Mohamed Abdallah Kiumbe,'Chif kiumbe' mwenye kanzu yanjano.JINA
alilopewa na wazazi wake ni Mohamed Abdallah Kiumbe, lakini baada ya
mihangaiko yake huku na kule, akipiga hatua taratibu za maendeleo,
akajikuta amepata umaarufu mkubwa mno, sasa akijulikana kama Chief Kiumbe.
Ninamfahamu kiasi huyu jamaa, ni mchangamfu, mtu wa watu, lakini
usisahau, ni kijana wa kisasa. Enzi hizo ukikutana naye kwenye kumbi za
starehe, huwezi kumtofautisha na wasanii wa kileo kwa mavazi yao, pamba
kali, mikufu ya dhahabu shingoni na mikononi na utitiri wa wapambe.
Kila anayepita kwenye anga zake lazima anukie ua waridi. Amewasaidia
watu wengi sana, hasa wasanii wa muziki wa dansi na Bongo Fleva.
Amewasimamia baadhi ya watu wenye majina makubwa kama Profesa Jay, Q
Chilla, Hussein Machozi, Matonya na wengine wengi.
Kwa taarifa ya ziada, ndiye mhimili mkubwa wa mafanikio ya Extra
Bongo. Kama kuna watu ambao Ally Choki hawezi kuwasahau anapoizungumzia
bendi yake, basi ni huyu jamaa.
Ndiyo maana ni jambo la kawaida kusikia jina lake likitajwa kwenye nyimbo. Ndiye kiunganishi kikubwa cha wasanii wa muziki wa kizazi kipya wanaopata shoo nchini Kenya, hasa Mombasa.
Na nadhani utafahamu mtu mwenye pesa, anayezitoa pasipo shida na
anayekesha kwenye majumba ya starehe, akiwapigisha mitungi wapambe wasio
na idadi, atakuwa ni wa aina gani!
Lakini habari nzuri zaidi kuhusu Chief Kiumbe ni kwamba sasa amerudi
kwa Mola wake, kama angekuwa Mkristo, tungesema ameokoka, lakini kwa
Waislamu, labda tuseme amekuwa swala tano.
Anasali na msikiti wake mkubwa ni Masjid Jidda, uliopo Sinza, mitaa ya LionHotel.
Kama nilivyosema awali, kwa mtu aliyekuwa na maisha ya aina yake, ni
ukombozi mkubwa kusikia sasa amekuwa mtu wa kuswali. Bila shaka amebaini hakuna alilobakiza kulifanya baada ya Mungu kumpa mafanikio, isipokuwa kumrejea na kumshukuru!
Nimeandika kuhusu Chief Kiumbe ili kupata nafasi ya kuzungumza na
mapedeshee wengine, ili nao waangalie uwezekano wa kurejea kwenye nyumba
za ibada, kama shukurani kwa mafanikio waliyopata.
Wengi tunawaona ‘wakichezea’ pesa kwa kuwatunza wasanii majukwaani,
wakiishi maisha ghali, majumba ya kifahari na magari yenye thamani.
Wanajisikia zaidi kusifiwa na binadamu wenzao, lakini wanasahau kuwa
aliyewapa ni Mungu.
Wapo watu tunawajua, kuacha milioni moja au mbili katika ukumbi mmoja
siyo jambo la ajabu. Anaingia Mango Garden na wapambe, anaanza kugawa
hela kwa wanamuziki, wacheza shoo, kisha anawageukia marafiki na watu
maarufu.
Baada ya hapo anapanda gari anakwenda Msasani Club nako anafanya
hivyohivyo kabla ya kumalizia siku Mzalendo Pub ambako balaa
linaendelea. Ukijaribu kumpigia hesabu, unaona kitu kama shilingi
milioni nne hivi na ushee zinaondoka kwa siku kwa staili hii ya maisha.
Hayo ndiyo maisha yake ya kila siku. Kama hakuna dansi, anakwenda
club na huko nako mambo ni yaleyale. Kama umepata pesa na unazitumia
namna hii, ni jambo baya kufikiri ni ujanja wako.
Nyuma ya harakati zako, yupo Mwenyezi Mungu anakusimamia. Hata kama
unazipata kwa utapeli, misheni tauni au biashara halali, bado unapaswa
kumshukuru yeye aliye juu kwa sababu wengi tu wamejaribu kufanya kama
wewe ulivyofanya, lakini hawakufanikiwa na bado wanakwenda kwenye nyumba za ibada.
Kuna watu wana hela, hawajionyeshi, wanasaidia watu wasiojiweza na
makundi yenye uhitaji, lakini ni watu wenye kushiriki sana sala kwa
imani zao.
Nimalize kwa kusema kwamba, kwa hili Chief Kumbe amewazidi ujanja
mapedeshee wenzake na Inshaallah Mwenyezi Mungu amzidishie kama
alivyowahi kusema Q-Chillah.
No comments:
Post a Comment