Mwalimu
wa darasa la awali wa Shule ya Msingi Nakayaya, Teckla Milanzi (kulia)
akiwa na wanafunzi wake eneo ambalo hutumika kama darasa la wanafunzi
hao.[/caption]
WADAU
wa elimu nchini Tanzania wanaamini kwa kiasi kikubwa kwamba endapo elimu
ya awali (chekechea) nchini Tanzania itatolewa katika misingi
inayostahiki itakuwa ni njia moja wapo madhubuti ya kuimarisha ubora wa
elimu. Hii ndiyo maana wanaendelea kupaza sauti wakiitaka serikali
kupitia vyombo husika kuboresha kwanza elimu ya awali kabla ya kupanda
ngazi nyingine za juu.
Huenda
kilio hiki cha wadau wa elimu kimeanza kusikika serikalini. Kwani
tayari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliagiza tangu mwaka 2010
kuwa kila shule zake za msingi ni lazima lianzishwe darasa la awali ili
kuwenza kuwaandaa wanafunzi kuingia na darasa la kwanza. Awali elimu hii
ilikuwa ikitolewa kwa kiasi kikubwa na taasisi na vikundi mbalimbali na
hata watu binafsi nje ya shule za msingi, tena kwa hiyari. Kwa sasa
sera na miongozo ya elimu inatamka wazi kuwa nilazima kila shule ya
msingi iwe na darasa la awali kwa ajili ya elimu hiyo muhimu.
Changamoto
kubwa iliyoibuka kwa sasa baada ya utekelezaji wa agizo hilo ni namna
elimu hiyo inavyoendeshwa kwa kusuasua kwenye baadhi ya shule za
Serikali. Hivi karibuni mwandishi wa makala haya alitembelea baadhi ya
shule za msingi zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru
kuangalia hali ya utekelezaji wa zoezi hilo.
Uchunguzi
ulibaini zipo shule ambazo licha ya kusajili wanafunzi wa awali kila
mwaka hazina madarasa ya kusomea kwa watoto hao, hali ambayo inafanya
wanafunzi hao wadogo kufundishwa katika mazingira magumu na kudhohofisha
lengo zima la utoaji wa elimu hiyo. Wapo wanafunzi ambao hulazimika
kufundishiwa nje, yaani chini ya mti ama kwenye magofu (majengo ya shule
ambayo hayajakamilika) iwe madarasa au nyumba za walimu.
Teckla
Milanzi ni mwalimu wa darasa la awali, Shule ya Msingi Nakayaya.
Anasema kimsingi wanafunzi wa darasa la awali shuleni hapo wanasomea
chini ya mti kwa kuwa hawana darasa maalum kwa wanafunzi hao. Anasema
wakati wa mvua ama jua kali mara nyingine hulazimika kuhairisha masomo
kwa siku kutokana na hali ya hewa.
Baadhi ya wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Tunduru
Mchanganyiko wakiwa darasani kama walivykutwa na mwandishi wa makala
haya hivi karibuni
Anasema
anashukuru kwa sasa wanajihifadhi kwenye jengo moja ambalo linaendelea
na ujenzi shuleni hapo, jengo ambalo hata hivyo mara baada ya ujenzi
kukamilika na wahusika kukabidhiwa darasa watarudi kusomea chini ya mti
kama ilivyo ada. Hata hivyo, anasema licha ya changamoto hiyo darasa
hilo halina vitabu kwa ajili ya kufundishia wanafunzi, bali kuna nakala
moja moja kwa baadhi ya masomo ambavyo vilitafutwa kwa jitihada za
mwalimu mwenyewe.
“Mfano
kwa vitabu vya Kiswahili, Kiingereza, Sayansi na Hisabati kuna nakala
moja moja tu, ambazo hutumiwa na mwalimu mwenyewe. Anasema darasa hilo
licha ya kuwa na changamoto kedekede hata kwenye mgao wa fedha
zinazoletwa shuleni kila mara halimo hivyo hakuna kinacholetwa tofauti
na wanafunzi wengine,” anasema Bi. Teckla Milanzi.
Kwa
upande wake, Mwalimu Christina Komba wa darasa la awali Shule ya Msingi
Tunduru Mchanganyiko anasema madarasa ya elimu ya awali Wilayani Tunduru
yanakabiliwa na changamoto nyingi. Anabainisha kuwa madarasa mengi
likiwemo lake hawana vitabu wala miongozo ya namna ya ufundishaji kabisa
zaidi ya kila mwalimu anayefundisha kubuni nini afundishe kila uchao.
“…Kwanza
licha ya kutokuwa na vifaa vingine hatuna chumba maalumu cha wanafunzi
hawa (darasa) kwa sasa tunatumia jengo la darasa ambalo bado linaendelea
na ujenzi na hata hivyo jengo hili halijengwi kwa ajili ya wanafunzi wa
awali,” anasema mwalimu Christina Komba. Wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Nakayaya, wakiwa katika darasa lao.
“Madarasa
ya elimu ya awali hayana vitabu, hayana miongozo…huwa tunaanzima au
ukipata hela yako wewe binafsi unaenda kununua kitabu kimoja au viwili
ili uweze kuwasaidia watoto. Na baadhi ya masomo hayana vitabu kabisa
hata ukienda madukani katika Wilaya yetu (Wilaya ya Tunduru) vitabu kama
Haiba na Michezo, pamoja na Sanaa hazipo kabisa madukani. Anasema
uongozi wa juu wilayani unalitambua hilo.
Batadhari
Mkwela ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nanjoka anasema usajili wa
wanafunzi wa awali kila mwaka huongezeka japokuwa bajeti ya kuendesha
elimu hiyo ni changamoto. “…Darasa la awali linahitaji vitendea kazi
lakini havipo, hatuna vifaa kama vitabu vya kutosha, vyenzo za
kufundishia, hakuna bajeti hata ya vifaa hivi toka Serikalini, hatuna
madawati maalum kwa ajili ya wanafunzi wa awali,” anasema Mkuu huyo wa
Shule ya Nanjoka.
Hadija
Makamla ni mwalimu wa darasa la awali Shule ya Msingi Majengo. Mwalimu
huyu ambaye amehitimu kozi ya kufundisha darasa hilo, anasema anavyo
baadhi tu ya vitabu vinavyoitajika katika darasa hilo. Anabainisha kuwa
darasa hilo lina jumla ya wanafunzi 48 lakini hutumia darasa la
wanafunzi wa kawaida maana hawana darasa lililojengwa maalum kwa
wanafunzi wa awali.
“…Ninazo
nakala chache kwa ajili ya mwalimu tu ila wanafunzi hawana hata
kimoja…lakini kuna masomo mengine sina vitabu kabisa kama vile Sanaa na
Haiba ya Michezo sina kabisa hata mimi,” anasema mwalimu Makamla.
“…Unajua watoto kwa kiasi kikubwa wanajifunza kwa vitendo, picha na
uhalisia, sasa huenda tunavyowapa ni vikubwa zaidi au vidogo sana kwa
sababu ya kubuni mada kwa baadhi ya masomo.
Dorothea
George ni mwalimu wa darasa la awali shule ya Msingi Nanjoka Wilayani
Tunduru. Yeye anasema japokuwa hakuwahi kufanya kozi ya ualimu wa awali
kwa sasa amekabidhiwa darasa hilo kulifundisha katika shule yake.
Anasema darasa hilo kwa sasa lina wanafunzi 98 ambao wanasomea darasa
moja chini ya mwalimu mmoja.
Anasema
licha ya darasa hilo kuwa na madawati kadhaa lakini si maalum kwa ajili
ya wanafunzi wa awali bali ni ya wanafunzi wa kubwa, hata hivyo bado
kuna watoto wanalazimika kukaa chini kwa kile kukosa madawati ya kutosha
katika shule hiyo. Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi
Majengo, Madina Mkali anasema uendeshaji wa darasa la awali shuleni hapo
ni wa kusuasua kutokana na changamoto anuai zinazowakabili. Hakuna
bajeti inayoingia kuisaidia elimu hiyo, ispokuwa mwaka huu waliletewa
madawati kumi kwa ajili ya elimu ya awali.
Kaimu
Ofisa Elimu Wilaya ya Tunduru, Abdul Kazembe akizungumza na mwandishi wa
makala haya (hayupo pichani) ofisini kwake hivi karibuni.
“…Uendeshaji
elimu ya awali hapa ni wa wastani kwa kweli kutokana na changamoto
zinazotukabili, kwanza vifaa vya kuwafundishia watoto hawa ni tatizo na
wazazi kwa eneo hili wamekuwa hawana mwamko wa elimu hii kabisa. Kwanza
hawachangii michango ya chakula kama inavyotakiwa ili mtoto apate
chochote awapo shuleni,” anasema mwalimu Mkali.
Anabainisha
kuwa watoto pia wanatakiwa kupata uji wawapo shuleni lakini uchangiaji
kwa wazazi nao umekuwa tatizo kubwa. “…Wapo wanaochangia wengine
wanagoma tunasukumana hivyo hivyo na mambo yanasonga mbele…lakini
kutokana na uchangiaji duni kuna baadhi ya siku wanapata uji na
sikunyingine hawanywi kutokana na ugumu wa michango,” anasema mwalimu
George.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko, Adam Hausi katika
mazungumzo na mwandishi wa makala haya anasema uendeshaji wa elimu ya
awali katika shule hiyo ni juhudi binafsi za mwalimu wa darasa hilo.
Anasema darasa hilo halina bajeti yoyote kutoka serikalini hivyo hakuna
vitabu na vitendea kazi vingine vinavyohitajika.
“…Vitendea
kazi ndio tatizo kabisa, ila mwalimu anafundisha kwa jitihada zake na
darasa linaendelea. Alafu lina idadi kubwa sana ya wanafunzi (84) na
anafundisha peke yake…,” anasema Hausi. Anasema uboreshaji elimu ya
msingi ni suala la ushirikiano kati ya Serikali na jamii yenyewe lakini
wakati mwingine Serikali inakwamisha juhudi hizo kwa kushindwa
kuwajibika ipasavyo baadhi ya maeneo.
“…Mfano
sisi tulijenga madarasa mawili kwa nguvu za wananchi hadi yamekamilika
ilipofika suala kuezekwa tokaomba msaada wa Serikali pamoja na
kumaliziwa ili yaanze kutumika ilikuwa kazi kweli tulizunguzwa sana hadi
tukaanza kuyatumia hivyo hivyo,” alisema.
Bi.
Thabita Farara ni Mkazi wa Kata ya Mringoti Mashariki anasema bado
mwamko wa elimu ya awali kwa wazazi ni mdogo, maana wazazi wengi
wamekuwa wakijiandaa na darasa la kwanza tu kumuandikisha mtoto. Kwa
upande wake Asha Komba Mkazi wa Tunduru Stendi anasema yeye anaitambua
elimu ya awali na kuikubali lakini ni ile inayotolewa na shule binafsi
kama za taasisi. Lakini ile inayotolewa kwenye shule za Serikali ni
tatizo kubwa maana hazizingatii ubora wa elimu zaidi ya kuwalundika
watoto tu darasani.
“…Mimi
naitambua elimu ya awali na watoto wangu wote wamepitia lakini huwa
tunawapeleka kwenye chekechea za taasisi mbalimbali kama zinazomilikiwa
na makanisa majeshi na zinginezo maana huku ndiyo kidogo mtoto
anaandaliwa…kule Serikalini kwanza unakuta darasani wapo kibao alafu
muda wote wanacheza tu si kujifunza,” anasema Bi. Komba.
Abdul
Kazembe ni Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Tunduru, anasema kwa sasa kila
shule ya msingi sera inaelekeza lazima iwe na darasa la awali. Anasema
hata katika usajili wa wanafunzi wa darasa la kwanza kwa sasa watoto wa
mwanzo kusajiliwa ni wale waliopata elimu ya awali katika shule husika.
“…Kwa
hiyo kuna umuhimu wa kila shule kuwa na darasa la awali…changamoto sasa
inakuja kwenye vitendea kazi, kwa mwaka 2013 na kurudi nyuma uwepo wa
‘capitation’ ulikuwa pia unaelekeza watoto wa awali wapo mule na hata
tunapotoa takwimu za awali tulianza na ‘pre-primary’ (wanafunzi wa
awali) hivyo wenyewe wapo, tatizo hapa ni ujaji wa pesa yenyewe ya
‘capitation’ haitimii kama inavyo elekeza, yaani ile wastani ya kwamba
kila mtoto apate shilingi 10,000 kwa mwaka hautimii,” anasema.
Anatolea
mfano mwaka 2013/14 kiwango cha fedha ambacho kilitakiwa kuja katika
halmashauri ya wilaya hiyo ni zaidi ya milioni 366.7. Kiwango hiki ni
kile kilichoidhinishwa katika bajeti tu lakini ukirudi kwenye mahitaji
halisi ni zaidi ya kiasi kilichoidhinishwa. Anasema kilichokuja ni zaidi
ya milioni 196.5 fedha ambayo ni karibia nusu ya kiasi kilichopitishwa
kwenye bajeti. Anabainisha hilo ndilo tatizo kubwa kwani hata fedha
ambazo zimepitishwa haziji kama ilivyopitishwa kwenye bajeti.
“…Kwa
hiyo unaweza kuona kwamba ni ngumu kuigawa fedha hii katika matumizi
maana kwanza haitoshi na pili hata kilichotegemewa kuja ni pungufu zaidi
tena sana, sasa sijui unaweza kugawa kila shule ipate shilingi
ngapi…kwani haitoshelezi,” anasema.
Anasema
kwa upande mwingine miundombinu ya madarasa ni changamoto kubwa. Kwa
mwaka 2013 idadi ya mahitaji ya madarasa kwa wilaya nzima ilikuwa ni
1,715 lakini ukiangalia vyumba vya madarasa vilivyopo ni kama 900 na
kitu na mengine ni ya muda mrefu sana kiasi ambacho yanaelekea kuchakaa
jambo ambalo pia yanapungua.
Aidha
anaeleza kuwa ukienda kwenye bajeti ya ujenzi wa madarasa mapya milioni
171 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na miundombinu mbalimbali kiasi hiki
cha fedha waweza kuta kinauwezo wa kujenga madarasa kama nane tu. Kiasi
hicho cha fedha ni pamoja na ujenzi wa nyumba tano za walimu. Na kiasi
hicho cha fedha za ujenzi ni pamoja na kumalizia miradi viporo za nyumba
za walimu na vyumba vya madarasa. Anasema upungufu wa vyumba vya
madarasa eneo hilo ni karibia madarasa 800.
“Sasa
kwa ujumla unaweza kuona kuwa miundombinu pale shuleni haitoshelezi, ni
jambo la kawaida kuona walimu wakiacha ofisi itumike kama darasa au
darasa litumike kama ofisi. Huku kwa awali ni changamoto zaidi maana
licha ya upungufu wa vyumba hata wazazi hasa vijijini wanashindwa
kuchangia chakula (uji) kwa watoto wao unaweza kukuta wameandikishwa
wengi Januari lakini kila muda unavyozidi kwenda watoto wanapungua na
unaweza kukuta hadi mwezi Juni darasa linapotea kabisa kwa utoro,”
anasema.
Kazembe
anabainisha kuwa kuna jumla ya shule za msingi 144 katika wilaya hiyo,
huku shule zilizo na vyumba maalumu vya madarasa ya awali zikiwa 16 tu.
Anasema shule nyingine zote hazina vyumba vya madarasa ya awali na
matokeo yake ama wanatumia madarasa ya msingi kwa kupishana.
Anaongeza
kuwa uhamasishaji wa ujenzi wa madarasa ya awali na umuhimu wa elimu
hiyo unatolewa kwa walimu, wazazi na kamati za shule kupitia vikao
mbalimbali ambapo mara nyingi uongozi uhimiza wazazi kuchangia zaidi
nguvu zao katika kukamilisha ujenzi wa madarasa ya awali, utengenezaji
wa madawati na upatikanaji wa chakula cha mchana na uji shuleni.
“…lakini
tunaangalia sana chakula maana watoto hata kwenye mti wanaweza kukaa
wakasoma endapo wanamadawati pale au wamekaa chini kwenye kivuli,
japokuwa si mazingira mazuri sana shuleni…lakini wakiwa na chakula hata
utoro unapungua,” anasema.
Anasema
kwa mwaka 2013 serikali ilikumbuka kuleta fedha kwa ajili ya ununuzi
madawati ya wanafunzi wa awali, fedha ambazo tulizigawa na kununua
baadhi ya vitabu vya awali na madawati kwenye shule ambazo zinamadarasa
hai ya awali. Shule zilizonufaika na mgao huo ni shule za mjini Tunduru
tu ambazo nyingi ndizo zenye madarasa hai ya awali. Anasema ili
kukabiliana na hali ya upungufu wa walimu wa awali; imepitishwa walimu
wa gredi ‘A’ kufundisha madarasa hayo kwa kuwa wao mafunzo yao katika
kozi hujumuisha ufundishaji darasa la awali, tangu walioitimu mwaka
2013.
“…sasa
wakati mwingine unaweza kukuta mwalimu ni gradi A na kimsingi yeye anao
uwezo wa kufundisha darasa la awali, lakini wengine hawakubali hadi
aone ana cheti kabisa maalumu cha kufundisha darasa la awali…ukimuuliza
huyu atakwambia yeye hana taaluma ya kufundisha awali jambo ambalo si
sawa,” anasema Ofisa Elimu huyo wa Msingi.
“..Kwa
suala la vitabu kweli hii ni changamoto, hapo nyuma tulikuwa tunanunua
vitabu wenyewe wakini kwa sasa TAMISEMI wenyewe moja kwa moja wananunua
na kuvileta. Sasa huku kwetu ni nadra sana kuona wazabuni wetu wanaleta
vitabu vya awali kwa sababu soko lake ni dogo sana kutokana na idadi
ndogo ya uwepo wa elimu hii ya awali eneo husika,” anasema.
Hata
hivyo umeona unafuu maeneo ya mjini mzazi anatambua umuhimu wa elimu
hivyo anaweza kuchonga dawati kwa ajili ya mtoto wake lakini kwa
vijijini hali ni mbaya zaidi. Mzazi ukimwambia achangie dawati
anakushangaa na pia haoni umuhimu huo.
“…Nikwambie
unajua Wilaya ya Tunduru mzazi mtoto wake akifeli anafurahi sana…tena
baadhi wanaona kama ni sherehe, kwanza wakifanya mtihani tu wa la saba
barabarani akina mama wanashangilia wanaona wametua mzigo, unaweza
kujiuliza wazazi wanaoshangilia inamaana walikuwa wakiona ni adhabu
watoto wao kuwa shule? Lakini pia mtoto akisha faulu kwenda shule
hapelekwi hadi DC aunde kamati, atembee na hakimu na polisi kukamata
wazazi wanaogoma kusomesha watoto watishiwe ndo wanakubali
kusomesha…lakini kitendo cha wazazi kukamatwa kushikiliwa kwa kushindwa
kuwapeleka watoto shule wamegeuka na kuwarubuni watoto wao wasifaulu,”
anasema.
Anabainisha
kuwa ni kweli Serikali ina jukumu la elimu, lakini mzazi kwa upande
wake anajukumu zaidi, kuangalia mtoto wake anapata elimu gani na ya
kiwango gani na kama mzazi hayupo tayari basi haiwezekani na wakati
mwingine inakuwa ngumu. Kimsingi jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa
vifaa vya kufundishia na kujifunzia watoto wa awali zipo, lakini
upatikanaji wa fedha ndio.
Salum
Mtutula ni Mbunge wa Tunduru Kusini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Mbunge huyu katika mahojiano anakiri kuwa elimu ya awali ni muhimu na
msingi mzuri wa mtoto kielimu. Anasema mtoto anapopata elimu nzuri ya
awali huwa na msingi mzuri kielimu katika masomo yake ya mbele.
“…Ili
mtoto apate elimu bora ni lazima apate elimu ya awali
inayostahiki…hakiwa na msingi mbaya wa elimu ya awali kuna uwezekano
mkubwa way eye kufanya vibaya pia,” anasema Mtutula.
Hata
hivyo anaishauri Serikali kuingiza suala hili katika sheria na kanuni
zake kuwa kila shule ya msingi inapoanzishwa ianze na darasa la awali
kwanza ndipo madarasa mengine yafuate. “…Mimi nitafurahi kama suala hili
tutaliweka kwenye sheria au kanuni zetu kuwa kila shule ya msingi
inapoanzishwa basi lazima ianze na darasa la awali ndipo madarasa
mengine yafuate iwe shule za Serikali au binafsi,” anasema Mbunge
Mtutula.
*Imeandaliwa na: www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment