Wednesday, 10 September 2014
SIMULIZI TAMU YA BAHATI BUKUKU-12
ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA…
Alikuwa akisimulia jinsi alivyopata vipingamizi katika albamu yake ya kwanza kwa jinsi watu walivyokuwa wakiinua vikwazo katika maisha yake lakini baba yake alikuwa pamoja naye akimtia moyo.
ENDELEA…
Maisha yangu yalikuwa ya kawaida mno, kila siku niliendelea kumwabudu na kumwimbia Mungu. Niliyakumbuka maisha yangu ya nyuma na vile ambavyo vilitokea na kunipa changamoto.
Sikuacha kumtumikia Mungu kwa kuwa nilijua aliponitoa. Sikuishia kutoa albamu moja tu, niliendelea kutoa na nyingine zikiwemo Nani Aitikise Dunia, Ni Nyakati za Mwisho ambayo ilinipatia mafaniko makubwa na nyinginezo.
Niliendelea kupata jina makanisani, nilikuwa na furaha sana kila nilipokuwa nikikutana na mabinti na kuniambia kwamba walitamani siku moja wawe kama mimi, wamsifu Mungu katika roho na kweli.
Nikapata fedha kupitia muziki, sikuishia hapo kwa kuwa nilikuwa nikitaka kuwa na maisha mazuri kama walivyokuwa wengine, yaani kuyaona mafanikio ya kazi yangu, Mungu akanibariki na kunifanya kuwa kama nilivyokuwa.
Hata siku ambayo Mungu alinibariki kuwa na gari la kwanza, sikuamini, maskini mimi, eti naendesha gari langu tena likiwa limepatikana baada ya mafanikio makubwa.Nitamsifu Mungu milele, nilijisemea kila nilipokuwa nikiendesha gari langu.
Kupitia muziki wa Injili, nikaanza kufahamiana na wanamuziki wengine kama Christina Shusho, Rose Muhando, Flora Mbasha na wengine wengi.
Wakati nilipokuwa nikiendelea kupata mafanikio, shetani hakutaka kukaa mbali, kila siku alikuwa akiwainua watu wake ambao walikuja kinyume kwangu kwa ajili ya kuniangusha lakini hawakuweza.
Sikuwa mwanamke lelemama katika maombi, hiyo ndiyo silaha yangu kubwa ambayo niliibeba kila nilipokuwa.
Kuna kipindi nikawa sina maelewano mazuri na mume wangu. Sipendi kulizungumzia hili kwa sababu vyombo vya habari viliripoti sana japokuwa sikujua ni nani aliyekuwa akizivumisha stori zile.
Baada ya kuishi naye, kikafika kipindi ambacho kila kilichokuwa kikiendelea niliuona mwisho wa ndoa yetu ungekuwa nini. Katika hili ningependa kuwa mkweli kwamba kama ukija kwangu na kuniuliza nani alikuwa na tatizo ni lazima nitasema Daniel alikuwa na tatizo na hata ukimfuata Daniel na ukimuuliza nani alikuwa na tatizo, atasema ni mimi.
Katika hili, ili nisiweze kuharibu kitu chochote na kuonekana vibaya katika jamii, naomba nikae kimya kwa sababu namwamini Mungu anipae busara siku zote maishani mwangu.
Unapokuwa umeishi maisha na mwenzako halafu siku ikatokea kutofautiana na kujikuta upo peke yako, huwezi kuwa kama ulivyokuwa kipindi cha nyuma. Unapokuwa ndani ya nyumba, unajikuta upo naye, unapokuwa chumbani unajikuta upo naye, sasa mtu huyo anapoondoka, ni lazima hali itakuwa ni ya tofauti sana, haijalishi kama alikuwa akikufurahisha kila siku au kukuumiza, ni lazima kutakuwa na tofauti fulani.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwangu, siku za kwanza zilikuwa ni zenye mateso makubwa ila baada ya kipindi fulani Mungu akanisahaulisha na kila kitu kilichotokea, nikarudi katika hali ya kawaida na kuendelea na maisha yangu.
Nilipata mialiko mingi, Mungu aliendelea kufungua neema katika maisha yangu, sikuamini kwamba mwisho wa mateso makubwa, kudharauliwa shuleni, kuonewa na wenzangu mwisho wa siku ningeweza kuwa katika maisha ninayoishi sasa.
Jina langu likawa kubwa makanisani na sehemu nyingine na cha ajabu hata wale ambao hawakuwa wameokoka wakaanza kunifahamu.
“Mungu, hakika sauti yangu ni ya kukuimbia wewe tu, milele yote,” nilisema katika kila maombi niliyokuwa nikiyafanya chumbani kwangu.
“Uliniumba nikuabudu, hukuniumba nimuabudu shetani, kupitia hii sauti, nitataka watu waokolewe, kupitia hii sauti, nitataka wale watu wasiokujua basi waweze kukujua na kukuabudu milele yote.”
Mungu hakuishia hapo, anaendelea kunilinda mpaka leo hii na hata ajali iliyotokea wiki chache zilizopita Mungu alinionesha kwamba alikuwa akihitaji niendelee kuisambaza Injili kwa kutumia sauti hii aliyonibariki maishani mwangu
“Mungu akubariki Bahati, umekuwa muimbaji mzuri na kuisambaza Injili ya Mungu aliye juu, endelea kumtumikia katika maisha yako, Mungu atafanya mambo mengi katika maisha yako,” aliniambia Askofu Mkuu wa EAGT wa kipindi kile, Moses Kulola.
Maneno yake yalinitia nguvu, japokuwa alikuwa mtu aliyekuwa bize sana lakini kila nilipokutana naye alikuwa akinitia nguvu na hata kuniombea. Alitabiri mengi maishani mwangu na kunitia nguvu katika kila hatua ambayo nilikuwa nikipitia.
Mafanikio yangu yakabadilisha kila kitu. Kuna wale watu waliokuwa marafiki zangu wakanitenga lakini pia kulikuwa na wale maadui zangu, wakawa marafiki zangu wakubwa.
“Bahati, siamini kama umekuwa namna hii, upo tofauti na zamani, siamini kama ungeendelea kuwa na wokovu mpaka sasa hivi, maisha uliyopitia, mmh! Yakupasa kumshukuru Mungu milele,” aliniambia Neema, rafiki yangu niliyekuwa naye toka tulipokuwa shuleni.
Neema aliponiambia hivyo, nilimweleza kwamba kila kitu maishani mwangu kilitokea kwa mipango ya Mungu.Maisha yangu ya zamani yakabaki historia, kitabu cha maisha yangu ya nyuma kikafungwa, nikasahau kila kitu na kusonga mbele huku nikiwa nimetiwa nguvu upya.
Kwa wale walionitia nguvu katika kipindi chote cha matatizo, Mungu awabariki na hata wale walionitenga wakati wa matatizo na kuungana nami kwenye wakati wa raha, Mungu awabariki pia.
ASANTENI.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment