Msanii wa sinema za Kibongo, Wema Sepetu.
JAMAA wawili, mmoja fundi umeme, Rashid
Balazi na Juma Bushiri wanadaiwa kunusurika kifo baada ya kutekwa na
kusulubiwa nyumbani kwa msanii wa sinema za Kibongo, Wema Sepetu
wakituhumiwa kukwapua simu ya bei mbaya ya mpambe wa mwanadada huyo,
Petit Man, Amani limeichimba kwa kina.
Rashid Balazi akiwa na jeraha begani baada ya kutekwa na kupigwa.
Wakielezea mkasa huo wa
kutisha uliojiri mwishoni mwa wiki iliyopita nyumbani kwa Wema, Mtaa wa
Bwawani, Kijitonyama jijini Dar, manusura hao walisema siku ya tukio
waliitwa nyumbani kwa Wema na mdogo wake aitwaye Bite kwa ajili ya
kutengeneza mota ya kusukuma maji.Walisema walifika nyumbani hapo na
kuangalia mota hiyo ambapo waligundua kwamba haikuwa na tatizo bali
mushkeli ilikuwa kwenye bomba la maji.WAOMBA FEDHA YA MANUNUZI
Walisimulia kwamba, baada ya kugundua hilo waliomba fedha kwa Bite kwa
ajili ya kwenda kununua bomba, wakapewa shilingi elfu arobaini.“Lakini
kabla hatujafika kunakouzwa mabomba tulipigiwa simu na Bite kwamba
tunatakiwa kurudi kwa kuwa kuna tatizo.
PF 3 aliyopewa bwana Rashid Balazi kwa ajili ya kwenda kupata matibabu.
“Tulirudi na kumkuta Petit Man akiwa na mlinzi. Petit Man alisema eti
sisi tumemuibia simu yake ya bei mbaya aina ya Iphone 6, hivyo
tunatakiwa tuirudishe. “Tulimwambia hatukuchukua simu lakini akasisitiza
ni sisi, akasema tutairudisha tutake tusitake.
“Tulipoona tumevaa msala wa uongo tulimwambia atupeleke polisi,
akasema atawaita makamanda wake ambao ni ‘mbwa mwitu’ waje watuoneshe
kazi. Lakini kabla ya kuwaita makamanda wake, alimwita mganga wa
kienyeji. “Mganga alifika akaangalia kwa darubini zake akasema simu
hatujaiba sisi, lakini Petit Man hakutaka kumwelewa.
“Wakati huo alikuwa bado ametufungia ndani tusitoke, ghafla wakafika
hao makamanda wake, hatukuwahesabu lakini walikuwa wengi, wakatuteka na
kutufunga kabla ya kuanza kutusulubisha wakidai wao ni ‘mbwa mwitu’.
Jamaa walitupiga kipigo cha mbwa mwizi....”
SILAHA ZATUMIKA
Juma Bushiri akiuguza majeraha yake aliyoyapata baada ya kutekwa na kuteswa.
“Walikuwa wakitumia silaha mbalimbali kama viwembe, visu na fimbo
kisha baadaye walitumwagia maji ya moto. Kimsingi walitufanya kama
vibaka wanavyofanyiwa wakikamatwa.
“Kama hiyo haitoshi, Petit Man aliwaita mabaunsa wawili ambao walitutesa na kutuvua nguo tukabaki kama tulivyozaliwa.
PETIT MAN MBARONI
“Kipigo kilipozidi majirani
walisikia kelele na kuja kuchungulia ambapo walikimbilia kwa mjumbe wa
nyumba kumi na kumpa taarifa, yeye akaja kutuokoa na kutupeleka polisi
huku wakati huo difenda la polisi nalo likawa limeshafika na kumtia
mbaroni Petit Man na baadhi ya watesaji hao na kwenda kuwasweka mbaroni
kwenye Kituo cha Polisi Kijitonyama ‘Mabatini’ lakini wengine
walikimbia.”
Baadhi ya majeraha aliyoyapata Juma Bushiri.
WEMA ATOKA
“Wakati zogo hilo linaanza, Wema
alitoka na kumwambia Petit wawahi uwanja wa ndege (Julius Nyerere, Dar)
kwani walikuwa na safari (walikuwa wanakwenda nchini Ghana).
“Wema na Petit Man waliondoka na kuamuru kwamba tuwasubiri hapohapo tusiondoke.”
KIPIGO SAA 6:00 MCHANA HADI 9:00 ALASIRI
“Walipofika uwanja wa ndege wakawa wamechelewa ndege, Wema hakurudi
nyumbani ila Petit Man alirudi ndipo tukaanza kupigwa kuanzia saa 6:00
mchana hadi saa 9:00 alasiri,” walieleza jamaa hao wakiwa hoi kwa kipigo
cha shetani.
MAJERAHA
Katika tukio hilo, Juma alipata
majeraha kibao mwilini ambapo anatembea na mkongojo huku Rashid akiwa
amechanwa na kisu mgongoni, mguuni na mbavu moja ikiwa imepata ufa na
wote hao walipelekwa kwenye Hospitali ya Sinza-Palestina, Dar.Baadaye
Rashid alihamishiwa Mwananyamala kufuatia hali yake kuwa mbaya.
WEMA ATINGA KITUONI NAYE ATUPWA LUPANGO
Siku ya
kwanza Petit Man alilala kituoni ambapo kesho yake Wema alitinga, naye
akatupwa lupango kisha kuchukuliwa maelezo kabla ya baadaye wote
kuachiwa ambapo Petit Man alitoka kwa dhamana.
Hata hivyo, washitakiwa hao na walalamikaji walitakiwa kuripoti
kituoni hapo Jumatatu iliyopita lakini walalamikiwa walikiuka amri ya
polisi, hawakuonekana kwa madai kwamba wamesafiri kikazi kwenda nchini
Ghana.
SHAMBULIO LA KUDHURU MWILI
Kwa mujibu ya shitaka
lililofunguliwa kituoni hapo, Petit Man anakabiliwa na tuhuma za
kudhuru mwili katika jalada la kesi namba KJN/RB/11250/2014 na
KJN/RB/11220/2014 -SHAMBULIO LA KUDHURU MWILI.
Petit Man anayeshtakiwa kwa kosa la kuteka na kujeruhi.
Walalamikaji hao walieleza kwamba katika kupigwa huko, Juma aliibiwa
simu mbili na fedha taslimu shilingi laki tatu na themanini huku Rashid
akiibiwa shilingi laki tatu ambazo alipewa na mteja wake kwa ajili ya
kwenda kununulia vifaa.
MJUMBE AKIRI
Naye mjumbe wa eneo la tukio,
Muharami Seif alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kukiri kuwaokoa
jamaa hao wakiwa katika hali mbaya baada ya kupata taarifa kutoka kwa
majirani hivyo Petit Man na Wema wanasubiriwa watue Bongo kukabiliana na
mkono wa sheria.
No comments:
Post a Comment