Alhamisi wiki hii wakaazi wa Scotland watapiga kura kuamua juu ya uhuru
wao kutoka Uingereza. Utofauti wa kitamaduni na kisiasa wa Wascot
unathibitisha vyema jaribio hilo, anasema Daniel Scheschkewitz. katika
maoni yake.Kwa miaka kadhaa watu wengi nchini Ujerumani na Ulaya ya Kati
waliichukulia Scotland kama mkoa wa mbali kaskazini mwa Uingereza,
ambako mvua hunyesha kwa wingi, na wanaume wake hupendelea kuvaa sketi,
kunywa Whisky, na kwamba uchoyo wao wa kimethali ulikuwa ni zaidi ya
utani. Lakini kwa karne nyingi hadi mwaka 1707, Scotland ilikuwa nchi
huru iliojitegemea na kujivunia, ambayo nafasi ya historia yake ilifutwa
baada ya kuungana na Uingereza.
Ikiwa Wascot wataamua kupiga kura ya Ndiyo, nchi hiyo itarudi kwenye
ramani ya Ulaya baadaye, na matokeo yake ni kwamba Uingereza inaweza
kujikuta katika wakati mgumu kutokana na madhara ya kisiasa na kiuchumi
ambayo bado hayajulikana kiwango chake. Je, hii itakuwa hatua ya kurudi
nyuma? Au ni kosa la wakati litakalopelekea kuanza kuundwa kwa majimbo
madogo huru katika Ulaya ya sasa isiyo na mipaka? Nadhani siyo.
Scotland ilikuwa tofauti siku zote
Mara zote Scotland ilikuwa tofauti na jirani yake wa kusini England, na
Waroma walilitambua hilo. Ni kwa sababu hii Mfalme Hadrian alijenga
ukuta kutenganisha mpaka kati ya Scotland na England ili kuwadhibiti
Wascot katika karne ya pili. Ilikuwa ni baada ya muungano wa familia za
kifalme mwaka 1603, na jaribio lililoshindwa la Wascot kutaka kujenga
himaya ya kibaishara, ndipo walikubaliana mwaka 1707 juu ya kuunganisha
bunge lao na lile la England.
England na Scotland ziliungana na Wales iliyokuwa na utajiri wa makaa
ya mawe, na kuunganisha rasilimali za mataifa hayo kuufanya muungano wa
mataifa hayo - yaani Uingereza, kuwa taifa kubwa na lililostawi kisiasa
na kiuchumi. Tofauti za kisiasa na kitamaduni zilitoweka baada ya
muungano huo, lakini zilikuja kujitokeza tena katika nusu ya pili ya
karne ya 20 kwa nguvu kubwa.
Muungano na England umepitwa na wakati
Margret Thatcher aliiondolea Uingereza viwanda na kuikarabati bajeti
goigoi ya nchi hiyo kwa kutumia mafuta yanayochimbwa katika bahari ya
kaskazini ya Scotland. Wascot walilichukulia hilo kwanza kwa ufahari,
lakini baada ya kugundua kuwa sehemu kubwa ya wakaazi wa mji mkuu wa
mafuta wa Aberdeen, ambao kwao unapaswa kuwa kama Abu Dhabi ya
Scotlanda, wanaishi katika hali ya umaskini, walianza kuwa na mashaka.
Mashaka hayo yaliimarishwa na hisia kwamba wahafidhina walikuwa dhidi
ya Scotland, hata wakati Wascot walichagua mwakilishi mhafidhina katika
bunge la Uingereza katika chaguzi zote tangu mwaka 1997. Zilikuwa hisia
hizo zilizojenga mazingira ya kukua na kuimarika kwa chama cha wazalendo
cha SNP katika miaka ya 1990, chama ambacho kinaongoza kampeni ya uhuru
wa Scotland.
Kuzaliwa upya kwa Scotland
Kwa miongo kadhaa Scotland imekuwa ikushuhudia kuzaliwa upya kwa
utamaduni. Tamasha la utamaduni la Edinburg ni moja kati ya matamasha
yanayotembelewa zaidi na linalowakutanisha wasanii wabunifu zaidi
duniani. Muziki wa Scotland ni maarufu na unapendwa sana duniani. Vyuo
vikuu vya Scotland ni vya bure na vinapokea wanafunzi kutoka duniani
kote. Wanasayansi wa Scotland wanatambulika hata nje ya mipaka ya
uingereza.
Wakati nchini England elimu inazidi kuwa haki ya matajiri wachache na
shule nyingi binafsi zinazidi kuchipukia, elimu ya juu imeendelea kuwa
nafuu kwa watu wote nchini Scotland, na inavutia wahamiaji wengi wenye
ujuzi wa juu kutoka sehemu mbalimbali duniani. Huko chama cha UKIP
kinachopinga uhamiaji hakina maana yoyote, wakati huko England sera zake
za chuki dhidi ya wageni na kupinga uhamiaji zimekipatia mafanikio
katika uchaguzi.
Manufaa kwa Umoja wa Ulaya
Scotland huru ingeomba mara moja kujiunga na Umoja wa Ulaya, ambao
hauwezi kuikatalia. Tofauti na hii, waziri mkuu wa Uingereza David
Cameron ametangaza kura ya maoni juu ya kuamua mustakabali wa Uingereza
katika umoja huo ifikapa mwaka 2017. Hivyo anaweza kuwa amechelewa.
Ishara zinaonyesha nafasi ya 50 kwa 50 kwa Scotland kutumia fursa hii ya
kihistoria, na kupitia zoezi hilo la kidemokrasia kurejeshea taifa lao
kwa njia za amani.
Hata kiuchumi Wascot hawapaswi kuwa na hofu. Licha ya hifadhi ndogo ya
mafuta walionayo, serikali ya Scotland inaweza kutumia rasilimali zake
luluki kuwa ya nishati jadidifu na kuwa miongoni mwa mataifa 20
yaliyostawi zaidi kiuchumi duniani. Umoja wa Ulaya unaweza kunufaika na
taifa hilo jipya.
No comments:
Post a Comment