welcome

you are welcome dj zombie blog, dodoma tanzania. for latest videos, audios and news.

Sunday 14 September 2014

EALA limekuwa Bunge la watalii?


Kwa muda mrefu sasa, Bunge la Afrika Mashariki (EALA), limekuwa katika mizozo isiyoisha kiasi cha wananchi wengi katika nchi wanachama kuhofia kwamba Bunge hilo litasambaratika. Tulishuhudia mara kadhaa miezi michache iliyopita mizozo mikubwa ikiibuka, ikiwa ni pamoja na ule wa ya wabunge kutoka katika baadhi ya nchi wanachama kususia vikao wakipinga utaratibu wa vikao vyote kufanyika katika makao makuu ya jumuiya hiyo yaliyopo jijini Arusha, Tanzania.
Kama siyo busara za wakuu wa nchi wanachama, mzozo huo ungelisambaratisha Bunge hilo. Utaratibu mpya uliwekwa kwa kuboresha kanuni husika ili kuwezesha vikao hivyo kufanyika kwa mzunguko katika kila nchi mwanachama. Mgogoro huo ulimalizika pasipo kutokea madhara makubwa kisiasa, ingawa ulisababisha madhara makubwa kiuchumi kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kutokana na kugharimia safari, malazi na posho za wabunge hao wanapokuwa nje ya kituo chao cha kazi kilichopo jijini Arusha.

Katika kupigania utaratibu huo mpya wa kufanyia vikao katika nchi zote wanachama wa EAC, wabunge hao walijenga dhana kwamba hatua hiyo ingeongeza ufanisi katika shughuli za Bunge hilo. Kinadharia, walijenga taswira ya Bunge linalowajibika, linalopigania masilahi na maendeleo ya wananchi wa Afrika Mashariki. Kumbe walichoficha nyuma ya pazia ni kwamba walitaka starehe na matanuzi katika hoteli za kitalii katika majiji ya nchi wanachama, kwani sasa imethibitika kwamba wengi walikuwa hawahudhurii vikao vya Bunge hilo na mara nyingi Spika Margareth Zziwa alikuwa akilazimika kuahirisha vikao kutokana na kukosekana kwa akidi.
Jambo la kushangaza ni kuwa, hata ilipofika zamu ya Tanzania kuwa mwenyeji wa kikao cha Bunge hilo mwishoni mwa mwezi uliopita, walikataa kukutana Arusha palipo na huduma zote za shughuli za Bunge hilo na kumlazimisha Spika Zziwa kuhamishia vikao vyake jijini Dar es Salaam, pasipo kujali gharama ambazo zingetokana na hatua hiyo. Tulishuhudia Serikali ya Tanzania ikihaha na kutumia fedha za kodi za wananchi kukarabati Ukumbi wa Karimjee ili Bunge hilo liweze kufanyia vikao vyake, ingawa ukumbi huo haukuwa na hadhi ya kufanyia vikao hivyo.
Kilichotokea wakati Bunge hilo lilipoanza vikao vyake hapa jijini ni kichekesho cha mwaka. Wabunge wengi walikuwa watoro na kulifanya Bunge kuahirishwa zaidi ya mara mbili kutokana na kukosekana kwa akidi. Huo ndiyo umekuwa utamaduni wao na tukijiuliza wamefanya nini tangu waingie katika Bunge hilo zaidi ya miaka minne iliyopita hatuna jibu, kwani wengi wao wamejielekeza katika starehe na kusahau kilichowapeleka katika chombo hicho. Wakati wakijieleza katika mabunge ya nchi zao waliapa kufanya kazi kwa kujituma, kujitolea na kusimamia masilahi ya nchi zao. Nini kimetokea mpaka wakawasaliti wananchi wao ni kitendawili ambacho ni vigumu kukitegua.
Tutakuwa hatukosei tukisema wabunge wengi wa Bunge hilo wameharibiwa na tamaa za kidunia, kwa maana ya ubinafsi na kutafuta ‘utukufu’. Tulishuhudia jinsi walivyokuwa wamejipanga kumwondoa madarakani Spika Zziwa kwa kukataa ufisadi wa kuwalipa posho bila kuhudhuria vikao na pia kukataa madai yao ya kutaka kupewa nyongeza nono za mishahara kinyume na kanuni za fedha za jumuiya hiyo. Ni Bunge ambalo hakika wajumbe wake wengi siyo tu wamepoteza mwelekeo, bali pia wamepoteza uhalali wa kuwawakilisha wananchi waliowapatia ‘utukufu’ huo.

No comments: