welcome

you are welcome dj zombie blog, dodoma tanzania. for latest videos, audios and news.

Wednesday 15 October 2014

KOVA AKANUSHA UTEKAJI WA WATOTO DAR ES SALAAM

Hussein Makame-MAELEZO
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limekanusha vikali uvumi unaoendelea kuzushwa jijini Dar es Salaam kuhusu utekeaji nyara wa watoto wadogo wanaosoma shule za jiji hilo na kuwataka wananchi kuupuuza.
Akizungmza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema kuwa mpaka sasa jeshi hilo halina taarifa yoyote ya mtoto kutekwa au kufanyiwa madhara yoyote kwa mtindo wa utekaji nyara.
“Jeshi la Polisi limegundua kwamba huu ni uvumi ambao haujulikani chanzo chake hivyo wananchi wanaombwa kuachana nao na kuupuza kwani unaleta hofu katika jamii bila sababu za msingi” alisema Kova.
Alisema kuwa pia uvumi huo umeanza kuleta usumbufu ambapo mnamo Oktoba 3 mwaka huu saa 3:00 asubuhi huko Vingunguti, mtu mmoja aitwaye Prosper Makame (34) akiwa na mkewe Marystella Munis (30) walipata usumbufu unaotokana na uvumi huo.
Kamishna Kova aliongeza kuwa watu hao ambao ni wafanyabiashara wa vyombo vya nyumbani walifika maeneo ya shule ya msingi Kombo iliyopo Vingunguti kwa ajili ya biashara zao, wakiwa na gari aina ya Noah yenye namba  T252 DAY, ghafla walizingirwa na watu wakidaiwa wanateka wanafunzi.

“Pia mnamo Oktoba 13, 2014 majira ya saa 4:00 asubuhi huko katika kituo cha Polisi Tabata uliibuka uvumi kuwa gari namba T548 BUN aina ya Noah rangi nyeusi ambayo ni mali ya askari polisi A/INSP Ester wa kikosi cha usalama barabarani, ilivumishwa kwamba ndani ya gari hiyo kuna vichwa vitano vya watoto wa shule ya msingi Mtambani na kusababisha wazazi wenye watoto wanaosoma shule hiyo kukusanyika kituoni hapo ili kushuhudia na kuona vichwa hivyo” alisema Kamishna Kova na kuongeza:


“Na ndipo Mkuu wa kituo hicho  cha Polisi aliamuru gari hilo lifunguliwe na kuwathibitishia wananchi kuwa habari hizo ni za uongo na uvumi”
Kutokana na tukio hilo jeshi hilo lilifanya uchunguzi na kumkamata mtu mmoja Gilbert Stanley (32) mhehe mkulima na mkazi wa Tabata alipohojiwa alikiri kueneza habari hizo na kudai yeye aliambiwa na mtu ambaye hakumkumbuka.

Hivyo, Kamishna Kova alisisitiza kuwa uvumi wa kuwepo kwa kikundi cha wahalifu wanaowateka watoto wanafunzi si wa kweli hata kidogo na hivyo wananchi wanatakiwa kuepukana na taarifa hizo kwani zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Katika hatua nyingine, Kamishna Kova alithibitisha kutokea kwa vifo vya watu watano na wengine 16 kujeruhiwa katika ajali ya moto iliyotokea Oktoba 13 mwaka huu majira ya saa 5:00 usiku huko kwenye mzunguko wa Mbagala Charambe baada ya lori aina ya Scania  T347 BXG lilipoanguka likiwa na mafuta aina ya petrol lita 38,000.

Aliwataja waliofariki kuwa ni Masoud Masoud mkazi wa Charambe, Hassani Mohamed mkazi wa Mbagala Kibangulile, Mohamed Ismail, Ramadhani Halfan na Maulidi Rajabu wote ni wakazi wa Mbagala Charambe.

Alisema kuwa majeruhi wamelazwa kwenye hospitali ya taifa ya Muhimbili na hospitali ya wilaya ya Temeke wakiendelea na matibabu huku ajali hiyo pia ikisababisha nyumba ya kulala wageni iitwayo United kuungua moto na kuteketea kwa pikipiki saba za bodaboda zilizokuwa zimeegeshwa karibu na aneo hilo, maduka matano yenye bidhaa zenye thamani ya shilingi Milioni 197 yaliungua moto.

Kamishna Kova aliwataka wananchi kuacha tabia ya kukimbilia kwenye ajali za magari ya mafuta kwani ni hatari kwa maisha yao kwani watu wengi waliojeruhiwa walikuwa wakichota mafuta yaliyomwagika kutokanana ajali hiyo.

Katika tukio lingine, Kamishna Kova alisema kuwa Jeshi hilo limefanikiwa kumkamata jambazi sugu aitwaye Paulo Thamas Milanzi maarufu Chinga  (35) mmakonde mkazi wa  Chanika ambaye baada ya majibizano ya risasi jambazi hilo lilijeruhiwa na kufikshwa hospitali ya muhimbili kwa matibabu ingawa baadaye alifariki dunia.

Alisema jambazi hilo lilikuwa likitafutwa na polisi kutokan na kuhusika kwenye matuio ya mauaji na wizi ikiwemo tukio la kuuawa kwa Afisa Mwandamizi wa Usalama wa Taifa, Sylivabus Adrian Mzeru Aprili 29 mwaka huu liliotokea Uwanja wa Ndege.

Aliongeza kuwa jambazi lilikamatwa na bastola aina ya Star ambapo majambazi wenzake walikamatwa na sasa wako gerezani, hivyo ameitahadharisha jamii iachane na uhalifu kwani hauna manufaa yoyote.

No comments: