WADAU wa muziki nchini wamewapongeza
waratibu wa shindano la Dance 100% ambalo limefikia hatua ya fainali,
baada ya makundi matano kupenya nusu fainali, Jumamosi iliyopita.
Kivumbi hicho kilichoshindanisha makundi 10 yalipenya
hatua ya robo fainali, Iliyofanyika Viwanja vya Don Bosco, jijini Dar es
Salaam na kuvuta hisia za wengi kutokana na umahiri wa kila kundi.
“Nikiwa miongoni mwa watu waliojitokeza kushuhudia
shindano hili, nimepata burudani kubwa na kujifunza mengi, vijana
wameonyesha vipaji na uwezo wa kiwango cha hali ya juu,” alisema
Ramadhan Malenge ‘Ramso.’ Wapenzi wa shindano la Dance 100%.
Malenge alisema kilichomvutia katika shindano hilo, ni
kuona namna vijana walivyoonyesha uwezo mkubwa kiasi cha kuwapa wakati
mgumu majaji kuamua ni kundi gani la kutoka.
Alisema, hata vijana walioishia hatua hiyo ya nusu
fainali, bado ni wenye uwezo kwani wamenufaika na mengi katika shindano
hilo na kuwasihi wasiache kujiendeleza kimuziki.
Malenge aliyejitambulisha kama mpenzi na shabiki mkubwa
wa muziki, alisema kwa jinsi vijana walivyokuwa wakicheza staili
mbalimbali kwa ustadi mkubwa, ungetamani makundi yote yavuke, japo ni
kitu kisichowezekana.
Ramso alisema kwa umuhimu wa programu hiyo katika kuibua
na kuendeleza vipaji vya vijana, waratibu wa shindano hilo, kituo cha
televisheni cha East Africa (EATV) na kudhaminiwa na Vodacom Tanzania,
wanastahili pongezi.
Alisema, kama ngazi ya nusu fainali ilikuwa na ushindani
wa kiwango alichokishuhudia Don Bosco, majaji wa shindano hilo watakuwa
na kibarua kigumu zaidi siku ya fainali.
Makundi ya yaliyofanikiwa kuingia katika hatua ya
fainali, ni Wazawa Crew, Best Boys Crew, The W.T, Wakali Sisi na The
Winners Crew.
Shabiki mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Blandina
Kingu‘Queen B,’ mbali ya kupongeza uwepo wa shindano hilo, ametoa
ushauri wa bure kwa mchujo uwe unafanyika mikoa yote kabla ya fainali
kufanyika jijini Dar es Salaam.
Naye mratibu wa mashindano hayo, Happy Shame alikiri
kuwepo kwa ushindani mkubwa zaidi ikilinganishwa na miaka mingine miwili
iliyopita huku jamii ikizidi kulipa sapoti.
“Huu ni mwaka wa tatu EATV tunaandaa mashindano haya
chini ya udhamini wa Vodacom Tanzania, safari hii yamezidi kuwa na
umaarufu na ushindani kiasi cha kuwavutia vijana wengi ambao hujitokeza
kushiriki,” alisema Shame.
Shame, aliongeza kundi litakaloibuka kidedea katika
shindano hilo linalorushwa na kituo cha EATV kila Jumatano saa 1:00
usiku, litajishindia kitita cha shilingi milioni 5.
Naye Meneja Uhusiano wa Umma wa Vodacom Tanzania ambao ni
wadhamini wakuu wa shindano hilo, Matina Nkurlu aliwapongeza vijana
wote huku wakiwapa moyo walioshia hatua ya nusu fainali.
“Vodacom tunaamini, vijana ni chachu ya mapinduzi katika
sekta mbalimbali kama watawezeshwa, hivyo tunadhamini mashindano haya
tukiamini kuwa vijana wenye vipaji wanaoshiriki wataweza kujitangaza na
kujulikana ambapo katika siku za usoni ni rahisi kujiajiri kupitia
katika sanaa” anasema Nkurlu.
Alitoa wito kwa wakazi wa jijini Dar es Salaam kujitokeza
kwa wingi katika fainali ya shindano hilo itakayofanyika hivi karibuni
kuwatia moyo vijana na kununua bidhaa za Vodacom kwa bei nafuu katika
shindano hilo kama Modem na Simu aina ya Samsung E1205 zote zikiuzwa kwa
shilingi 25,000.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment