Matukio
ya mauaji ya watu wasio na hatia, yameendelea kuuandama Mkoa wa Geita,
kufuatia watu watatu kuuawa kwa kukatwa mapanga na kuchomwa mkukihuku mmoja akijeruhiwa baada ya mtu mmoja anayesadikiwa ni mgonjwa wa akili kutekeleza unyama wake. Tukio
hilo lililotokea jana asubuhi katika kijiji cha Nyamilyango wilayani
Geita, na aliyejeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita
ni Mathayo Sindamsanga, na hali yake imeelezwa ni mbaya. Mganga Mfawidhi
wa hospitali hiyo, Dk. Adam Sijaona, alithitibisha kupokea miili mitatu
iliyohifadhiwa hospitalini hapo pamoja na majeruhi mmoja.
Dk. Sijaona aliwataja waliouawa kuwa ni Pindo Makono, Ndakazi Bertha Masabile na Jacob Bukulu, ambao ni wakazi wa kijiji hicho.
Hata hivyo, mtu huyo aliyesababisha mauaji hayo, alikamatwa na wananchi wenye hasira na kisha kumfikisha kituo cha polisi.
Dk. Sijaona alisema
marehemu hao walifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi mwilini
kufuatia muuaji kutumia panga na kuwacharanga na kisha mkuki kuwatoboa
miili.
Akizungumzia tukio
hilo, Diwani wa Kata ya Bugulula, Elisha Lupuga, alisema lililotokea
juzi saa 1:00 jioni katika kitongoji cha Misheni katika kijiji cha
Nyamilyango baada ya mtuhumiwa, Rashid Ramadhani, mkazi wa kijiji hicho
kutumia mkuki na panga kuwaua watu hao.
“Dhamira yake mpaka
sasa haijafahamika ilikuwa nini, lakini amekuwa na tabia ya kuvuta bangi
kwa muda mrefu, hivyo tunahisi amevurugukiwa akili yake,” alisema
Lupuga.
Hata hivyo, Lupuga
alisema baadhi ya waliouawa walikuwa na mahusiano na mtuhumiwa, lakini
hakufafanua ni mahusiano ya namna gani waliyokuwa nayo.
Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alithibitisha kutokea tukio hilo na kwamba
mtuhumiwa anashikiliwa katika kituo cha polisi akisubiri hatua za
kisheria kuchukuliwa dhidi yake.
Tukio hilo limeibua
upya simanzi na vilio kwa wananchi wa mkoa huo ambao mara kwa mara
wamekuwa wakikumbwa na matukio ya mauaji ya aina mbalimbali.
Hilo ni tukio la pili ndani ya wiki moja baada ya usiku wa kuamkia Septemba 7, mwaka huu,
watoto wanne wa familia moja kuuawa kufuatia nyumba yao kuteketezwa na
moto katika kitongoji cha Elimu kata ya Kiangalala wilayani Geita.
Watoto walioteketea na
moto huo ni Reginald Robert (9) mwanafunzi wa darasa la nne na Sofia
(6) wa Shule ya Msingi Ukombozi na Remijius (4) wa chekechea pamoja na
Scolastika (15) aliyekuwa akisoma shule ya sekondari Mwatulole.
No comments:
Post a Comment