema na mama Diamond hawakai meza moja. Sijui anaogopa nini, kwani
hawa si watu ambao watoto wao wana mpango wa kuoana?” alihoji mwalikwa
mmoja.
KUMBUKUMBU MUHIMU
Katika bethidei hiyo, Wema alizawadiwa magari mawili, Nissan Murano
lenye thamani ya shilingi milioni 36 alilopewa na Diamond na BMW 545i
lenye thamani ya shilingi milioni 56, inadaiwa alizawadiwa na Kadinda!
No comments:
Post a Comment