Dar es Salaam. Mbunge wa Kawe, Halima Mdee amechaguliwa kwa
kishindo kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha)
kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Suzan Lyimo.
Mkutano Mkuu wa Bawacha wa uchaguzi ulifanyika
katika Ukumbi wa Mlimani City jijini hapa na ulianza juzi asubuhi na
kuhitimishwa jana asubuhi.Msimamizi wa uchaguzi huo, Arcado Ntagazwa akitangaza matokeo hayo jana
alisema, Halima Mdee amepata kura 165 dhidi ya wapinzani wake sita ambao
ni, Lilian Wasira kura (11), Chiku Abwao (15), Sophia Mwakagenda (18),
Rebeka Magwisha (14) na Janeth Rither(35).
Kwa upande wa nafasi ya makamu mwenyekiti bara, Ntagazwa
alimtangaza Hamida Abdalla aliyepata kura 125 dhidi ya Mariam Msabaha
aliyejikusanyia kura 66 katika uchaguzi ulioingia ngwe ya pili baada ya
kwanza kukosekana mshindi kutokana na kutofikisha asilimia 50 ya makamu
mwenyekiti katika kura zilizopigwa. Naye Hawa Mwaifunga aliibuka mshindi
wa nafasi ya makamu mwenyekiti bara kwa kupata kura 136 dhidi ya kura
99 alizopata Victoria Benedict katika uchaguzi uliorudiwa mara ya pili
baada ya awali kushindwa kumpata mshindi.
Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe akizungumza mara
baada ya kutangazwa mshindi jana asubuhi alianza kwa kuwashukuru
wanawake wote waliompigia kura na hata wale ambao hawakumchagua kwani
walitumia demokrasia yao.
“Wanawake tutaweza kusonga mbele kama tukipendana
kwani uwezo, nguvu na nia tunazo, siri ya kuingia Ikulu mwaka 2015 ni
kuwa na wanawake wengi ndani ya Bawacha lakini watakaokipigania chama,”
alisema Mdee na kuongeza:
“Viongozi tuliochaguliwa tunatakiwa kushughulikia
matatizo ya wanawake ili waweze kutuamini kwani taifa linatutegemea na
tusiruhusu rushwa iwe kwetu.”
Kuhusu malengo ya Bawacha kwa siku za usoni Mdee
alisema kwa kipindi cha miezi miwili watafanya operesheni kubwa nchi
nzima ya kutoa elimu kwa wanawake waweze kujiunga na chama hicho ili
kiweze kuwa na mizizi kuanzia ngazi za chini.
“Operesheni tutakayokwenda kuitangaza kuanza
itakuwa kubwa, tutakwenda hadi ngazi za chini kabisa, tutawahamasisha
wasichana wadogo ambao wamekuwa wakihofu kujiunga na vyama vya saisa
hasa vya upinzani waweze kujiunga,” alisema Mdee.
Juzi viongozi wapya wa Baraza la Vijana la chama
hicho (Bavicha) waliochaguliwa ni mwenyekiti, Paschal Patrobas, Makamu
mwenyekiti bara, Patrick Ole Sosopi, Makamu mwenyekiti Zanzibar, Zuedi
Abdullah.
Katibu Mkuu ni, Julius Mwita, Naibu Katibu Mkuu
Zanzibar, Omary Othuman Nassor na Naibu Katibu Mkuu Bara ni Getruda
Ndebalema na mtunza hazina amekuwa Evelin Meena.
No comments:
Post a Comment