Wakati Rais Jakaya Kikwete wa
Tanzania na Rais wa Zanzibar, Dr Ali Mohammed Shein, leo jioni
wakitarajiwa kukabidhiwa rasimu ya katiba iliyopitishwa na Bunge Maalum
la Katiba, nchi hiyo inajikuta ikiwa katika mgawanyiko wa kisiasa ambao
haujashuhudiwa kwa muda mrefu.
Hassan Mhelela anatathmini mchakato mzima wa kusaka katiba mpya na changamoto zake.
Rasimu
hiyo ya katiba ilipitishwa kwa kura ya ndiyo ya wajumbe wengi wa chama
tawala CCM na wale wa kundi maalum, huku wajumbe wa vyama vya upinzani
wakisusia na wala hawakushiriki katika kupiga kura ya mwisho
Kwa
sasa imeweza kuvuka hatua kuu mbili, kinachofuata baada ya Rais Kikwete
kukabidhiwa itakuwa ni kupigiwa kura ya maoni na wananchi, lakini bado
barabara ya kuifikia katiba kamili imejaa visiki na utelezi.
Katika
hatua hiyo bado hakuna uhakika endapo itafanyika ndani ya miezi sita
iliyopangwa kwa mujibu wa sheria, au kazi hiyo itasogezwa mpaka mwaka
2016 baada ya uchaguzi mkuu wa 2015.
Lakini kizingiti kingine
ambacho katiba itakabiliwa nacho ni kuoanisha katiba ya Jamhuri ya
Muungano ya Tanzania kuendana na katiba ya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar – zinazounda Muungano wa Tanzania.
Ikumbukwe kuwa kabla
ya mabadiliko haya kuanza mwaka jana, Zanzibar ilikuwa imefanya
mabadiliko ya katiba yake mwaka 2010 kama hatua mojawapo ya maridhiano
ya amani yaliyomaliza uhasama kati ya chama tawala CCM na upinzani CUF.
Swali la kujiuliza ni kwamba kutokana na msimamo wa wajumbe kutoka
Zanzibar kupinga rasimu hiyo, je watakubali kufanya mabadiliko katika
katiba ya Zanzibar ili iendane na rasimu inayopendekezwa, na lini
litafanyika hilo?
Kimsingi ili mabadiliko ya katiba ya Zanzibar
yafanyike inatakiwa ipitie katika Baraza la Wawakilishi (sawa na Bunge
la Zanzibar) na baada ya hapo iidhinishwe kwa theluthi tatu ya kura ya
maoni ya wananchi wa Zanzibar.
Kwa upande mwingine, maswala
makubwa yaliyosababisha mgawanyiko ni muundo wa serikali – ziendelee
kuwa mbili kama ilivyo sasa au ziwe tatu kama rasimu ya kwanza na ya
pili zilivyopendekezwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliyoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Jaji Joseph Warioba?
Hapo
katikati kumetokea mvurugano ambao umeacha maswali mengi zaidi kuliko
majibu yanayotoa ufumbuzi – hata tume iliyokusanya maoni imekuwa
imepuuzwa na wajumbe wake kurushiwa vijembe kutoka nje na ndani ya Bunge
Maalum la Katiba kuwa iliegemea upande mmoja.
Rais wa Zanzibar Dr
Ali Mohammed Shein amemfukuza kazi aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa
Zanzibar, Othman Masoud Othman kutokana na msimamo wake wa kupinga
rasimu hiyo ya katiba.
Nafasi yake imechukuliwa na Said Hassan
Said, aliyetangazwa siku moja kabla ya rasimu kukabidhiwa kwa Rais
Kikwete na Rais Shein wa Zanzibar.
Huo ni msimamo ambao ni nadra sana kujitokeza hadharani katika siasa
za Tanzania, na wachambuzi wa mambo wanasema haishangazi kuona hatua
zilizochukuliwa.
Vile vile waliokuwa wajumbe wa tume hiyo
wamekanusha kupendelea upande wowote, badala yake wameeleza kuwa
walichowasilisha ni maoni ya watanzania.
Ingawa chama kikuu cha
upinzani CHADEMA kimejaribu kuhamasisha maandamano ya nchi nzima kupinga
mchakato huo wa katiba, hakijapata mafanikio makubwa kutokana na
serikali kutumia vyombo vya dola kudhibiti maandamano hayo.
Jambo
la kusubiri kwa hamu ni kuona kama Rais Kikwete atatoa hotuba
itakayojaribu kuwaunganisha watanzania wakijiandaa na hatua inayofuata
ya katiba, au atawapuuza wapinzani na wananchi wanaopinga rasimu hiyo.
Ikumbukwe
kwamba mwezi uliopita Rais Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa
Tanzania ikiwemo chama chake cha CCM, walikubaliana kuwa mchakato wa
kupata katiba mpya usimame baada ya hatua hii ya Bunge hadi baada ya
uchaguzi mkuu.
Hata hivyo suala hilo pia linategemea kuzua mvutano
mwingine wa kisheria kwakuwa sheria ya kuanzisha mchakato wa katiba
inataka rasimu ikitoka Bungeni ipelekwe kwa wananchi ndani ya miezi
sita.
No comments:
Post a Comment