Kamati za ulinzi na usalama kutoka wilaya za Mkinga na Korogwe zimelazimika kufanya operesheni maalum kwa kutumia silaha za moto katika msitu wa hifadhi wa Bombo magharibi uliopo mpakani mwa wilaya hizo mbili kufuatia baadhi ya raia wa Kenya kufanya uvunaji haramu wa miti aina ya Mikarambati kisha kuanzisha viwanda vidogo vya kutengeneza bidhaa aina ya vinyago ambavyo huuzwa zaidi katika nchi za ulaya kupitia nchini Kenya.
Operesheni hiyo imesababisha kubainika kwa viwanda vidogo vya
kutengeneza vinyago katikati ya msitu wa hifadhi Bombo magharibi na
kukuta shehena ya vinyago ambavyo vimeanza kutengenezwa na watuhumiwa
kisha kusafirishwa kupelekwa katika mashine maalum za kusafisha na
kutengeneza vinyago zilizopo nchini Kenya baada ya watuhumiwa kutoroka
kwa madai kuwa viongozi wa serikali ngazi za kata na vijiji
vinavozunguka msitu wanashirikiana nao.
Hata hivyo baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa kushirikiana na
wavunaji haramu wa msitu huo wa Mikarambati kutoka nchini Kenya
walipoulizwa kuhusu tuhuma hizo wamesema kwamba wamekuwa wakitoa taarifa
kwa viongozi ngazi za kata hadi wilaya lakini zimekuwa hazifanyiwi kazi
hatua ambayo imewafanya na wao kuacha msitu huo uvunwe kwa kuhofia
maisha yao kwa sababu baadhi ya watuhimiwa wana silaha za moto.
Hata hivyo mkuu wa wilaya ya korogwe bwana mrisho gambo pamoja na
afisa misitu wa wilaya ya mkinga bwana frank chambo wameahidi
kulifikisha suala hilo katika ngazi ya mkoa na taifa kwa ujumla kisha
kufunga shughuli za kibinadamu za msitu huo ambazo zinafanywa na baadhi
ya wakazi wanaoishi pembeni mwa hifadhi ya msitu huo.
No comments:
Post a Comment