"Sitamwaacha binti yangu ateseke kama mimi ninavyoteseka nikiwa katika siku zangu. Familia yangu inafanya nijihisi najisi.
"Siruhusiwi kwenda jikoni, Siwezi kuingia hekaluni, Siwezi kukaa na wengine."
Kuna
hisia ya dhamira katika sauti ya Manju Baluni mwenye umri wa miaka 32.
Nilikutana naye katika kijiji cha Uttarakhand, jimbo lenye miinuko
kaskazini mwa India.
Nchini
India,kuna ukimya kuhusu suala la afya ya wanawake, hususan wawapo
katika siku zao. Kuna mwiko uliojikita katika jamii hizi kuhusu suala la
mwanamke awapo katika hedhi: wanawake si wasafi, wachafu, wagonjwa na
wakati mwingine wamelaanika katika kipindi hicho.
'Wasiwasi na Mashaka'
Watu wanaamini kuwa wanawake wanaokuwa katika hedhi hawatakiwi kuoga na wana upungufu wa damu.
Uchunguzi
wa hivi karibuni wa kampuni ya kutengeneza taulo maalum za kujisitiri
kina mama wanapokuwa katika hedhi umeonyesha kuwa asilimia 75% ya
wanawake wanaoishi mijini bado wananua taulo hizo zikiwa zimefungwa
katika mifuko au gazeti ili kutoonyesha kilichomo ndani kwa sababu ya
aibu inayohusishwa na hedhi.
Na kamwe hawawaombi wanaume katika familia kuwanunulia taulo hizo maalum.
Nimekulia katika nyumba yenye wanawake wengi, lakini bado hatuwezi kujadili kwa uwazi suala hili ambalo ni la kawaida.
Wasichana
wanajifunza kuficha nguo zao wanazotumia wawapo kwenye hedhi kwa
wanaume baada ya kuzifua, anasema Rupa Jha. Mama yangu alitumia mashuka
makuu kuu na kuzificha katika sanduku, tayari kwa kutumiwa na mabinti
zake wanne.
Changamoto
kubwa ni namna ya kukausha vipande hivyo vya nguo. Nina kumbukumbu za
kuhisi wasiwasi na mashaka juu ya mchakato mzima.
Nilifundishwa
mbinu nadada zangu wakubwa - namna ya kuficha nguo zenye madoa ya damu
chini ya nguo nyingine bila ya mwanaume yeyote kugundua. Hatukuthubutu
kuziacha peupe kwenye jua ili zikauke kabisa.
Nilihisi 'mchafu sana'
Matokeo ni kwamba kamwe hazikukauka vizuri, ziliacha harufu ya uvundo. Nguo hizo zisizo safi zilitumika tena na tena.
Ukosefu
wa maji ulifanya kazi ya ufuaji kuwa ngumu na isiyo na usafi. Hali hiyo
haijabadilika sana tangu wakati huo kwa wanawake wengi wa Kihindi.
Uchunguzi
mwingi uliofanyika siku za karibuni umeonyesha kuwa mila hizi
zimesababisha madhara makubwa ya kiafya. Imeripotiwa kuwa mmoja kati ya
wasichana watano nchini India anaacha masomo kutokana na kadhia ya
hedhi.
Baadhi
ya wasichana wanaacha kwenda shule wawapo katika kipindi cha hedhi.
Margdarshi mwenye umri wa miaka kumi na mitano anaishi katika kijiji cha
ndani cha Uttarakashi.
Anapenda
kwenda shule japo inamaanisha safari ngumu akipita katika eneo lenye
vilima vikali. Kamwe hajawahi kukosa masomo, isipokuwa kwa mwaka jana
wakati ambapo nusura aache masomo baada ya kupata siku zake kwa mara ya
kwanza.
"Tatizo
kubwa kuliko yote ilikuwa namna ya kukabiliana na hali hiyo. Bado lipo.
Najisikia kufedheheshwa, hasira na mchafu sana. Mwanzoni niliacha
kwenda shule."
'Suala la kibinadamu'
Anataka
kuwa daktari na anashangaa kwa nini wavulana katika darasa lake wakati
wa somo la elimu ya viumbe(baolojia) wanacheka sana mwalimu anapoelezea
njia ya hedhi.
"Nachukia.
Natamani tungekuwa huru zaidi na kujisikia huru tunapozungumzia suala
hili. Hali hii inatokea kwa kila mwanamke kwa hiyo kuna nini cha
kuchekesha hapo?"
Anshu
Gupta, mwanzilishi wa shirika lisilo la kiserikali, Goonj, anahisi kuwa
tatizo hili limejikita katika ukweli kwamba linahusishwa na wanawake.
Nchini
India wanawake wanatumia taulo za kujihifadhi wakati wawapo katika siku
zao kwa kutumia nguo kuu kuu. "Si suala la wanawake pekee. Ni suala la
kibinadamu lakini tumelibagua. Baadhi yetu tunataka kuondokana na
utamaduni huu wa kuona aibu na kunyamaza. Tunahitaji kuvunja utamaduni
huu."
Shirika hili linafanya kazi katika majimbo 21 kati ya 30.
Shirika
hili pia linatengeneza taulo rahisi kutokana na nguo zilizochakatwa
upya ili kuwasaidia asilimia 70% ya wanawake wa India ambao hawawezi
kupata taulo salama na safi.
Muhimu zaidi, wanaanza kuzungumzia suala hili. Bila kuhisi kufedheheka.
Makala
ya BBC ya BBC's 100 Women yamekuwa yakitangazwa katika mtandao, katika
televisheni na radio ya Idhaa ya Dunia tangu Oktoba 27-29. Changia maoni
yako katika mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter, ukitumia alama
#100Women.
No comments:
Post a Comment