Dodoma. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mizengo Pinda amesema kuwa nafasi hiyo siyo ya kuing’ang’ania
au kuililia kwa kuwa ni kama moto.
Pinda alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu
yaliyofanyika nyumbani kwake mjini Dodoma ambapo alieleza kuwa nafasi ya
uwaziri mkuu ina mambo mengi hasa yenye changamoto zikiwamo za kiuchumi
na ya kuondoa wananchi katika umaskini.
“Aah, uwaziri mkuu moto rafiki yangu,” alisema Pinda huku akicheka na kufafanua:
“Nafasi hizi za uongozi, Mungu wangu. Nafasi hizi za uongozi
zina mambo mengi, hasa mnapokuwa mnajaribu kumsaidia kiongozi wa nchi
kuongoza nchi ambayo ina changamoto nyingi hasa za kiuchumi.
“Kimsingi nchi yetu bado maskini, huku
tunahangaika kusaidia nchi tuondoke katika umasikini, lakini wakati
huohuo, uwezo wa kutuondoa, nayo ni changamoto.”
Pinda aliyekuwa akijibu swali lililotaka kujua
changamoto za nafasi yake ya uwaziri mkuu, alieleza kuwa changamoto ya
kwanza kwa nafasi hiyo ni namna ya kumsaidia Rais aweze kulivusha na
kuliondoa taifa katika dimbwi la umaskini na kuliweka kwenye hali ya
neema.
Alisema kuwa katika hali hiyo ndiyo sababu
Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imekuja na mpango unaoendelea wa kuweka
vipaumbele vichache kwa wakati na kuvipa umuhimu ili kuondoa umaskini na
kuwapeleka wananchi katika hatua nyingine zaidi kimaendeleo.
“Kazi siyo nyepesi kama inavyosemwa, lakini
ukimwezesha mwananchi anaweza kufanya vizuri katika mambo mengi; katika
elimu na afya, lakini kiutendaji siyo jambo rahisi.
“Changamoto kubwa ninayoiona ni namna ya kuwaondoa
wananchi katika dimbwi la umaskini, kiutendaji siyo kazi ndogo, lakini
lazima tufike huko. Bajeti ndogo, matatizo mengi, wizi, mimi hiyo naona
ndiyo changamoto ya msingi zaidi, hivyo ni lazima kuwa na vipaumbele
vichache,” alisema.
Akizungumzia majaribio ya wabunge kutaka kumng’oa
madarakani kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye, Pinda alisema
kuwa hali hiyo ni changamoto, lakini hakutishika kwa sababu anafahamu
nafasi aliyonayo siyo ya kung’ang’ania, bali ni dhamana tu.
“…Ni changamoto, lakini unajua uzuri wa vitu hivi,
nafasi hizi ni dhamana tu, kiongozi wa nchi anakuamini, anaamini
utamsaidia katika jukumu alilotaka, anakupa. Ukipewa siyo jambo la kufa
na kupona, siyo kitu cha kung’ang’ania, chako...chako...chako,”alisema
akiongeza:
“ Hii ni dhamana tu, siyo cha kufikiri ni kitu
chako, ndiyo maana sikutishika, lakini ni changamoto kwa maana kwamba
wenzako wanafanya wewe ubaini maeneo ambayo unatakiwa kuongeza nguvu
katika kuyatekeleza, tukifanya hivyo tutafika mbali.”
No comments:
Post a Comment