MANCHESTER, ENGLAND
KILA biashara ina masharti yake. Lakini biashara
ya Radamel Falcao kubaki jumla Manchester United inaweza kuwa rahisi tu.
Masharti yake ni rahisi kuliko ya mganga wa kienyeji.
Kwa mujibu wa habari za ndani za Old Trafford,
inadaiwa kuwa mkopo wa nyota huyo wa kimataifa wa Colombia unaweza kuwa
usajili wa muda mrefu kama tu atafanikiwa kucheza mechi 15 na kufunga
mabao matano.
Akifanikiwa katika hilo, United
italazimika kutoa dau la Pauni 35 milioni huku ikimlipa mshahara wa
Pauni 11 milioni kwa mwaka baada ya makato ya kodi, pia atajichotea
kiasi cha Pauni 2.4 milioni kama bonasi.
Falcao mwenyewe ana matumaini kuwa bodi ya United
itamchukua jumla baada ya mkopo wake wa Pauni 6 milioni kutoka Monaco
ambao utaisha Juni mwakani. Juzi Alhamisi alitambulishwa katika Uwanja
wa Old Trafford pamoja na kiungo Daley Blind aliyesajiliwa kwa Pauni 14
milioni kutoka Ajax.
“Natumaini nitabakia Manchester United kwa miaka
mingi na kuweka historia katika klabu hii. Nilipokuwa Porto na Atletico
Madrid siku zote nilipenda kuimarika na niliota kuchezea klabu kama hii.
Nataka kubaki hapa kwa miaka mingi,” alisema Falcao.
“Naona kwa sasa klabu ipo katika kipindi ambacho
kila mmoja anataka kumjua mwenzake. Lakini hapa kuna wachezaji wa hali
ya juu na wana akili sana na ambao wana uwezo wa kufanya kile ambacho
kocha anataka.
“Kuhusu suala la nitacheza wapi nadhani hilo ni
jambo ambalo kocha ataamua kwangu. Nimekuwa na bahati ya kucheza katika
klabu kubwa duniani kote katika mechi kubwa na fainali. Nimejikita
katika kufurahia soka langu na kutumia nafasi ambayo Manchester United
wamenipa.
“Siku zote huwa nina tabia ya kuweka malengo yangu binafsi, hilo ndilo ambalo wachezaji wanapaswa kujipa changamoto wenyewe.”
Staa huyo kwa msimu wa tano sasa hajafanikiwa kucheza katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Falcao anatarajiwa kuvaa jezi ya Manchester United
kwa mara ya kwanza kesho Jumapili katika pambano la Ligi Kuu England
dhidi ya QPR uwanjani Old Trafford.
No comments:
Post a Comment