Benson Okumu, enzi za uhai wake akiwa na mtoto wa marehemu George Okumu Otieno ‘Tyson’ , Sonia.
Misiba
kila kona! Achilia mbali watu wasiokuwa na majina hasa vijana wadogo,
ndani ya saa 24 wamefariki dunia wasanii wanne wa kutoka kwenye tasnia
za Bongo Movies na Bongo Fleva, Amani lina habari yenye kuumiza moyo. HAWA HAPA
Matukio hayo yalitokea kati
ya Jumatatu jioni na Jumanne asubuhi ambapo kutoka kwenye tasnia ya
filamu waliotangulia mbele ya haki ni pamoja na Sherry Salum ‘Sheri
Magali’, Arafa na Benson Okumu Otieno.
Kwa upande wa Bongo Fleva,
Yessaya Ambikile ‘YP’, naye alitangulia mbele ya haki ikiwa ni siku
chache tu alionekana kwenye kumbi mbalimbali jijini Dar.
ALIANZA MDOGO TYSON
Jumanne jioni, gazeti hili
lilipokea kwa masikitiko kifo cha mdogo wa marehemu George Okumu Otieno
‘Tyson’ aitwaye Benson Okumu Otieno ‘Benii’ ambaye alifariki dunia baada
ya kupata homa kali na kuchanganyikiwa.Marehemu YP kutoka Kundi la TMK Wanaume Family enzi za uhai wake.
Babari za ndani zilieleza
kwamba Benii alianza kuumwa mkono kawaida ambapo alitumia dawa lakini
baada ya siku chache mkono huo ulianza kuvimba na kupata homa kali
iliyosababisha kwenda hospitali.
Ilielezwa kwamba Benii
alikwenda Hospitali ya Lugalo, Dar ambapo homa ile ilipanda kichwani na
kumfanya achanganyikiwe, mwisho akaaga dunia.
Baada ya msiba huo kutokea,
taratibu za kuusafirisha mwili kwenda kijijini kwao Kisumu nchini Kenya
zilifanywa nyumbani kwa mdogo wake wa kike maeneo ya Sinza-White Inn
jijini Dar.
Habari zilieleza kwamba
Benii alikuwa akifanya kazi za uongozaji wa filamu (director) ambapo
alifanikiwa kufanya filamu na wasanii mbalimbali.
Benii alianza kazi hiyo
alipofika jijini Dar akiwa anaishi na kaka yake, George Tyson
aliyefariki dunia Mei 30, mwaka huu kwa ajali ya gari iliyotokea maeneo
ya Gairo mkoani Morogoro.Marehemu Arafa aliyekuwa msanii chipukizi ndani ya Bongo Movies enzi za uhai wake.
“Jamani tatizo ni nini? Hata
maumivu ya kifo cha kaka yake hajaisha, jamani na Benii naye? Tumuombe
sana Mungu atuepushe na balaa hili la vifo,” alisema mwigizaji mkubwa
Bongo, William Mtitu.
ARAFA WA BONGO MUVI AFIA INDIA!
Huku na huku, wakati watu
wakitafakari kifo cha Benii na taratibu za kuusafirisha mwili wake,
ghafla ziliibuka habari nyingine mbaya kuwa chipukizi wa Bongo Movies
aliyetajwa kwa jina moja la Arafa naye aliaga dunia jioni hiyo ya
Jumatatu.
Habari zilieleza kwamba
Arafa, mtoto mzuri mwenye mvuto huku akiwa na umri chini ya miaka 20,
anadaiwa kupelekwa nchini India na mama mmoja kwa shughuli
binafsi.Ilielezwa kwamba, akiwa nchini humo aliumwa ghafla (ugonjwa
haukutajwa) ndipo akapoteza uhai hivyo taratibu za kuurejesha mwili wake
Bongo zinaendelea.Marehemu Sherry Magali wa Bongo Movies enzi za uhai wake.
YP NAYE AAGA DUNIA
Msanii YP kutoka Kundi la TMK Wanaume Family, naye aliaga dunia usiku wa kuamkia Jumanne wiki hii.
Habari kutoka kwa familia
yake zilieleza kwamba YP alianza kusumbuliwa na kifua tangu mwezi Machi,
mwaka huu ambapo alitibiwa na kuanza dozi.
Kwa mujibu wa mkewe, Sakina
Robert na dada yake Hawa Ambikile, YP alimaliza dozi mwezi Septemba,
mwaka huu ambapo hivi karibuni hali ilibadilika na kuwa mbaya
zaidi.Mkewe alisema alikimbizwa katika Hospitali ya Temeke, Dar ambako
alipatiwa matibabu hadi umauti.
Meneja wa TMK Wanaume
Family, Said Fela alisema msiba wa msanii huyo uliwekwa Keko, Dar
nyumbani kwa baba yake na alitarajiwa kuzikwa jana saa 10:00 jioni
kwenye Makaburi ya Chang’ombe jijini Dar.
Fela alisema kuwa YP
alifanya vizuri kimuziki wakati na msanii mwingine Y Dash ambapo
alisikika kwenye ngoma kibao kama Ulipenda Pesa na Pumzika.
MASKINI! ALIPANGA KUACHIA NGOMA MPYA
Ngoma nyingine nyingi
alifanya na TMK Wanaume Family kama Twende Zetu ya Chegge Chigunda, Dar
Mpaka Moro, Kichwa Kinauma na Tufurahi na tayari alikuwa amerekodi wimbo
wake mpya akiwashirikisha Tip Top Connection unaokwenda kwa jina la
Wazee wa Jiji aliopanga kuuachia mwezi ujao.
YP ameacha mke na mtoto mmoja wa kike mwenye umri wa miaka saba.
BURIANI SHERRY MAGALI!
Wakati pigo la TMK Wanaume
Family likiumiza, majira ya saa 6:00 mchana, siku ya Jumanne iliyopita,
ghafla kuliibuka habari nyingine mbaya kwenye Bongo Movies baada ya
kuondokewa na mwigizaji ambaye ni mchekeshaji, Sherry Magali.
Sherry Magali aliaga dunia
wakati akipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro
baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kifua na moyo kwa muda mrefu.
Jumamosi iliyopita
mwanahabari wetu alimtembelea wodi namba nane ambapo Sherry Magali
alisimulia namna alivyokuwa akipata maumivi makali nay a muda mrefu
tangu mwaka jana huku akionekana kudhoofu mwili na kukosa nguvu.
Baada ya kukutwa na umauti, msiba uliwekwa nyumbani kwao maeneo ya Mji Mpya mjini hapa kwa mzee Msafiri Ngedele.
Mazishi ya Sherry yalitarajiwa kufanyika jana kwenye makaburi ya Kola mjini hapa.
Enzi za uzima wake, Sherry
Magali alisifika kwa kuchekesha na lile umbo lake zuri lililokuwa
likiwatoa midume udenda.Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema
peponi-Mhariri.
Imeandaliwa na Hamida
Hassan, Chande Abdallah, Deogratius Mongela, Shani Ramadhan, Gladness
Mallya na Dustan Shekidele, Morogoro.
No comments:
Post a Comment