Kwanza niwaeleze wazi kuwa wivu ndiyo chanzo kikubwa cha kuvunjika kwa ndoa au uhusiano wa kimapenzi. Hii hutokana na kufumaniana. Mtu mwenye wivu kwa mwenzake hatulii katika kumchunguza. Kila akipata nafasi, atachukua simu yake na kuanza kuangalia majina au sms.
Kama ni mwanaume, ataanza kukagua majina ya kiume kwenye simu ya mke au mpenzi wake. Atakapoliona lenye kutilia shaka, ama anaweza kuuliza huyu ni nani au atapiga mwenyewe na kuuliza uhusiano wa aliyempigia na mkewe. Na ikiwa ni mwanamke, naye atakuwa na tabia kama hiyo kwenye simu ya mtu wake.
Licha ya kukagua majina, lakini pia anapitia sms zilizoingia na kutoka, akizipata anazozitilia mashaka, mambo nayo yanabadilika. Baadhi ya wenye wivu, hutuma sms za matusi kwa anayemhisi bila kuwa na uthibitisho wowote. Wengine hufuta namba zote walizo na mashaka nazo.
Matokeo ya hali kama hii, ni vurugu. Kama mke atamhisi mumewe kutembea na mfanyakazi mwenzake, iko siku anaweza kutoka nyumbani na kwenda kuleta vurumai kazini kwa mumewe. Kwake yeye, anaamini analinda na kutetea chake, lakini kwa upande mwingine, anamharibia mwenzake kazini.
Inapotokea hivi, kila mtu anajua kinachoendelea. Mume aliyeletewa vurugu kazini hawezi kukubali, ataona mkewe amemdhalilisha na kumuaibisha.
Kule kwenye simu nako kwa mfano, mke au mume anapofuatilia sms na simu za mwenzake, mwisho wa siku ni kelele, ambazo kwa vyovyote hazina matokeo mazuri.
Lakini kama mtu ataweka wivu mbali kwa mtu wake, anapunguza sehemu kubwa ya hatari ya ndoa au uhusiano wake kuvurugika. Jambo moja la msingi kukumbuka ni kwamba, kadiri mizozo na misuguano inavyokuwa mingi, ndivyo uwezekano wa kutengana unavyozidi.
Kutokuwa na wivu hakumaanishi haupendi. Unampenda lakini unajitahidi kumpa nafasi ya yeye kukuheshimu. Watu wengine huamua kusaliti kwa sababu ya hasira, hufanya kama wanakomoa kwa sababu mtu unajijua hufanyi lolote, lakini mwenzako kila siku kelele.
Kudumu kwa ndoa au uhusiano ni pamoja na kila mmoja kukubali kuamini juu ya nyendo za mwenza wake. Inapotokea umefumania, iwe ni bahati mbaya sana, ambayo hata aliyefumaniwa atajisikia vibaya, lakini siyo kufumania kwa kulazimisha.
Ukiwa hujishughulishi naye kwa kiwango kile, hata yeye unampa wasiwasi, anakuwa mgumu kuamini kama unampenda kweli, hivyo atazidisha umakini ili asije akawa chanzo!
No comments:
Post a Comment