YANGA kupitia kwa Kocha Mkuu wake, Marcio Maximo, imechimba
mkwara na kuwatangazia wapinzani wake wakubwa ambao ni Simba, Azam na
Mbeya City kwamba kazi imeanza rasmi uwanjani na yale waliyokuwa
wakiyaona kwenye mechi za kirafiki ni rasharasha tu.
Kwa kusisitiza wana Jangwani hao wametamba kwamba
Azam watajibeba kesho Jumapili kwa kukumbana na makali yao kwenye mechi
ya Ngao ya Hisani ndani ya Uwanja wa Taifa.
Mchezo huo unaashiria ufunguzi wa msimu mpya wa
Ligi Kuu Bara ambapo Yanga msimu uliopita ilishika nafasi ya pili na
Azam ambayo ni klabu tajiri zaidi nchini na Afrika Mashariki ikatwaa
ubingwa.
Azam ipo kambini katika hosteli zake za Chamazi ikijifua chini
ya Kocha wao Mcameroon Joseph Omog ambapo licha ya kumkosa nahodha wake
ambaye pia ni mshambuliaji muhimu, John Bocco, bado kikosi hicho kina
nguvu ya wachezaji wapya walioongezwa kama Didier Kavumbagu, Leonel
Saint-Preux na Ismaila Diara na beki anayenyumbulika Shomari Kapombe.
Azam ilijinoa kwa kushiriki Kombe la Kagame na Yanga ikapiga kambi
Pemba.
“Tutamkosa Bocco ambaye bado anauguza goti lake,
wachezaji wangu wengine wako sawa tutacheza mpira wetu tunaocheza wakati
wote, tunawaheshimu Yanga lakini tutapambana nao,”alisema Omog ambaye
ndiye kocha anayelipwa mshahara mkubwa zaidi nchini.
Yanga yenyewe ipo katika hoteli ya Tansoma iliyopo
Gerezani, Kariakoo na inafanya mazoezi katika uwanja wenye vipara wa
Shule ya Sekondari Loyola, lakini huenda ikamkosa Mbrazil Andrey
Coutinho ambaye ana maumivu ya kifundo cha mguu huku mshambuliaji wake
mpya, Genilson Santos ‘Jaja’ akiwa fiti tayari kuwakimbiza mabeki wa
Azam, David Mwantika na Aggrey Morris.
Maximo alisema: “Azam ni timu nzuri imefanikiwa
kujijenga kwa kuwa na vifaa vya kutosha na benchi zuri la ufundi,
tunawaheshimu lakini kwetu sisi tunatambua ligi itaanza Septemba 20
lakini kwetu ligi tutaanza Jumapili dhidi ya Azam.
“Kila mchezaji wangu anajua umuhimu wa mchezo huo,
lakini pia kila mmoja anajua majukumu yake, hatuoni kitu kinachoweza
kutunyima ushindi, tunakwenda kupambana njooni muone nini tutakifanya
katika mchezo huo tunaamini itakuwa mechi nzuri.”
Waamuzi wa mchezo huo ni Simon Mbelwa (Tanga)
atakayepuliza kati kwa usaidizi wa Samuel Mpenzu (Arusha) na Charles
Simon (Dodoma).
Maximo atetea kujihami
Maximo amefafanua, anapenda kutumia viungo wengi katika timu ambayo ndiyo staili yake kama ulivyo mpira wa Kibrazili.
“Ni kweli tunashinda kwa mabao machache moja au
mbili hii ni kutokana na mfumo wangu ninaotumia kwa kuchezesha viungo
wengi. Napenda kuiimarisha timu kuanzia nyuma kwenye beki, viungo hadi
mbele,” alisema.
No comments:
Post a Comment