Na Mwandidhi Wetu, Dodoma
BENKI
ya Posta Tanzania (TPB) kupitia tawi lake la Dodoma, imejenga madarasa
mawili pamoja na ofisi ya walimu katika Shule ya Msingi Msenjelele ikiwa
ni jitihada zake za kukuza elimu nchini na kupambana na madhari ya
ujinga na umaskini kwa Wananchi wa Kijiji cha Chunyu Mpwapwa.
Akikabidhi
msaada huo katika Kijiji cha Chunyu Mkoani Dodoma jana, Ofisa Mtendaji
Mkuu wa Benki ya Posta Tanzania (TPB), Sabasaba Moshingi alisema benki
yake ilichukua jukumu la kusaidia ujenzi wa madarasa hayo na ofisi ya
walimu baada ya kuguswa na kitendo cha wanafunzi kutembea umbali mrefu
hasa wale wenye umri mdogo kutembea umbali mrefu kwenda kijiji jirani
kuifuata huduma ya elimu.
Alisema
TPB iliguswa na umbali wa zaidi ya kilomita 12 ambazo wanafunzi
walilazimika kutembea kila siku kwenda shuleni kijiji cha jirani na
Kijiji cha Chunyu. Alisema mara baada ya kupokea ombi lakusaidia ujenzi
huo toka kwa uongozi wa Kijiji cha Chunyu walikubali na kuanza ujenzi
huo.
Alisema
ujenzi huo wa madarasa pamoja na ofisi ya walimu yaliojengwa kisasa
umeigharimu Benki ya Posta Tanzania kiasi cha shilingi milioni 50, hivyo
kuwaomba wanafunzi na wananchi wa eneo hilo kuyatunza na kuyatumia
vyema ili yaweze kudumu kwa muda mrefu.
Kwa
upande wake Mbunge wa Mpwapwa Gregory Teu, akipokea msaada huo wa
majengo aliishukuru Benki ya Posta Tanzania kwa moyo wao wa ukarimu na
upendo waliouonesha kwa wananchi wa Kijiji cha Chunyu ambao walikuwa
wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa.
Alisema
kwa upande wake alikuwa akiguswa na kero hiyo ya wananchi wake
waliyokuwa wanaipata hivyo kuamua kutafuta ufadhili wa kujengewa
madarasa kutoka kwa taasisi mbalimbali. "..Naishukuru Benki ya Posta kwa
kuitikia wito huo mara moja na bila kusita," alisema Mbunge huyo.
Alitoa
wito kwa wanakijiji cha Chunyu kuhakikisha watoto wao wanakwenda shule
sasa na kufuatilia maendeleo yao ili kukuza ufaulu na kujenga kizazi
chenye msingi mzuri wa elimu watakao kuja kuwa viongozi bora wa kesho.
No comments:
Post a Comment