Saturday, 20 September 2014
Hatari: Wajawazito watumia dawa za kienyeji kuongeza uchungu
Imeelezwa kuwa kitendo cha baadhi ya wanawake wajawazito kutumia dawa za kienyeji kuongeza uchungu ili waweze kujifungua mapema ni moja kati ya sababu inayochangia kuongezeka kwa vifo vya Mama wajawazito kutokana na dawa hizo kuwadhuru.
Taarifa zinaeleza kuwa mbali na tatizo hilo pia kitendo cha Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) kuchelewesha dawa na vifaa tiba kwa ajili ya wajawazito kutofika kwa wakati katika maeneo husika hali hiyo haiwezi kusaidia kupunguza vifo vya kundi hilo.
Baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini ukiwemo mkoa wa Singida, wamesema ikiwa MSD watafikisha kwa wakati vifaa tiba na dawa kwaajili ya wajawazito ni dhahiri kuwa vifo hivyo vitapungua kwa kuwa wajawazito hao watajifungua katika mazingira yaliyo salama kuliko kutumia dawa za kienyeji.
Chales Bakari, mkazi wa mkoa huo amesema endapo akina mama watajifungua katika mazingira salama, nchi ingeweza kufikia malengo ya milenia ya kupunguza vifo vya mama wajawazito licha ya vifo hivyo kupungua kutoka vifo 452 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi kufikia 432 kwa kila vizazi hai 100,000.
Akizungumza na FikraPevu Kaimu Mkuu wa MSD, Cosmas Mwaifwani, amesema tangu mwaka wa fedha uliopita wameanza kupeleka vifaa tiba moja kwa moja katika ngazi na vituo vya afya na kufikisha kwa mlaji kwa lengo la kufikisha huduma kwa mlengwa ilia pate huduma ubora na kwa wakati.
Amesema hatua hiyo imeboresha huduma ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kutoka asilimia 45 hadi kufikia asilimia 88.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya mkoa wa Kigoma, Dkt. Leonard Subi, amesema tatizo la kukosekana kwa dawa na vifaa tiba mkoani humo lipo kwa asilimia kubwa na kwamba juhudi za kunasua vifo vinavyotokana na ukosefu wa dawa linashughulikiw ana mamalaka husika kutokana na vifo vingi kutokea maeneo ya vijijini.
Akizungumzia suala la vifo vinavyotokana na baadhi ya wajawazito kutumia dawa za kienyeji kuongeza uchungu amebainisha kuwa “Juzi tu nimeshuhudia mama amekufa kwa kunywa lita tatu za dawa za kienyeji na bahati mbaya kizazi kilipasuka na yeye alikufa japo kuwa tulifanya jitihada za kumuokoa lakini zilishindikana, jamii inatakiw akujua kwamba dawa za kienyeji sasa hivi sio dili, tunazodawa nzuri waendelee kutumia vituo vya afya badala ya kukimbilia kuzalishwa nyumbani kusiko na usalama”
Kwa upande Mganga Mkuu wa Hospitali ya mkoa wa Mtwara, Ligula, Dkt. Shaibu Maarifa, amebainisha kuwa licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali bado kitendo cha wanawake wajawazito wanaojifungulia majumbali na kutumia dawa za kienyeji kwa ajili ya kuongeza uchungu kimekuwa changamoto kubwa katika kukabiliana na vifo hivyo.
Baadhi ya Hospitali zilizopo jijini Dar es Salaam ikiwemo ya Sinza Hospitali, Daktari wa kitengo cha wazazi, Dkt. Suzan Mwasha, amesema bado changamoto ya vifo vya kundi hilo ni kubwa kutokana na wengi wao kujifungulia majumbani badala ya kutumia vituo vya afya vyenye wataalamu kutokana na Imani potofu kuwa watajifungua salama.
“Tumeshuhudia mara kadhaa wanajawazito wanaleta Hospitalini wakiwa wameshindwa kujifungulia majumbani kwa muda mrefu lakini juhudi za kuokoa maisha yao zilifanyika na wachache kati yao afya zao zinazidi kuimarika”
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa moja ya taarifa iliyoripotiwa na FikraPevu hivi karibuni ilionyesha kuwa serikali ya Tanzania imeshindwa kukabiliana na tatizo la vifo vya mama na mtoto wenye umri chini ya miaka mitano, kutokana na uzazi unaofanyika chini ya kiwango bila kuboresha miundombinu ya barabara, majengo, vitendea kazi vya kitaaluma pamoja na kushindwa kufikia malengo ya milenia namba nne na tano ifikapo 2015 ikiwa imesalia miezi kadhaa bila kukamilika kwa malengo hayo.
Takwimu mbalimbali zilionyesha kuwa wanawake wengi katika nchi za Afrika ikiwamo Tanzania, hupoteza maisha kutokana na tatizo la ujauzito ambapo inakadiriwa kuwa wanawake 3,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na matatizo yatokanayo na uzazi ukiwemo ugonjwa ya fistula huku wanawake 19 wakifa kila siku nchini kutokana na matatizo hayo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment