Kwa muda mrefu sasa, Bunge la Afrika Mashariki (EALA), limekuwa
katika mizozo isiyoisha kiasi cha wananchi wengi katika nchi wanachama
kuhofia kwamba Bunge hilo litasambaratika. Tulishuhudia mara kadhaa
miezi michache iliyopita mizozo mikubwa ikiibuka, ikiwa ni pamoja na ule
wa ya wabunge kutoka katika baadhi ya nchi wanachama kususia vikao
wakipinga utaratibu wa vikao vyote kufanyika katika makao makuu ya
jumuiya hiyo yaliyopo jijini Arusha, Tanzania.
Kama siyo busara za wakuu wa nchi wanachama, mzozo
huo ungelisambaratisha Bunge hilo. Utaratibu mpya uliwekwa kwa
kuboresha kanuni husika ili kuwezesha vikao hivyo kufanyika kwa mzunguko
katika kila nchi mwanachama. Mgogoro huo ulimalizika pasipo kutokea
madhara makubwa kisiasa, ingawa ulisababisha madhara makubwa kiuchumi
kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kutokana na kugharimia safari,
malazi na posho za wabunge hao wanapokuwa nje ya kituo chao cha kazi
kilichopo jijini Arusha.
Katika kupigania utaratibu huo mpya wa kufanyia vikao katika
nchi zote wanachama wa EAC, wabunge hao walijenga dhana kwamba hatua
hiyo ingeongeza ufanisi katika shughuli za Bunge hilo. Kinadharia,
walijenga taswira ya Bunge linalowajibika, linalopigania masilahi na
maendeleo ya wananchi wa Afrika Mashariki. Kumbe walichoficha nyuma ya
pazia ni kwamba walitaka starehe na matanuzi katika hoteli za kitalii
katika majiji ya nchi wanachama, kwani sasa imethibitika kwamba wengi
walikuwa hawahudhurii vikao vya Bunge hilo na mara nyingi Spika
Margareth Zziwa alikuwa akilazimika kuahirisha vikao kutokana na
kukosekana kwa akidi.
Jambo la kushangaza ni kuwa, hata ilipofika zamu
ya Tanzania kuwa mwenyeji wa kikao cha Bunge hilo mwishoni mwa mwezi
uliopita, walikataa kukutana Arusha palipo na huduma zote za shughuli za
Bunge hilo na kumlazimisha Spika Zziwa kuhamishia vikao vyake jijini
Dar es Salaam, pasipo kujali gharama ambazo zingetokana na hatua hiyo.
Tulishuhudia Serikali ya Tanzania ikihaha na kutumia fedha za kodi za
wananchi kukarabati Ukumbi wa Karimjee ili Bunge hilo liweze kufanyia
vikao vyake, ingawa ukumbi huo haukuwa na hadhi ya kufanyia vikao hivyo.
Kilichotokea wakati Bunge hilo lilipoanza vikao
vyake hapa jijini ni kichekesho cha mwaka. Wabunge wengi walikuwa watoro
na kulifanya Bunge kuahirishwa zaidi ya mara mbili kutokana na
kukosekana kwa akidi. Huo ndiyo umekuwa utamaduni wao na tukijiuliza
wamefanya nini tangu waingie katika Bunge hilo zaidi ya miaka minne
iliyopita hatuna jibu, kwani wengi wao wamejielekeza katika starehe na
kusahau kilichowapeleka katika chombo hicho. Wakati wakijieleza katika
mabunge ya nchi zao waliapa kufanya kazi kwa kujituma, kujitolea na
kusimamia masilahi ya nchi zao. Nini kimetokea mpaka wakawasaliti
wananchi wao ni kitendawili ambacho ni vigumu kukitegua.
Tutakuwa hatukosei tukisema wabunge wengi wa Bunge
hilo wameharibiwa na tamaa za kidunia, kwa maana ya ubinafsi na
kutafuta ‘utukufu’. Tulishuhudia jinsi walivyokuwa wamejipanga kumwondoa
madarakani Spika Zziwa kwa kukataa ufisadi wa kuwalipa posho bila
kuhudhuria vikao na pia kukataa madai yao ya kutaka kupewa nyongeza nono
za mishahara kinyume na kanuni za fedha za jumuiya hiyo. Ni Bunge
ambalo hakika wajumbe wake wengi siyo tu wamepoteza mwelekeo, bali pia
wamepoteza uhalali wa kuwawakilisha wananchi waliowapatia ‘utukufu’ huo.
No comments:
Post a Comment