STRAIKA mahiri wa Simba, Mrundi Amissi Tambwe, amesema
alisikitishwa na taarifa za kutaka kuchujwa kikosini kumpisha
mshambuliaji Emmanuel Okwi raia wa Uganda na kuongeza kuwa anasubiri
dirisha dogo la usajili lifunguliwe ili afanye uamuzi mgumu.
Tambwe aliibuka kinara wa mabao msimu uliopita
lakini uongozi wa klabu hiyo ulikuwa unafikiria kumchomoa kikosini hapo
baada ya kutakiwa kupunguza mchezaji mmoja wa kigeni kupisha usajili wa
Okwi ili kukidhi idadi ya wachezaji watano wa kigeni wanaoruhusiwa
kucheza katika klabu moja.
Simba tayari ilikuwa na Joseph Owino raia wa Uganda, Donald
Mosoti na Raphael Kiongera raia wa Kenya pamoja na Warundi Pierre
Kwizera na Tambwe hivyo kutakiwa kumpunguza mmoja. Mosoti ndiye
aliyekuja kuondolewa baadaye baada ya hoja ya Tambwe kupata upinzani
mzito.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Tambwe alisema:
“Najua kuwa mimi ndiye niliyekuwa chaguo la kwanza la kuondolewa ili
kumpisha Okwi, nilisikitika sana nilipopata hizo taarifa kwani tayari
nilikuwa na mipango yangu mingi niliyokuwa nimeiahirisha kwa ajili ya
Simba.
“Siwezi kuweka wazi klabu nilizotaka kwenda lakini
nilikuwa na mipango mingi, kwa sasa nasubiri dirisha dogo ili niweze
kukamilisha mipango yangu, mimi naifahamu kazi yangu na huwa sichezi kwa
kubahatisha,” alisema Tambwe.
Hata hivyo straika huyo alisema: “Mosoti tayari
ameshaondoka, hakuna ujanja hao vijana wanatakiwa wajitahidi kucheza kwa
kuelewana na kuisaidia timu, hapo tutasogea lakini ukweli ni kwamba
kuna vitu vya Mosoti ambavyo tutavikosa.”
No comments:
Post a Comment