MAPENZI YA MAMA YAMTESA, MWENYEWE AMTOROKA
ILIPOISHIA
Khadija
Kopa aliishia pale aliposema kwamba katika kipindi hicho ndicho
alipogundua kwamba mbali na ukimya wake, uoga wake lakini Mungu alikuwa
amempa kipaji cha uimbaji. Hivyo aliamini kwamba kingeweza kumsaidia
katika maisha yake ya baadaye.
Malkia wa miondoko ya taarabu, Bi Khadija Omari Kopa.
ENDELEA...
Nilipofika darasa la saba, hapo ndipo niligundua kwamba nilikuwa na
uwezo wa kuimba, mbali na sura nzuri ambayo Mungu alikuwa amenibariki
lakini pia alinipa sauti nzuri.
Katika Chuo cha Madrasa tulikuwa tukiimba huku wavulana wakipiga
madufu, hapo ndipo nilipoendelea kujiridhisha kwamba sauti yangu
ilimvutia kila mmoja kiasi kwamba mwalimu wetu akanifanya kuwa kiongozi
wa chuo kile katika uimbaji.
Wanachuo wengi wakaanza kuisifia sauti yangu, ilikuwa ni ya kipekee
sana ambayo kwa kila aliyekuwa akiisikia alikuwa akishangaa. Kuna
wanachuo wengine walitaka niwafundishe lakini sikujua ni kwa namna gani
ningeweza kufanya hivyo.
WASICHANA WAMCHUKIA
Siku zikaendelea kukatika,
nilijijengea heshima mpaka shuleni, maisha yangu yalikuwa tofauti na
maisha ya wanafunzi wengine, nilikuwa mfano wa kuigwa japokuwa kulikuwa
na wasichana wengine ambao hawakupendezwa na sifa nilizokuwa nikipewa. Khadija Kopa akiwa ni mwenye furaha.
“Anapenda sifa, kwanza wala siyo mzuri.”
“Umeona, kwanza wala havutii, hawezi hata kuufunga ushungi wake,” alisema msichana mwingine.
Hayo yalikuwa maneno machache ambayo ninaweza kuyakumbuka mpaka leo
hii, wasichana wengi walikuwa wakinichukia kwa sababu tu sikuwa nikitaka
urafiki nao, hicho ndicho kilikuwa chanzo cha hayo yote.
Kwa darasani, kama kawaida sikuwa na uwezo mkubwa lakini sikuwa
miongoni mwa wanafunzi waliokuwa wakifanya vibaya. Japokuwa kulikuwa na
masomo ambayo sikuwa nikiyapenda, lakini kiukweli nilipenda somo la
hisabati na ndilo ambalo nilikuwa nikifanya vizuri zaidi.
Japokuwa kuna baadhi ya watu wanaweza kunichukulia vibaya lakini
ningependa kuyaweka wazi maisha yangu kwamba nilizaliwa katika familia
iliyomjua Mungu na hata nilipokuwa nakua, bado niliendelea kuishi katika
maisha hayo.
Sikuwahi kukosa kwenda msikitini, ilikuwa ni nadra sana kwa mtoto wa
Kiislamu hasa Zanzibar kukosa kwenda msikitini. Mtaa mzima kulikuwa na
watoto wa Kiislamu, kwa hiyo linapofika suala la kwenda msikitini,
kutokwenda lilikuwa jambo gumu.
AMSUMBUA BIBI KUHUSU MAMA
Mama hakuweza
kunitenga, japokuwa katika kipindi hicho alikuwa akija mara chache sana
lakini nilikuwa nikimpenda sana. Niliyamisi sana mapenzi ya mama,
hakukuwa na kitu nilichokuwa nikikitamani kama kuwa karibu na mama
yangu.
Si kwamba bibi hakunipa malezi mazuri, la hasha! Alinipa lakini
upendo wa mama huwa ni wa kipekee sana kwa mtoto, hivyo nikatamani
kuishi na mama yangu.
“Bibi, mama yangu yupo wapi?” nilimuuliza bibi yangu.
“Atakuja tu. Subiri.” Alinijibu kwa sauti ya chini.
“Lakini ninataka kumuona mama yangu, ninataka kukaa na mama yangu bibi.”
“Sawa. Akija mwambie hayo yote.”
“Atakuja lini?”
“Hivi karibuni.”
“Lini?”
“Usijali. Atakuja tu.”
Nilionekana kama msumbufu lakini ukweli
wenyewe ni kwamba nilimkumbuka sana mama yangu. Kama kuishi na bibi,
nilikuwa nimekwishayazoea mapenzi yake na hivyo nilitaka kuyaonja
mapenzi ya mama yangu.
Kila siku niliendelea kumwambia bibi kwamba nilimtaka mama yangu
arudi tena lakini ahadi zake zilikuwa zilezile kwamba kuna siku
angekuja.Wiki nzima nilimsubiria mama yangu, kitendo cha kuja mara
mojamoja na kuniachia fedha za matumizi pamoja na zawadi mbalimbali
sikufurahishwa nacho, mapenzi yake yalikuwa ni zaidi ya fedha na zawadi.
Sikuwa na jinsi, kwa umri wangu, Zanzibar ilikuwa kubwa, kitendo cha
kusema niondoke na kuelekea mitaani kwa ajili ya kumtafuta mama yangu
lilikuwa jambo gumu, hivyo nilitakiwa kusubiri kitu kilichonifanya
kuziona siku zikienda taratibu kwa mwendo wa kinyonga.
MAMA AMTEMBELEA TENA, AMNG’ANG’ANIA
Nakumbuka
wikiendi ya siku hiyo, kama kawaida mama alikuja tena nyumbani. Sikuwa
mahali hapo, nilikuwa tuisheni. Alipofika, bibi alimwambia kila kitu
kilichoendelea kwa wiki hiyo, hivyo hakutaka kuondoka.
Niliporudi na kumuona, nikashindwa kuvumilia, nikamsogelea mama na
kumkumbatia kwa furaha, nilimng’ang’ania sana na sikutaka kumuachia.
“Nataka kuondoka na wewe....nataka kuondoka na wewe....” nilimwambia mama huku nikilia.
Japokuwa alinibembeleza kwa kuniambia maneno matamu lakini sikutaka
kumuelewa, kumuachia aondoke na kuniacha nikiwa na bibi, lilikuwa jambo
gumu kutokea, nilichohitaji ni kuondoka naye tu.
Siku hiyo mama hakutaka kuondoka, akaamua kulala hapohapo huku usiku
mzima nikiwa nimemng’ang’ania kwani sikutaka aniache kwa bibi, hukohuko
alipokwenda, nilitaka kwenda naye.
Nilipoamka asubuhi, hakuwa ameondoka, nilikuwa naye pembeni huku
akinionyeshea upendo wa hali ya juu niliokuwa nikiutamani kutoka kwake.
Ilipofika saa mbili asubuhi, akaniambia niende madrasa.
“Nataka
kubaki na wewe mama,” nilimwambia. Kila nikikumbuka kipindi hicho, huwa
ninabaki nikicheka tu, nilimng’ang’ania mno mama yangu.
“Nenda madrasa, ukitoka huko, tutakwenda wote.”
“Utanikimbia.”“Siwezi kukukimbia. Nenda kwanza chuo.”
MAMA AMTOROKA
Nilikubaliana naye lakini moyoni
nilikuwa na wasiwasi mno, nilijua angenitoroka. Nilikubali kwenda chuoni
lakini bado sikujisikia amani kabisa. Sikusoma kwa raha, mawazo yangu
yalikuwa kwa mama tu.
Kitu kilichoniuma siku hiyo, ni kwamba
niliporudi nyumbani, mama hakuwepo, alikuwa amekwishaondoka. Vuta picha
niliumia kwa kiasi gani.
“Atarudi tena,” aliniambia bibi, sikutaka kumsikiliza, nikaondoka na
kuelekea chumbani, nikaufunga mlango kwa ndani na kuanza kulia, sikutaka
kuufungua na sikutaka kuonana na mtu yeyote, niliyakusanya mashuka na
kuyalalia, machozi yalikuwa yakinibubujika, siku hiyo, sikutaka hata
kula.
Nilihitaji sana mapenzi ya mama maishani mwangu.
No comments:
Post a Comment