Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), leo kinafanya uchaguzi mkuu wa kumpata mwenyekiti
na makamu wenyeviti wake watakaokiongoza chama hicho kwa miaka mitano
ijayo huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa mwanasiasa mkongwe wa nchini
Kenya, Raila Odinga.
Mchuano katika nafasi ya uenyekiti ilitarajiwa
kuwa kati ya mwenyekiti anayemaliza muda wake, Freeman Mbowe na
aliyekuwa mwenyekiti wa mkoa wa Tabora wa chama hicho, Kansa Mbarouk
ambaye jana alitangaza kujitoa katika kinyang’anyiro.
Hivyo kujitoa kwa Mbarouk kuna maanisha kwamba nafasi hiyo
imebakisha wagombea watatu watakaochuana kuwania kiti hicho ambao ni
Daniel Luvanga na Gambaranyera Mongateo.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa
akizungumzia maandalizi ya Mkutano Mkuu wa chama hicho alisema kila kitu
kinakwenda sawa ikiwa ni pamoja na vikao vya Kamati Kuu na Baraza Kuu
ili kuandaa ajenda na kupitia majina ya walioomba kuteuliwa kuwania
nafasi mbalimbali za uongozi.
Gazeti hili lilikuwapo katika ukumbi wa Mlimani
City jijini hapa na kushuhudia wajumbe wakiendelea kujiandikisha huku
Kamati Kuu ikiendelea na mkutano wake kisha Baraza Kuu ikiwa ni kuweka
kila kitu katika hali ya ufanisi.
Katika uchaguzi huo kundi ambalo linatarajiwa kuwa
na ushindani ni la kuwania ujumbe wa kamati kuu ambapo hadi jana
waliokuwa wameomba kuteuliwa kuwania kuingia katika chombo hicho kikubwa
cha uamuzi walikuwa ni 58 kati ya nafasi hizo sita za Tanzania Bara na
mbili Zanzibar, huku wajumbe wake watachaguliwa kwa uwiano sawa wa
kijinsia.
Mbarouk akitangaza kujitoa katika kinyang’anyiro
hicho alisema hawezi kuwa miongoni mwa wanachama wanaoikiuka na kuivunja
katiba ya chama.
“Viongozi wetu wamekiuka katika ya chama,
nilimwekea pingamizi Mbowe kutokana na kutokuwa na sifa za kugombea
kwani ameongoza kwa miaka kumi jambo ambalo halimlazimu kuendelea tena,”
alisema Mbarouk na kuongeza:
“Hatua nitakazochukua nitakwenda kwa msajili kuomba ufafanuzi wa kifungu cha 6.3.2 C kuhusu ukomo wa uongozi”.
na hapo ndipo tutaona jinsi uongozi utakaopatikana utakuwa hautambuliki.”
Mbarouk alisema Chadema ni chama makini,
kinachojiandaa kushika dalo hivyo viongozi wake wanatakiwa kuheshimu
misingi ya katiba ya chama na si kutumia ubabe na ndiyo sababu
iliyomfanya kujitoa.
Katiba barua yake kwenda kwa Katibu Mkuu, Dk Slaa
ambaye alikiri kuipokea jana saa5.20 asubuhi Mbarouk alihitimisha kwa
kusema “Kwa mazingira haya sioni uwezekano wa kutendewa haki kwani
mazingira ya uchaguzi huru na haki hayapo.”
No comments:
Post a Comment