Watumiaji wengi wa huduma ya simu za mkononi wamekuwa wakilalamikia wizi wa pesa unaofanywa na baadhi ya makampuni hayo, leo katika kikao cha Bunge Dodoma Serikali imesema inatambua kuhusu wizi unaofanywa na baadhi ya makampuni ya simu za mkononi na
kutoa tamko namna ambavyo imejipanga kukabiliana na wizi wa aina hiyo.
Akitoa tamko hilo Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia
January Makamba amesema Serikali itaanzisha kituo maalum cha
kushughulikia malalamiko hayo CCC, kitakachokuwa kinasimamiwa na TCRA.
Akiuliza swali kuhusiana na jinsi Serikali ilivyojipanga kukabiliana na wizi huo Mbunge wa Konde Khatib Said Haji amesema; “…
Wizi huu unaofanywa na makampuni ya simu si wizi mkubwa kama ule wa
ESCROW.. ni wizi mdogo mdogo unaowaibia Watanzania elfu tano elfu tatu
lakini kwa ujumla wake, Mpemba aliyeko Konde akiibiwa elfu tatu,
Mnyamwezi wa Tabora elfu mbili, Ukizijumlisha ni mamilioni ya shilingi
wanaibiwa Watanzania… Leo watu hao elfu tatu elfu mbili unawaambia
wapeleke malalamiko yao, gharama hiyo umeikadiriaje hata mtu huyo akadai
malalamiko ya elfu tatu..”
“.. Hivi serikali yenu makini imekuwa wapi muda wote mpaka kukiri
kama Watanzania wamekuwa wakiibiwa na bila wenyewe kujijua?, na bado
hamna hatua mlizozichukua, ni nani aliyeko nyuma ya pazia hili la kuibia
Watanzania na ninyi mkaridhia ama ni yale yaliyosemwa kama CCM ina fund
katika wizi huu..?”- Khatib Said Haji.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia
January Makamba amesema; “…Napenda nikiri tatizo la wizi au dhuluma kwa
wateja lipo na ndio lililopelekea tukaweka hizi kanuni ambazo zinaweka
adhabu na hatua za kuchukua katika kuchukua katika kudhibiti wizi huo..
Licha ya utaratibu wa kawaida wa kulalamika katika makampuni ya simu,
kwa sababu moja ya matakwa ya sheria ni kwamba kampuni za simu zinapaswa
kuweka utaratibu wa kuhudumia watekja wake, lakini tumebaini kwamba
utaratibu huo una matatizo, unaweza ukapiga simu muda mrefu
isipokelewe, unaweza kuambiwa usubiri na wakati unasubiri kulalamika pia
unakatwa..
Kwa hiyo Serikali inafahamu hilo, pamoja na hatua tulizozichukua ni
kuweka ule mtambo wa kufuatilia mawasiliano ambao moja ya kazi yake sio
kufuatilia tu mapato lakini ubora wa mawasiliano.. Kwa kutambua kuwa
makampuni ya simu haya wakati mwingine yanachelewa wakati mwigine
yanapuuza wateja, kituo hiki ambacho tunakianzisha namba zake
zitasambazwa kila mtu atakuwa nayo, kwa hiyo huna haja kusafiri
kufuatilia shilingi elfu mbili elfu tatu elfu tano. Kutakuwa na namba
ambayo ni bure kupiga..”- January Makamba.
“ Kila utakapopiga kulalamika utapewa namba maalum ya lalamiko lako,
na lisiposhughulikiwa hata kitengo cha kampuni ya simu kutoshughulikia
lalamiko lako na yenyewe itakuwa sababu ya makampuni hayo kuadhibiwa..”-
January Makamba.
No comments:
Post a Comment