Katika eneo hili, PPP mbili zinaonekana zaidi, ile ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) na Richmond/Dowans. Tofauti ni kwamba, wakati kashfa ya Richmond/Dowans ilifikia kulazimisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa (Februari 2008), hakuna ambaye amechukuliwa hatua kuhusu IPTL –ambao ni mradi wenye hasara kubwa zaidi na umekuwa ukitengeneza umeme wa bei mbaya ya kinyama kwa zaidi ya muongo mmoja.
Mada hii bainifu inaelezea ilikotoka IPTL na kuchukuliwa kwake ‘kisheria’ hivi karibuni na Pan-Africa Power Tanzania Ltd (PAP). Ni hadithi tahadharishi ya jinsi mahusiano kati ya dola na sekta binafsi yanavyoweza kutumika kwa manufaa ya wachache kwa kuumiza walio wengi, kuleta hasara zenye athari pana katika uchumi na uwezo wa kuendesha uchumi kwa jumla.
Wahusika wawili muhimu wa IPTL ni James Rugemalira wa VIP Engineering and Management (VIPEM), Harbinder Singh Sethi wa PAP na mlolongo wa makampuni mengine ambayo yana rekodi chafu nchini Kenya.
Matokeo ya kashfa hiyo ni kuwa Sethi sasa 'anamiliki' mtambo wa kufua umeme wa megawati 100 ambao hajawekeza hata thumni na Rugemalira ametia mfukoni kiasi cha dola milioni 75 (Shilingi bilioni 123 kwa viwango vya sasa) kutokana na hisa zake asilimia 30 katika kampuni ambayo hajawekeza hata senti tano.
Mada hii inafananua jinsi kati yao, na kwa ushiriki wa viongozi wa Tanzania na maofisa wa serikali, watu hao wawili walijichotea kutoka BoT zaidi ya dola milioni mia moja ishirini na nane za Marekani sawa na shilingi za Tanzania bilioni mia mbili.
Kiwango hiki cha fedha kinaweza kujenga barabara ya lami kilometa 217 kutoka Itigi (Singida) mpaka Tabora Mjini. Kwa namna nyingine, fedha hizi zingeweza kujenga kipande cha barabara cha Ndundu – Somanga cha kilometa sitini mara tatu na chenji kubakia. Kipande hiki kinalalamikiwa sana na wananchi wa mikoa ya Kusini yenye utajiri wa gesi na Serikali ya Awamu ya Nne imeshindwa kabisa kukimaliza lakini imeweza kujenga bomba la gesi kutoka mikoa hiyo kuelekea Dar es Salaam!
Mada hii bainifu inafafanua vianzio nilivyovitoa katika makala ya hivi karibuni, iliyochapishwa kwenye magazeti ya hapa Tanzania; The Citizen kwa lugha ya Kiingereza na Raia Mwema[1] na magazeti ya Tanzania Daima na Mwananchi kwa Kiswahili.
Katika makala hiyo nilihoji madai yasiyo ya kawaida ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, ambayo baadaye yalirudiwarudiwa na wengine, kuwa fedha iliyokuwa kwenye akaunti ya Escrow ya Tegeta 'Si fedha ya umma.' kwa vile vitabu vya TANESCO vinaonyesha fedha ya escrow kuwa ni akiba.
Nilisisitiza kuwa hapakuwa na amri ya Mahakama Kuu kuhusiana na kutolewa fedha ya escrow ilipwe kwa wadai, uongo mwingine uliorudiwa na maofisa kadhaa waandamizi, kama ambavyo unayakinishwa hapa chini.
Tatu, nilidai kuwa kuchukuliwa kwa asilimia 70 ya hisa za Mechmar kutoka IPTL na PAP, dili linalohusisha kampuni isiyoeleweka ya Paperlink na visiwa vya Virgin (British Virgin Island) vya Uingereza, pia ilikuwa uporaji. Hizi na hoja nyingine nilizotoa katika makala zinaelezewa kwa kirefu zaidi hapa.
Mwaka 2009, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, ambayo nilikuwa Mwenyekiti wake wakati huo, ilitoa agizo kwa Benki Kuu isitoe fedha katika akaunti hiyo ya Tegeta escrow. Katika nafasi yangu ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha za Serikali, hapo Machi 20 mwaka huu nilimwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu kufanya Ukaguzi Maalum wa kina wa akaunti ya escrow ya Tegeta kwa nia ya kupata undani wa jinsi ambavyo wamiliki wa IPTL na PAP walifaulu kuiingia na kuchukua zaidi ya nusu ya fedha zilizokuwamo humo.
Ukaguzi huo utajumuisha tathmini ya uhalali wa PAP kuchukua hisa za IPTL kutoka Mechmar na VIP Engineering.
Mada hii imegawanyika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza inatoa muhtasari wa ilikoanzia IPTL na shughuli zake katika miaka ya 1990 hadi sasa. Tunajaribu kuonyesha jinsi uporaji wa hivi karibuni wa akaunti ya escrow una mizizi yake katika kuingiza sekta ya Nishati katika mfumo wa soko katika miaka ya 1990, ambako angalau mhusika mmoja muhimu (Rugemalira) ni muhimu kwa muda wote huo. Sehemu ya pili inaelezea habari za akaunti ya escrow ya Tegeta na mikakati ya washiriki wakuu waliohusika. Tunajaribu kuonyesha jinsi wanasiasa kadhaa na majaji walivyotoa udhamini wa wizi wa mchana kweupe wa Benki Kuu.
Sehemu ya tatu inajadili matokeo ya uporaji huo, na rushwa ya jumla katika sekta ya nishati, kwa uchumi, watumiaji wa umeme, serikali na wafadhili. Tutafikia tamati kwa kuangalia masuala ambayo hayajatatuliwa ambayo yatahitaji kuangaliwa ili mkasa wa IPTL ufungwe kabisa. Kiambatanisho 1 kinatoa vianzio vya mada hii. Kiambatanisho 2 kinaorodhesha rejea za vyombo vya habari na mitandao.
Sehemu ya Kwanza:
Kufikia IPTL na Pan-Africa Power (Ona Kiambatanisho 1: 1994-..)
(2)
"Kama huu ni mfano wa ushirikiano wa nchi za Kusini, basi ukoloni ulikuwa afadhali." ----------- Julius Nyerere
Mchango wa IPTL kwa Sera ya Nishati nchini na ufanisi wake tangu 2004 umekuwa kwa jumla ni hasi. IPTL ilihujumu juhudi za serikali kupunguza utegemezi katika vianzio vya maji na mafuta kwa kutumia utajiri wa gesi asilia nchini. IPTL ilianzia katika majadiliano ya ngazi za juu kati ya wanasiasa wa Tanzania na Malaysia mapema miaka ya 1990. Waziri Mkuu Mahathir Muhammad alipigia debe biashara za Malaysia katika Afrika, ikiwemo Tanzania, kama njia ya kuendeleza ushirikiano wa nchi za Kusini, na kutatua utegemezi kwa nchi za Magharibi. Hivyo IPTL mapema ilipewa kipaumbele na serikali, hivyo kuweka kando kuendelezwa kwa mitambo ya kutumia gesi.
Mnamo mwezi Mei 1997, benki za Bumiputra na Sime (Singapore) ziliikopesha kampuni ya Malaysia ya Mechmar zaidi ya dola milioni 100 za Marekani kujenga mtambo wa IPTL eneo la Tegeta, Kaskazini ya Dar es Salaam. Baada ya hapo, benki ya Bamiputra ilitangaza mkopo huo kuwa hauna tija. Mnamo Agosti 2005, benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) ilinunua deni hilo, lenye thamani ya dola milioni 125; kwa dola 74 milioni. (3)
Kampuni ya Finland ya Wartsila ilijenga na kuendesha mtambo wa IPTL ambao una vinu 10 vya ukubwa wa kati, vinavyotumia dizeli kufua umeme wa megawati 100.
Ukizingatia kwamba IPTL inazalisha chini ya asilimia kumi ya umeme wote unaozalishwa hapa nchini, imepata tuhuma kubwa na inazostahili mahakamani katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.
Mgongano wa muda mrefu kuhusu gharama za ujenzi wa mtambo - na hivyo bei ambayo Shirika la Umeme nchini (TANESCO) inahitajiwa kulipa kwa umeme wake - ilichelewesha kwa muda mrefu kuzinduliwa kwa IPTL.
Badala ya kufua umeme kupunguza upungufu uliokuwa unazidi wa umeme nchini, IPTL ilitumia miaka ya 1997 hadi 2001 ikilumbana na TANESCO, ikiwa ni pamoja na kufikishana katika vyombo vya kimataifa vya usuluhishi mwaka 1998. Mnamo Februari 2001, Kituo cha Kimataifa cha Kutatua Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) kilifikia tamati kuwa IPTL ilikuwa imejiongezea thamani yake kwa dola milioni 23.5, hivyo kulazimisha upunguzaji wa malipo ya uwezo wa mitambo (capacity charges) ambayo TANESCO inahitajiwa kimkataba kulipa kwa umeme wa IPTL.
IPTL mwishowe ikazinduliwa Januari 2002, karibu miaka minane tangu kampuni hiyo imeundwa, Lakini chini ya mwezi mmoja baadaye mwenye hisa chache za IPTL, VIP Engineering and Management (VIPEM) iliwasilisha madai mahakamani kuwa kampuni hiyo ivunjwe, kwa msingi kuwa VIP haijapata asilimia 30 ya hisa za IPTL. Hadi 2013,VIP ilikuwa inajaribu kufunga IPTL dhidi ya upinzani wa Mechmar Bhd, kampuni yenye hisa nyingi zaidi ya Malaysia (asilimia 70) ikiwa ni 'mshirika' wa VIP.
Rugemalira, mmoja wa ‘vigogo’ wa IPTL, ana tabia ya kutoa madai ya kipuuzi dhidi ya washirika na washindani wake kibiashara. Kutokana na nafasi yake muhimu katika mkasa wa IPTL katika miaka 20 iliyopita, ana bahati hakuwahi kumulikwa kwa karibu na vyombo huru vya habari, ambavyo kwa kawaida vinajitahidi kuonyesha rushwa katika ngazi za juu inayohusisha wawekezaji kutoka nje.
Ukinzani kuhusu IPTL katika miongo mmoja uliopita ulilenga gharama kubwa za umeme wa IPTL, kuwekwa kando kwa mradi wa umeme wa Songas wakati IPTL ilipotokea na uhusika wa wanasiasa wa ngazi za juu kusukuma dili hilo –wakipinga ushauri wa kitaalamu na upinzani wa TANESCO na maofisa wa ngazi za juu serikalini.
Benki ya Dunia - iliyotoa fedha nyingi zaidi kwa mradi wa Songas - pia iliikosoa IPTL, kama lilivyofanya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), na Umoja wa Ulaya (EU) na baadhi ya nchi wafadhili.
Kwa mujibu wa Gratwick na Eberhard (2006:46), mwaka 2005, malipo kwa IPTL na Songas yalifikia kiasi cha kushangaza cha theluthi mbili ya mapato yote ya TANESCO. (4) Kuharibu zaidi, mwaka uliofuata:
"..........wakuu serikalini, walifanya mzaha uleule wa IPTL. Walitoa tenda ya kufua umeme wa haraka kwa kampuni hewa (ya mfukoni), Richmond Ltd, na kuiacha nchi 'gizani' kwa zaidi ya miezi mitatu na kugharimu taifa mamilioni ya dola za Marekani zilizoibwa na kuparaganyika kwa uchumi (Brewin 2011). (5)
Mnamo mwaka 2005, benki ya Standard Chartered (Hong Kong) *SCB) ilinunua deni la IPTL wa dola milioni 74 kutoka kwa kampuni wakala wa madeni ya ngazi ya pili wa Malaysia iitwayo Donahatra,, ambako benki ya Bumiputra ilikuwa imeliweka kama amana isiyo na tija. Kuanzia 2005 hadi sasa, SCB-HK ilijaribu bila mafanikio kupata jawabu la mivurugano ya kisheria ya IPTL ili kuendeleza mtambo bila matatizo na kulipa deni lake. Walihujumiwa na VIP na PAP, ambao walitafuta njia ya kuchukua mtambo huo bila kulipa chochote ikiwa bado katika hatua ya kufilisiwa.
Hapo Agosti 2007, serikali ilisimamisha ulipaji wa gharama za uwezo wa kuzalisha kwa IPTL kuhusiana na thamani ya mtambo kwa gharama halisi za ujenzi. TANESCO ilidai kugundua baada ya muda kuwa VIP ilikuwa imeweka tu kiasi mfano cha hisa (sehemu ya mtaji) katika mradi (sehemu ya hisa inatumika katika kufikia malipo ya uwezo wa mtambo). Hivyo TANESCO ikaona kuwa ilikuwa ikilipa zaidi ya jinsi inavyotakiwa kulipa.
Licha ya kuwa dhamira ya kubadilisha mtambo wa IPTL kutoka mafuta kwenda gesi ulipendekezwa tangu mwanzo, ulishindikana kutekelezwa, hivyo kulazimisha gharama zisizo za lazima kwa uchumi kwa kuagiza dizeli hiyo nje na kwa watumiaji kwa umeme ghali (angalia Timeline Desemba 28, 2009).
Songas inadai kuwa imeiokolea nchi mamilioni ya dola za Marekani ambazo zingetumika kununulia mafuta kutoka nje. Licha ya kuwa kuwekeza katika matumizi ya gesi kungepunguza gharama na kuongeza faida kwa IPTL, kuagiza mafuta kunatoa mwanya wa watu kujipatia fedha kwa udanganyifu, kwa wahusika katika sekta ya umma na sekta binafsi (angalia Timeline Agosti 8, 2012). Makisio ya kiasi ambacho ingegharimu kubadili mtambo wa IPTL kutoka diseli kwenda gesi inatofautiana, ila tarakimu ya dola milioni 20 za Marekani linatajwa mara kwa mara. Kubadilisha kungeiokolea TANESCO kiasi kinachokisiwa kufikia dola milioni 840 katika uagizaji wa mafuta kwa miaka 20 ijayo.
Kati ya miradi muhimu ya ubia wa sekta binafsi na umma kwenye sekta ya Nishati, IPTL na Richmond zinajitokeza kama makosa ya gharama kubwa ambayo nchi ingefaidika kutokuwa nayo. Lakini wakati Richmond ilitwaa kichwa cha Lowassa, hakuna ambaye amebanwa kuhusiana na hasara zilizotokana na kashfa ya muda mrefu ya IPTL. Sehemu ya pili inaangalia jinsi kati yao Harbinder na Rugemalira walivyolitapeli taifa zaidi ya dola milioni 128 (na zinaongezeka hadi dola milioni 250).
Sehemu ya 2: 'Kununuliwa' kwa IPTL na wizi wa akaunti ya escrow ya Tegeta
Akaunti ya escrow ya Tegeta iliundwa baada ya TANESCO kuacha kulipia uwezo wa mitambo ya IPTL mnamo 2006. Jinsi fedha katika akaunti ya escrow ya Tegeta zilipongezeka, ndivyo shauku ilivyozidi miongoni mwa kundi fulani la wafanyabiashara kuichukua kampuni hiyo yenye migogoro, akiwemo Sethi. Akiwa anajulikana kama mwekezaji kutoka Kenya katika vyombo vya habari, Bw. Sethi kwa yakini ni mzaliwa wa Iringa, mwaka 1958 (ona Kisanduku 1). Hapa tunaelezea jinsi Sethi alivyochukua hisa kwanza za Mechmar na halafu zile za VIP Engineering.
Hisa asilimia 70 za Mechmar
Kuhamishwa kwa hisa kutoka Mechmar kwenda kampuni ya Piperlink ltd na halafu PAP ilikuwa ni wizi mtupu. Ni kwa njia gani ambako PAP ilichukua hisa za Mechmar katika IPTL mwaka 2010 wakati Mechmar ikiwa inafilisiwa? Sheria za nchi zote ulimwenguni haziruhusu jambo hilo kutokea kwani ni marufuku hisa za kampuni iliyo chini ya muflisi kuuzwa au kufanyiwa biashara yeyote.
Au, kama wengine wanavyoamini, wakurugenzi wa Mechmar waliwazidi akili wasimamizi wa Malaysia, ikiwa ni pamoja na Mahakama Kuu, na kufaulu kuuza hisa zao? Anachoeleza Harbinder ni kuwa Mechmar kwanza iliuza hisa zake katika IPTL kwa kampuni kificho inayoitwa Piper Link, ambayo ilizihifadhi, kwa sababu moja au nyingine, huko British Virgin Islands vya Uingereza.
Wapokeaji wa dhamana za Mechmar walidai kuwa Mkurugenzi wa Mechmar, Datuk Baharuden bin Abdul Majid alikiuka Amri ya Mahakama ya Oktoba 4, 2010 kwa kuipotosha Mahakama kwa kuingia makubaliano ya kununua hisa (kwa dola milioni sita za Marekani) na hao Piper Link Investments mnamo Septemba 9, 2010. Wapokeaji (waliokuwa wanaifilisi Mechmar) walifaulu kupata hati ya Mahakama Kuu ya BVI (visiwa hivyo) kuitisha vyeti vya uuzaji huo wa hisa kwa msingi kuwa ulikuwa kinyume cha sheria. Vyeti hivyo vya hisa vilifikishwa na muuzaji kwa Mahakama Kuu ya BVI. (6) Hivyo ni kwa njia gani Piper Link ilifaulu kuuza hisa zake kwa PAP wakati ushahidi unaonyesha kuwa wakurugenzi wa kampuni hiyo walikuwa wamezuiliwa kukamilisha mpango huo mnamo Aprili 2011? Ni hati zipi ambazo wamiliki wa PAP walifikisha Wizara ya Nishati na Madini kuthibitisha umiliki wa IPTL? Kwa mujibu wa Sheria ya Fedha 2012, kifungu cha 29 wizara inatakiwa kuruhusu uuzaji baada ya kukpokea cheti cha kuthibitisha kuwa mahitaji yote ya kodi yametimizwa kutoka Mamlaka ya Kodi Tanzania. Hati zinaonyesha kuwa Pipelink ilinunua hisa za Mechmar kwa shilingi milioni sita na baadaye kuuza hisa hizo kwa PAP kwa dola 300,000. Kampuni zote mbili, Mechmar na PiperLink zililipa kodi ya ongezeko la mtaji siku hiyo hiyo katika tawi la CRDB la Azikiwe mnamo Desemba 5, 2013, siku moja baada ya Benki Kuu kuachia fedha za akaunti ya escrow kwa PAP.
Hisa asilimia 30 za VIPEM: Jawabu la kitendawili cha IPTL kufungwa lilitengenezwa na Harbinder na Rugemalira, kwa PAP kununua hisa za VIP asilimia 30 za IPTL kwa dola milioni 75 baada ya VIP kuondoa madai ya mwaka 2002 katika Mahakama Kuu kufunga kampuni hiyo. (Kiambatanishi 1).
Kuporwa kwa akaunti ya escrow: Katika barua yenye tarehe ya Novemba 28, 2013 (isiyo na namba ya rejea) IPTL inaiomba Benki Kuu kuhamisha dola milioni 22 na shilingi bilioni nane kutoka katika akaunti ya escrow kwendaa akaunti za PAP "kama uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ya Septemba 5, 2013 unavyoagiza."
Maofisa wa serikali na PAP wanasema kuwa hukumu ya Septemba 2013 ya Jaji Utamwa J, iliambatana na amri ya kuondoa fedha katika akaunti ya escrow. Kwa jambo hilo, mwandishi wa habari wa gazeti la Daily News aliripoti matukio hayo kwa usahihi:
" ....Mnamo Septemba 5, 2013,, Jaji wa Mahakama Kuu John Utamwa alimwamuru Kabidhi Wasii Mkuu (mfilisi wa muda wa IPTL) kutoa usimamizi wa shughuli zote za kampuni, ikiwa ni pamoja na mtambo wa umeme, kwa PAP." (7)
Hakuna mahali akaunti hiyo ya escrow ilipotajwa. Kufuatilia hukumu ya Jaji Utamwa ya Septemba 5, mapema mwezi Oktoba 2013, maofisa wa TANESCO na IPTL walikutana katika hoteli ya Kunduchi Beach. (8) Minute za mkutano huo zinasomeka kwa uchache:
"..Mahakama Kuu imemwamuru Mfilisi wa Muda kutoa mali zote za IPTL ikiwa ni pamoja na mtambo ya umeme wa IPTL na amana zinazopokelewa za akaunti ya escrow ya Tegeta kwa Pan Africa Power Solutions (T) Limited." (9)
Lakini ukisoma kwa uangalifu unaona kuwa hapakuwa na amri katika hukumu hiyo kutoa amana hizo 'zinazopokelewa.' Tofauti hii haikuonekana au ilipuuzwa na wanasheria katika Benki Kuu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kama amri muhimu kama hiyo ingetolewa, si ni wazi kuwa mwandishi Faustine Kapama, ambaye kwa kawaida anaandika inachosema VIPEM kuhusu suala la IPTL, angeiandika katika habari yake iliyonukuliwa hapo juu? Hoja isiyo sahihi kuwa akaunti ya escrow iliamriwa kufungwa na Mahakama Kuu ilichukuliwa na Mwanasheria Mkuu na Gavana wa Benki Kuu, Benno Ndulu.
Katika barua kutoka kwa Werema, ya tarehe 2 Oktoba 2013 kwa Katibu Mkuu, Hazina, Dk. Servacius Likwelile, Mwanasheria Mkuu haoni sababu yoyote kwanini Benki Kuu isihamishe fedha za akaunti ya escrow kwa PAP na Serikali isionekane kuyumba katika kutekeleza "kile ambacho mahakama iliamua." (10)
Mnamo Septemba 10, 2013, E.S. Maswi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini alimwandikia Bw. Sethi katika nafasi yake kama Mwenyekiti na Ofisa Mtendaji Mkuu wa IPTL, kuwa, 'kufuatia mashauriano kati ya TANESCO na ninyi" hakuwa na kipingamizi kutia saini makubaliano ya kutoa fedha za akaunti ya escrow ya Tegeta (ona Timeline, Kiambatanisho 1). Hata hivyo mkutano unaotajwa ulikuwa wa kawaida tu kati ya maofisa wa ngazi za chini wa TANESCO bila kuwepo watendaji wakuu wa VIP au PAP wakihudhuria.
Hapa chini tunatoa wasifu wa wahusika wakuu wawili wa VIP na PAP. Historia zao wote wawili zinaonyesha kuwa walikuwa na uwezo wa kubuni mkakati wa kuitoa IPTL kutoka mikononi mwa mpokeaji wake rasmi nchini Malaysia, kununua hisa za Mechmar kwa kupitia dalali feki, kupata umiliki kamili wa IPTL kwa kupitia ujanja wa kisheria,, na mwishowe kudaka fedha ya akaunti ya escrow kwa msaada wa maofisa wa serikali.
Kisanduku cha 1: Harbinder Singh Sethi ni nani?
Harbinder Singh Sethi ni mmoja wa wawekezaji vijana wenye asili ya Kiasia ambao walitajirika miaka ya 1980 wakati Rais Daniel arap Moi wa Kenya alipoanza kutengeneza himaya yake binafsi ya biashara na majengo.
Akitajwa katika magazeti kama mfanyabiashara wa Kenya na tajiri mkubwa, Sethi alizaliwa na kulelewa Iringa, katika Nyanda za Juu Kusini. Katika umri wa miaka 20 na ziada kidogo, Sethi na kaka zake wawili Nota Singh na Manjit Singh walisajili kampuni ya Ruaha Concrete Co. Ltd (Novemba 1977), wote watatu wakitoa anuani ya S.L.P. 498 Iringa kama anuani yao.
Katika miaka ya 1980, Singh alihamia Nairobi ambako alianza kuwa mbeba mifuko wa mwanae wa kwanza Rais Daniel arap Moi, Gideon. Anasemekana pia kuwa alikuwa rafiki wa karibu wa Nicholas Biwott, mwanasiasa na mfanyabiashara tajiri na mtu wa karibu wa Moi.
Akiwa nao anasemekana kumiliki sehemu ya mtambo ulioleta zogo wa megawati 47 wa Westmont mjini Mombasa, akiwa na Mukesh Gohil, Kamlesh Pattni, Bw. Gichuru, Mkurugenzi Mtendaji wa KPLC, Bw. Mutitu, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Gideon Moi (Oktoba 1997).
Uchunguzi wa Kroll ulionyesha kuwa Gideon anamiliki mali kadhaa nchini Afrika Kusini.. Inaelezwa zipo mali zake ambazo zimeandikishwa kwa kutumia jina la Harbinder Singh Sethi. Mtanzania huyo wa Iringa anaelezwa kuwa na mali 74 zilizooreshwa chini ya "mashirika yaliyofungwa," ambayo yote yameandikishwa kwa jina la Sethi.
Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Mashirika nchini Kenya (1997) inataja kandarasi iliyotolewa kinyume cha utaratibu na kampuni ya serikali Kenya Pipeline Company kwa Ruaha Concrete Ltd kujenga barabara ya kilomita tisa kufikia mtamboni, ambako kulikuwa na ucheleweshaji, kuongezeka kwa gharama, na utekelezaji hafifu.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi Mkuu, "Ruaha imesajiliwa katika kundi la wapaka rangi na wajenzi wa barabara za ndani katika mashamba makubwa."
Mhandisi msimamizi A.S. Kitololo alijiuzulu baada ya kukataa kutia saini kuwa kazi iliyozembewa imekamilika. Gharama ya mradi wote ilipanda kutoka Ksh 197 milioni mnamoi Februari 1995 hadi zaidi ya Ksh510 milioni mwezi Juni 1998, ambako mradi huo hatimaye ulikamilika.
Katika ukaguzi, barabara iligundulika kuwa imejengwa kwa kiwango cha chini. Ripoti ilitoa rai kuwa Ruaha Concrete iwekwe kwenye orodha ya makampuni yasiyotakiwa na ipelelezwe.
Kampuni nyingine ya Sethi, Pan African Builders and Contractors, (PABCO), iliingia mkataba na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wa Kenya, kujenga nyumba, maghorofa ya kupangisha na eneo la maduka Kitisuru jijini Nairobi ambako NSSF ina nyumba za kupangisha, kwa gharama ya Ksh2bilioni.
Tarehe iliyopangwa kumalizika ilikuwa Mei 2000, Mradi huo ulicheleweshwa baadaye na kupunguzwa ukubwa wake kufikia Ksh82.2milioni. Akikabidhi mradi huo, malipo hayo hayakukamilishwa, na PABCO ikaishtaki NSSF mahakamani kutaka ilipwe Ksh1.3billioni.
Mnamo Agosti 31, 2010 Mahakama Kuu ilitoa hukumu kuipa haki PABCO kulipwa Ksh668milioni, pamoja na gharama na riba ya fedha hizo. PABCO mwishowe ikakubali kuishia katika malipo ya Ksh590milioni. PABCO ikashindwa kulipa kwa wakati unaohitajiwa kwa Mamlaka ya Kodi nchini Kenya kodi ya kiasi cha Ksh260milioni.
Kutokana na biashara zake zenye giza, Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Umma (PIC) ikamweka Sethi katika fungu la watu wasioaminika, ikitoa rai asipewe kandarasi za ujenzi kokote nchini. Kukamilisha picha, kama mkurugenzi wa Hydrotanz Ltd, Sethi pia ana hisa katika utafutaji wa mafuta na gesi katika uwekezaji wa pamoja na Adhulink Group, kampuni ambayo imetwaa kitalu cha mafuta na gesi Mnazi Bay, kisiwa cha Songosongo. Hydrotanz ipo kiwanja na. 887 mtaa wa Mrikau, Masaki jijini Dar es Salaam, anuani moja na PAP.
Hivi karibuni, Sethi ameibuka na kuanza kutoa misaada mbalimbali kwa jamii kama sehemu ya uwajibikaji kijamii wa IPTL/PAP kwa kutoa michango kadhaa: Sh. 11milioni kwa SACCOS ya kundi la kwaya ya kanisani la Kanisa la Mtakatifu Rita Wakashia lililoko Kimara, Sh10 milioni kwa ujenzi wa kituo cha polisi cha Mbweni-Malindi, Sh14.5milioni kusaidia ujenzi wa Kanisa la Mtakatifu Petro jijini na Sh.20 milioni kwa ajili ya Chama cha Mchezo wa Riadha nchini (AT) kusaidia kufanyika kwa mashindano ya riadha ya taifa. (Jumla ya uchangiaji kwa uwajibikaji kijamii ni sh.55.5milioni).
Kwa kificho pia, Sethi amekuwa akifadhili baadhi ya vyama vya siasa nchini ili kuhakikisha kwamba vinakaa kimya bila kuhoji uporaji uliofanyika. Uchunguzi wa kina wa matumizi ya vyama vyote vya siasa nchini ukifanyika kwa kulinganisha na ‘forensic investigation’ inayofanywa na TAKUKURU utaweza kuibua kiasi cha fedha ambacho Bw. Seth ametoa kwa vyama tajwa. Baadhi ya viongozi wa vyama hivi ni marafiki wa Seth wa muda mrefu.
Kianzio: Makubaliano ya wanahisa wa Ruaha Concrete 1977, Ripoti ya Kroll (vipande),, Taarifa ya Mkaguzi Mkuu (Mashirika) kuhusu hesabu za Kenya Pipeline Company kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30. 1997 (ukurasa wa 75-78), "Masahihisho' ya NSSF ya Kenya kuhusu taarifa za magazeti, Aprili 3, 2012; HYDROTANZ LIMITED, TANZANIA.
Ona rejea (Kiambatanisho 2) kwa viashiria vya dili feki za kibiashara za Dethi nchini Kenya, nafasi yake kama mbeba mikoba wa Gideon Moi na uhusiano wake wa kibiashara na Biwott na Pattni, na kuingia kwa Hydrotanz yake katika utafutaji wa gesi.
Rais Moi aliwatumia Waasia nchini Kenya kama washirika wake wakati akiwaingiza watu wa kabila lake la wa-Kalenjin katika kina cha mamlaka za kiuchumi na kisiasa. Wa-Kalenjin waliingia katika miradi ya pamoja na wafanya biashara wa Kiasia ambao mara nyingi walikuwa wakipelekwa mbele kwa niaba ya wa-Kalenjin ambao walikuwa wameupata utajiri.
Waliofaulu zaidi walitumia dola kupata kandarasi katika sekta ya umma kwa kushirikiana na watu wa kabila la Kalenjin waliokuwa wanamzunguka Rais Moi.
Licha ya kuwa Mtanzania kwa kuzaliwa, Harbinder alikuwa mmoja wa wafaidika wakuu wa ulaji rushwa rasmi wa enzi za Rais Moi.
Kisanduku 2:
James Rugemalira ni nani?
James Burchard Rugemalira ndiye mhusika mkuu wa Tanzania katika mkasa wa muda mrefu wa IPTL. Akijiita kuwa ni mtaalamu huru, mshauri wa kimataifa na 'mzalendo mkubwa,' Rugemalira ni mwajiriwa wa zamani wa Benki Kuu ambaye alistaafu mapema na kusomea biashara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alipata shahada daraja la kwanza licha ya kuwa hakuwa mwanafunzi mwenye kipaji kinachoonekana.
Katika nafasi yake kama Mkurugenzi wa VIPEM Ltd, alikuwa mtu muhimu katika kuwezesha mradi wa IPTL kuharakishwa katika mikondo tofauti ya utawala nchini - na hasa kwa vile ulikuwa ni mradi wa haraka. Migongano ya kisheria ilizuia mradi huo kuzinduliwa hadi miaka saba baada ya makubaliano ya msingi (MoU) kutiwa saini.
Miradi anayoshiriki ubia (Tritel, IPTL) na uwakala wa usambazaji (Windhoek, Heineken) mapema au baadaye huishia mahakamani. Mahakama za Tanzania zimesaidia kumbadili Rugemalira kuwa mmoja wa matajiri wakubwa sana hapa nchini. Wakati Rugemalira anapopeleka madai katika mahakama za hapa nchini dhidi ya wabia wake wa miradi ya ubia au washindani wake kibiashara, kesi zinafunguliwa dhidi yake na washirika wake katika mabaraza ya usuluhishi ya kimataifa. Kesi ya mwaka 2002 katika Kituo cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) ilitokana na jaribio la kihuni la IPTL kutunisha gharama za mradi huo wa umeme wa dharura.
Mkakati wake umekuwa kupeperusha bendera ya kitaifa na kuhoji uhalali wa washiriki kutoka nje katika kutatua madai tofauti, iwe ni makampuni, wanasheria, mahakama, akidai kuwa sheria za Tanzania ndizo peke yake zinaweza kutumika katika masuala hayo.
Licha ya kuwa mshirika wa kutafuta haki katika mabaraza ya usuluhishi ya kimataifa hapo awali, mafanikio yake ya kuiparamia akaunti ya escrow ilihitaji kwanza hatua ya kupuuza kilichoamuliwa na ICSID.
Licha ya kuwa maamuzi ya hivi karibuni ya mahakama nchini yameinua maslahi yake, kwa zaidi ya miaka kumi alishindwa kuifikisha IPTL kufungwa ili aweze kupata asilimia 30 yake ya hisa.
Kama ametia mfukoni dola milioni 75 alizokuwa anadai. basi huko kungoja kumekuwa na faida ya kutosha, kwani muongo mmoja uliopita angeambulia sana sana dola milioni 30. 'Akihojiwa' juu ya dili ya IPTL, Rugemalira alinukuliwa akisema "Inahitajika Watanzania wenzangu wanione kuwa ni mzalendo mkubwa kwa sababu mkataba huo ulilenga zaidi maslahi ya taifa. Nilikuwa nastahili kupata dola milioni 600 lakini nimepata dola milioni 75 ambayo ni vijisenti tu.."
Chanzo: Cooksey 2003, Citizen Reporter 2014c, allafrica.com/stories/2013/02281263.html, Daily News Reporter, 17 March 2014. Ona rejea na Kiambatanisho 2.
Baadhi ya Watanzania wasingeshangaa kama 'peanuts' zilizotajwa katika habari ya Kiingereza ni sawa kabisa na alichosema kwa Kiswahili, kuwa ni 'vijisenti' (kama ilivyotafsiriwa hapa).
Mwezi Septemba 2008, upinzani ulianza kuitaka serikali kununua mtambo wa Dowans wa megawati 100 kupunguza makali ya kukatika kwa umeme,, lakini serikali ikasita kufanya hivyio, ikisema kuwa hainunui mitambo wala bidhaa ambazo zimekwishatumika.
Kama serikali ingenunua mtambo wa Dowans. IPTL ingekuwa imeondolewa katika biashara kwa sababu ya urahisi wa kumudu umeme wa Dowans unaotokana na injini zinazotumia gesi, na hadi sasa IPTL inafua umeme kutumia mafuta mazito yanayoagizwa kutoka nje, licha ya karibu miongo miwili ya ahadi ya kubadilisha mtambo wa awali kuwa na njia mbili, ya mafuta na ya gesi.
Kwanini ubadilishaji huo haukuwahi kufanywa wakati ilikuwa wazi kuwa kwa maslahi ya umma kubadilishwa kungewezesha kubana malipo ya matumizi ya umeme kwa mtumiaji wa kawaida na serikali inafichua tatizo kubwa la kuweza kufanya kitu kwa pamoja, ambayo ina athari ya kuzuia utekelezaji kimantiki wa sera.
Hivi inavuka mpaka kusisitiza kuwa umeme wa ghali mno wa mitambo isiyo na mshindani ya IPTL ulikuwa unalindwa katika ngazi za juu kabisa? Kama IPTL ilileta zogo lote hilo, kwanini TANESCO iliendelea kuingiza mamilioni ya dola za Marekani katika akaunti ya escrow wakati ikiwa hailipi madeni mengine mengi tu? Nani atakayelipia ubadilishaji wa mtambo huo? Tutaacha hili na masuala mengine yanayofanana nalo kwa majadiliano.
Hadi sasa, VIP imekuwa ndiyo mfaidika mkuu wa uporaji wa Benki Kuu, Kama Rugemalira analipwa kikamilifu, atapata dola milioni 75 za Marekani kati ya dola milioni 122, au kiasi cha asilimia 60 ya kiwango kilichotolewa katika akaunti hiyo hadi sasa.
Lakini inasemekana bado kuna kiasi cha dola za Marekani 128milioni zilizobaki katika akaunti ya escrow ambazo Harbinder anatazamia kuingiza mikono yake hapo punde na siyo baadaye kidogo. Isitoshe, PAP, ambayo dili zake za kitapeli zimempa Harbinder mtambo wa IPTL bure, anakuwa katika nafasi ya kuendelea kuvuna kodi za pango (capacity charges shilingi bilioni 3.8 kila mwezi za kutumia mtambo huo) kama IPTL itaendelea kuruhusiwa kuwa katika shughuli zake kama kawaida, chini ya mfumo uliopo hivi sasa kisiasa.
PAP imeelezea nia yake ya kuongeza uzalishaji wa umeme wa IPTL mara tano, kubadilisha kutumia gesi, na kupunguza bei ya umeme hadi kufikia senti za Marekani sita hadi nane kwa uniti moja.
Kwa sasa, wanadai kufua umeme katika kiwango cha juu, wakitumia dizeli ya ghali, huku wakipata malipo ya uwezo wa mtambo yasiyofahamika kutoka TANESCO.
1. Matokeo: ubepari wenye vielelezo vya Kitanzania
".......Hivyo, wananchi ndiyo walikuwa walipaji wa bei ya mwisho. Hakuna umeme na uzalishaji mali ni mdogo, giza totoro usiku na gharama kubwa za uzalishaji wakati watu binafsi na makampuni wakigharamia kununua jenereta na mafuta kwa kuwasha taa na kuzalisha." (11)
Ufanisi huu duni wa sekta ya umeme, ikiwa ni pamoja na kujirudiarudia kwa makato makubwa ya umeme kwa miaka 20 iliyopita, na madeni makubwa ya TANESCO, ambayo yanachukua sehemu si ndogo ya pato la taifa kwa jumla, ni matokeo ya moja kwa moja ya kashfa za IPTL na Richmond, pamoja na udhaifu na rushwa katika utendaji wa kazi TANESCO. (12) Hapa tunatoa rejea ya athari za kashfa ya IPTL kwa washikadau muhimu.
Vyama vya siasa:
Kufichuliwa kwa tuhuma hizi kuhusu IPTL kutazidi kuvuruga imani ya wananchi kwa utawala wa Rais Jakaya Kikwete katika kujitayarisha kwa uchaguzi mkuu wa 2015. Imani hiyo inaweza kuanguka kabisa kama Sethi na Rugemalira wataruhusiwa kufurahia uporaji wao wa mchana kweupe.
Tunatumaini na tunaamini kuwa wanasiasa wa vyama vyote watahamasisha kusaidia kuwafikisha waliotekeleza kashfa ya IPTL/PAP mbele ya sheria mara watakapokuwa wamepata vielelezo vinavyohitajika.
Kwa wakati huu, Rugemalira na Sethi bado wanatamba na kutishia watu, kama ilivyoonekana kwa vitendo vyao vya kupeleka magazeti na wanasiasa mahakamani (mnamo Julai 13, 2014 IPTL na PAP walimshitaki mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila kwa kuwaharibia sifa, wakitaka sh. bilioni 310 kama fidia).
Ni wakati sasa kwa vyama vya upinzani na wapenda jema miongoni mwa wale walioko katika chama tawala kuchukua msimamo wa kimaadili dhidi ya uhalifu huu wa kiuchumi uliofanywa na IPTL, PAP na wahalifu wenzao.
Watumiaji umeme wa majumbani:
Chini ya Mtanzania mmoja kati ya 50 anapata umeme kutoka gridi, na weengi zaidi hukaa maeneo ya mijini. Jumla ya kaya milioni 7.2 zinasemekana hazina umeme, hasa vijijini. (13).
Bila uwazi zaidi na uwajibikaji katika sekta ya umeme, watumaji wa nyumbani watazamie mengine kama hayo katika miaka ijayo.
Biashara na uchumi:
Kwa mujibu wa OECD (2013), ukuaji wa uchumi unaanza kupita uwezo wa uzalishaji umeme:
"...........Kukua kwa wastani kwa uzalishaji umeme (ambako kulikuwa asilimia 4.2 tu kwa muongo uliopita) kunatofautiana na asilimia 7.1 ya wastani wa ukuaji wa uchumi na asilimia 8 hadi 13 ya kukua kwa mahitaji ya nishati kwa mwaka.'
Umeme usio na uhakika unavuruga biashara za kila ukubwa. Kwa mfano, mwaka 2002, kampuni ya Tanga Cement ilidai kupoteza kati ya Sh80 milioni na Sh400 milioni kwa mwezi kutokana na kukatwa kwa umeme. (14) Tafiti za kimataifa mara kwa mara zinataja kutokuwepo umeme wa kuaminika kama kikwazo cha kupatikana faida katika biashara nchini.
Kielelezo cha 1 kinataarifu juu ya maoni ua wafanyabiashara kuhusu udhaifu katika mazingira ya kufanya biashara nchini.
Kielelezo 1: Udhaifu wa mazingira ya biashara nchini, 2008-2012
.......... Kimsingi mchoro unaonyesha wasiwasi kuhusu umeme ukibaki tatizo la kwanza kwa wafanyabiashara, ambako halikubadilika katika nafasi yake kwa kipindi chote cha takwimu hiyo. Maeneo mengine ya wasiwasi yalikuwa yakipanda na kushuka, kwa mfano hali ya barabara, upatikanaji wa maji, usimamizi kodi, viwango vya kodi, fedha (mikopo) na hata rushwa. Upatikanaji wa umeme ulikuwa ndiyo udhaifu mkubwa uliotajwa na wafanyabiashara kutoka 2008 hadi 2012.
Fedha za Umma na Bajeti:
Ripoti hii imedhihirisha matokeo mabaya ya usimamizi mbovu wa sera katika sekta ya umeme kwa bajeti ya Tanzania. Katika ripoti ya nchi kuhusu Tanzania, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linasema:
"Licha ya kuongezeka kwa asilimia 40 kwa bei za umeme mnamo Januari 2012, nakisi ya ulipaji wa TANESCO kwa wanaowapa huduma ilifikia kiasi cha kukisia cha dola za Marekani 252milioni (takriban asilimia moja ya pato la taifa) hadi kufikia mwisho wa Oktoba 2012. ( Ukurasa wa 5). Kuvurugika zaidi kwa hali ya kifedha ya TANESCO kutafikia mwishowe kuwa ni mzigo kwa bajeti na kunaweza kusababisha makato ya nguvu ya umeme, hivyo kuweza kuvuruga matumaini ya kukua kwa uchumi." (ukurasa wa 6) (15).
Hasara ya Shirika la TANESCO kwa mwaka sasa imefikia shilingi bilioni 300 mwaka 2013 kutoka hasara ya shilingi bilioni 5 mwaka 2011. Hasara yote hili anayeilipia ni Mtanzania masikini kupitia bei kubwa ya umeme na kodi lukuki anazolundikiwa kila kukicha kwenye kila bidhaa anayotumia.
Kichangiaji kimojawapo muhimu katika kuongezeka kwa pengo la bajeti nchini na kukopa kwa dharura ni utawala mbaya na rushwa katika sekta ya nishati.
Wafadhili:
Mara ya mwisho fedha za aina hiyo zilipoporwa kutoka Benki Kuu ilikuwa ni Akaunti ya fedha za mikopo ya kigeni (EPA) iliyochelewa uliofanyika kabla na baada kidogo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 ambao uliingiza utawala uliopo madarakani sasa.
Jibu la wafadhili kwa wizi huo wa wazi lilikuwa wazi na la kusisitiza: serikali iajiri kampuni binafsi ya uhasibu kuchunguza suala hilo na kuwapeleka wahusika mahakamani. La kwanza lilifikiwa, hata kama si la pili.
Hivi sasa, ni Balozi wa Uingereza peke yake ndiye amezungumza hadharani kuhusu kashfa iliyojitokeza - ambayo kimsingi ni mbaya zaidi kuliko ile ya EPA katika athari zake zitokanazo - na akasemwa vibaya bungeni kwa sababu hiyo, kama inayoelezwa katika Kiambatanisho 1 (Mei 7, 2014).
Mfadhili ambaye yuko karibu zaidi na suala hili ni Benki ya Dunia, ambayo imetoa fedha mara kadhaa kuitoa gizani kifedha TANESCO hadi sasa, na sasa inatoa fedha kwa ajili ya kuigawa TANESCO kuwa sehemu tatu zinazojitegemea. Hapo mwezi Machi mwaka huu, Benki ya Dunia iliidhinisha:
"Mkopo wa IDA wa dola za Marekani milioni 100 kwa ajili ya shughuli za sera ya pili ya maendeleo ya sekta ya umeme na gesi, ambayo itaisaidia Tanzania kuboresha uthabiti kifedha wa sekta ya umeme, na kuinua ushirikiano sekta ya umma na binafsi kuongeza uwezo wa uzalishaji umeme," (16)
Mkopo huu unaendeleza jadi ambako wafadhili wanaitupia kamba TANESCO kujiokoa badala ya kuhitaji kufumuliwa kabisa kwa mpangilio wa ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi uliopo sasa ili kuwezesha misaada hapo baadaye.
Kama mashirika ya maendeleo yatapuuzia athari za kashfa hii kwa progamu wanazosimamia, basi watapoteza sifa kama wadau halisi wa kupiga rushwa na kuendeleza utawala bora mbele ya macho ya jamii na kuongeza kuungwa mkono kwa wale wanaoona mashirika ya maendeleo ni sehemu ya tatizo. Benki ya Maendeleo ya Afrika yenyewe imeendelea kumwaga fedha kwenye shimo lisilojaa la TANESCO.
Vyombo vya habari, asasi za jamii:
Tusingekuwa tunajadili undani wa kashfa hii yenye utata mwingi hivi sasa kama magazeti ya Nation Group, The Citizen na Mwananchi yasingekuwa yameitoa habari hiyo mwezi Machi.
Mara baada ya habari hiyo kutokea, PAP na IPTL ziliyapeleka magazeti hayo mahakamani zikidai kuwa makala hizo zililenga kutoa picha kuwa IPTL na PAP ni 'matapeli, wahalifu, wanaohusika na dili chafu zenye nia ya kupata fedha kwa udanganyifu na ni watu wa maadili hafifu."
Tunadhani kuwa maelezo haya yamepimwa vyema. Iwapo uhamishwaji wa umiliki kutoka Mechmar kwenda PAP ulikuwa ni kibadhirifu (fraudulent), hakuna neno bora zaidi la kuwaelezea PAP na makuwadi zaidi ya wao kuwa ni waporaji, wanyonyaji na matapeli waliokubuhu.
Rugemalira na Sethi wanaweza kujitambulisha bila kupingwa kama wazalendo na wawekezaji halisi, wakiwa wamepania kufanya jambo linalofaa kwa jamii, wakati ni wasanifu wa tatizo tulilo nalo la umeme, inaonyesha ni kiasi gani vyombo vya habari na asasi za jamii nchini ni dhaifu katika kutoa habari za ulaji rushwa mkubwa.
Hivi hakuna hata mmoja kati ya waandishi wetu wa habari aliyehangaika ku-'Google' Harbinder Singh Sethi kudhihirisha kuwa haiba yake nchini Kenya ni ya msukaji, tapeli aliyekubuhu? Unatafuta bila mafanikio kwa makala au tahariri katika moja ya magazeti yetu ambayo angalau inahoji nafasi ya Bw. Rugemalira na alichofanya katika ujanja wote huu? Kwa miaka mingi, gazeti la serikali la Daily News, limekuwa likitoa anachoeleza Rugemalira katika suala la IPTL.
Na ziko wapi asasi za kijamii zinazochukua suala hilo katika mwelekeo wa 'kupinga rushwa' au kufuatilia 'utawala bora'?
Kwenda mbele:
Ili kufanikiwa, mikakati hatarishi ya Sethi na Rugemalira inahitaji ushiriki wa dhati au wa kujitolea miongoni mwa wanasiasa waandamizi, maofisa wa serikali, majaji na vyombo vya habari. (17) Watuhumiwa wakuu walioko mstari wa mbele ni pamoja na wale ambao, tangu The Citizen na Mwananchi waanze kuelezea habari ya IPTL/PAP, wametetea kiliochofanyika au kuwasema wakinzani wake kwa nguvu. Nje ya Rugemalira na Sethi, orodha hiyo ni pamoja na:
* Mwanasheria Mkuu, Frederick Werema, ambaye anadai akaunti ya escrow siyo fedha za umma, na kuitaka Hazina kutokusitasita kuhusu kutoa fedha ya akaunti ya escrow. Anatuhumiwa kuiagiza Mamlaka ya Kodi kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika malipo ya uwezo wa mtambo.
* Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ambaye alidai bungeni kuwa wabunge wa upinzani wamehongwa kuinua suala la IPTL. (Wangehitaji vipi kuhongwa ili kuibuka na habari tamu kama hiyo?)
* Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, ambaye alimtuhumu balozi wa Uingereza kuwataka wafadhili na mashirika yasiyo ya kiserikali kuchukua msimamo kuhusu kashfa iliyoanza kujitokeza.
* Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi, ambaye alisema taarifa wanazotumia wabunge wa upinzani kuhoji uhalali wa kutolewa fedha za akaunti ya escrow 'siyo sahihi.' Alidai kuwa benki ya Standard Chartered ya Hong Kong siyo mhusika katika tofauti za IPTL na TANESCO. Alikuwa mtekelezaji mkuu wa kuhakikisha kuwa fedha za escrow zinaondolewa Benki Kuu.
* Utawala wa TANESCO, ambao hadi sasa haujatoa ukinzani wowote kuhusu kuondolewa kwa maamuzi ya ICSID kuwa upande wake na uporaji wa akaunti ya escrow,ambao kiasi fulani kilitakiwa kurudishwa TANESCO ambayo iko taabani kifedha.
- Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu, ambaye alichukua tahadhari kubwa kuzuia lawama kwa Benki Kuu kuhusiana na madai yoyote ya ziada kuhusu IPTL baada ya kufungwa kwa akaunti ya escrow ila akashindwa kueleza kwanini hakuhoji kuondolewa fedha za akaunti kwa kurejea uamuzi wa usuluhishi wa ICSID na uamuzi wake (Februari 2014) unaounga mkono dai la TANESCO kuwa walilipa kupita kiasi kinachohitajiwa kwa uwezo wa mtambo wa IPTL.
* Mfumo wa Mahakama: Mahakama nchini zinatoka katika mkasa wa IPTL zikiwa na haiba ya sura mchanganyiko, Licha ya kuzuia kwa miaka mingi juhudi za kila maara za kuifunga kampuni hiyo, tangu alipoteuliwa Mfilisi wa Muda, Rugemalira anaonekana kuweza kuitumia Mahakama Kuu atakavyo. Hivi Jaji Utamwa ana lipi la kusema kuhusu utumiaji mbaya na PAP wa hukumu yake ya mwezi Septemba kupora akaunti ya escrow?
Pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) hivi sasa inaichunguza PAP/IPTL kwa kuombwa na Waziri Mkuu (baada ya agizo la PAC la tarehe 20 Machi 2014, kwa nia ya kutoa tathmini kama kilichofanyika katika mada hii ni rushwa.
Katika wakati uliopita, PCCB iliwakingia lawama wanasiasa waandamizi, licha ya kuwa kulikuwa na ushahidi mkubwa wa kuwaingiza hatiani (18) Kama PCCB inataka kuinua mwonekano wake katika jamii itafanya uchunguzi wa kina ya kilichojiri katika suala hili kabla ya kufikia mahitimisho yoyote.
Maswali kadhaa ambayo hayajajibiwa:
Hivi imekuaje kwa mtambo wa kati wa kufua umeme ulete mgogoro mkubwa kisheria na katika vyombo vya habari kwa karibu miongo miwili na ukaruhusiwa kuvuruga vipaumbele vya uzalishaji umeme nchini?
Hivi imekuaje mradi huu uchangie kutokea kwa hasara kubwa kwa sekta ya umma na binafsi? Mradi huu ni kielelezo kimojawapo cha utawala mbovu katika sekta ya nishati hapa nchini.
Kama mkasa wa muda mrefu wa IPTL haufikii tamati yake hivi karibuni, upotevu wa kasi wa fedha za umma (na za wafadhili) utaendelea, kuvuruga zaidi udhaifu wa ushindani wa uchumi wa Tanzania. Tunahitimisha na maswali kadhaa ambayo hayajajibiwa:
* Kwanini TANESCO iliilipa IPTL kwa muda mrefu hivyo bila kuhoji malipo ya uwezo wa mtambo?
* Ni kwa muda gani mtambo wa IPTL ulikuwa haufanyi kazi, na ni wakati gani ulipoanza tena? Nani alilipia matengenezo yake wakati ukiwa haufanyi kazi?
* Ni wapi uhusiano wa Rugemalira na Harbinder ulipoanzia?
* IPTL ilikuwa inafanya nini na mapato yake, ni sehemu gani ya deni lake ililipwa?
* Ni fedha gani au hisa zilizobadilishwa kati ya PAP na Mechmar/Piper Link? Nani anamiliki Paper Link kama siyo Harbinder Singh Sethi? Nani anammiliki mwanahisa mwingine wa PAP anayeitwa Simba Trust?
* Ni fedha kiasi gani imebaki katika akaunti ya escrow, kama ipo?
* IPTL inafanya kazi? Nani anaimiliki? Hali yake ya fedha ikoje? Inapata fedha za uendeshaji wa mtambo hivi sasa? Ni kiasi gani? Nini kimekubaliwa na TANESCO?
REJEA
1. Zitto Kabwe, 2014 "Akaunti ya escrow ya Tegeta ni fedha za umma," The Citizen, Dar es Salaam, Juni 29,
2. Kipande hiki kinatoa muhtasari wa Cooksey (2002) kuhusu suala hilo katika chapisho Afrika Kusini, "The Ugly Malaysians?" n.k. katika Institute for Black Research, Durban
3. Punguzo hilo la dola milioni 51 za Marekani linaelezea thamani halisi ya sasa ya deni hilo na uhatarishi uliopo katika kununua dhamana ya tija duni. Hadi sasa, SCB-HK haijalipwa chochote kutoka IPTL.
4. Gratwick, Katherine Nawaal na Anton Ebehard (2008), "Kifo cha mfumo wa kawaida wa urekebishaji wa sekta ya umeme na kuzuka kwa masoko mchanganyiko ya umeme," katika jarida la Energy Policy, 36 (10): uk. 3948-3960
5. Degani, Michael "Umeme wa Dharura: Muda, Maadili na Umeme katika Tanzania baada ya Ujamaa," na Brewin, David "Rushwa, waliochelewa..." katika jarida la Tanzania Affairs 99: uk 15-19
6. Barua na viambatanisho kutoka kwa Lim Litt na Andrew Heng, wafilisi rasmi wa
Mechmar, kwa Zitto Kabwe, Mwenyekiti, Kamati ya Hesabu za Serikali, Machi 28, 2014
7. Faustine Kapama 2014, "PAP yaanza mipango ya kupunguza gharama za umeme," Daily News, Aprili 5
8. Walikuwa: John Kabadi, Meneja Mwandamizi, Mipango/Mikakati, Heromini Shirima, PDEO (?), na Stella Rweikiza, Ofisa Mkuu Sheria (wote wa TANESCO) na Joseph Makandege, Mwanasheria wa Kampuni, na XX (wote wa IPTL). Tarehe halisi ya mkutano huo haiko wazi katika minuti za mkutano huo.
9. Minuti za mkutano wa maofisa wa TANESCO na IPTL, Hoteli ya Kunduchi Beach, October 2013 (uk. 1-2)
10. Barua namba ya rejea GCC/E.80/6/65 (mkazo umeongezewa)
11. OECD 2013, Mapitio ya Sera za Uwekezaji, Tanzania, Agosti 6, uk, 101
12. Wakati wa kuandika mada hii, Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa TANESCO alikuwa mahakamani, akikabiliwa na mashtaka ya kuingiza kampuni ya mkewe katika kashfa ya manunuzi. TANESCO pia inahusika na kashfa ya ununuzi wa mafuta ambayo inaihusisha IPTL (ona maelezo).
13. TANESCO ina kiasi cha watumiaji wa umeme 900,000, ambao asilimia 80 wanaishi mijini.
14. George Sembony 2012, "Wafanyabiashara wamechoshwa na kukatika umeme," Citizen, Desemba 28
15. IMF 2013, Ripoti ya nchi, Tanzania, uk. 6
16. Lazaro 2014 (Kiambatanisho 1 Machi 21, 2014)
17. Kwamba hawa ni wengi inathibitishwa na jinsi maofisa wa vyeo vya juu wanavyoingia na kutoka kwa haraka wakati Sethi akiwa katika anga zake kwenye hoteli ya Sea C liff, ambako anakaa mara kwa mara anapokuwa jijini Dar es Salaam.
Zitto Kabwe, Mb
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
No comments:
Post a Comment