welcome

you are welcome dj zombie blog, dodoma tanzania. for latest videos, audios and news.

Saturday 4 October 2014

Elimu ya awali Tunduru na changamoto zake

Mwalimu wa darasa la awali wa Shule ya Msingi Nakayaya, Teckla Milanzi (kulia) akiwa na wanafunzi wake eneo ambalo hutumika kama darasa la wanafunzi hao.Mwalimu wa darasa la awali wa Shule ya Msingi Nakayaya, Teckla Milanzi (kulia) akiwa na wanafunzi wake eneo ambalo hutumika kama darasa la wanafunzi hao.[/caption]

WADAU wa elimu nchini Tanzania wanaamini kwa kiasi kikubwa kwamba endapo elimu ya awali (chekechea) nchini Tanzania itatolewa katika misingi inayostahiki itakuwa ni njia moja wapo madhubuti ya kuimarisha ubora wa elimu. Hii ndiyo maana wanaendelea kupaza sauti wakiitaka serikali kupitia vyombo husika kuboresha kwanza elimu ya awali kabla ya kupanda ngazi nyingine za juu.

Huenda kilio hiki cha wadau wa elimu kimeanza kusikika serikalini. Kwani tayari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliagiza tangu mwaka 2010 kuwa kila shule zake za msingi ni lazima lianzishwe darasa la awali ili kuwenza kuwaandaa wanafunzi kuingia na darasa la kwanza. Awali elimu hii ilikuwa ikitolewa kwa kiasi kikubwa na taasisi na vikundi mbalimbali na hata watu binafsi nje ya shule za msingi, tena kwa hiyari. Kwa sasa sera na miongozo ya elimu inatamka wazi kuwa nilazima kila shule ya msingi iwe na darasa la awali kwa ajili ya elimu hiyo muhimu.

Changamoto kubwa iliyoibuka kwa sasa baada ya utekelezaji wa agizo hilo ni namna elimu hiyo inavyoendeshwa kwa kusuasua kwenye baadhi ya shule za Serikali. Hivi karibuni mwandishi wa makala haya alitembelea baadhi ya shule za msingi zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kuangalia hali ya utekelezaji wa zoezi hilo.

Uchunguzi ulibaini zipo shule ambazo licha ya kusajili wanafunzi wa awali kila mwaka hazina madarasa ya kusomea kwa watoto hao, hali ambayo inafanya wanafunzi hao wadogo kufundishwa katika mazingira magumu na kudhohofisha lengo zima la utoaji wa elimu hiyo. Wapo wanafunzi ambao hulazimika kufundishiwa nje, yaani chini ya mti ama kwenye magofu (majengo ya shule ambayo hayajakamilika) iwe madarasa au nyumba za walimu.

Teckla Milanzi ni mwalimu wa darasa la awali, Shule ya Msingi Nakayaya. Anasema kimsingi wanafunzi wa darasa la awali shuleni hapo wanasomea chini ya mti kwa kuwa hawana darasa maalum kwa wanafunzi hao. Anasema wakati wa mvua ama jua kali mara nyingine hulazimika kuhairisha masomo kwa siku kutokana na hali ya hewa.Baadhi ya wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko wakiwa darasani kama walivykutwa na mwandishi wa makala haya hivi karibuni. Baadhi ya wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko wakiwa darasani kama walivykutwa na mwandishi wa makala haya hivi karibuni

Anasema anashukuru kwa sasa wanajihifadhi kwenye jengo moja ambalo linaendelea na ujenzi shuleni hapo, jengo ambalo hata hivyo mara baada ya ujenzi kukamilika na wahusika kukabidhiwa darasa watarudi kusomea chini ya mti kama ilivyo ada. Hata hivyo, anasema licha ya changamoto hiyo darasa hilo halina vitabu kwa ajili ya kufundishia wanafunzi, bali kuna nakala moja moja kwa baadhi ya masomo ambavyo vilitafutwa kwa jitihada za mwalimu mwenyewe.

“Mfano kwa vitabu vya Kiswahili, Kiingereza, Sayansi na Hisabati kuna nakala moja moja tu, ambazo hutumiwa na mwalimu mwenyewe. Anasema darasa hilo licha ya kuwa na changamoto kedekede hata kwenye mgao wa fedha zinazoletwa shuleni kila mara halimo hivyo hakuna kinacholetwa tofauti na wanafunzi wengine,” anasema Bi. Teckla Milanzi.

Kwa upande wake, Mwalimu Christina Komba wa darasa la awali Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko anasema madarasa ya elimu ya awali Wilayani Tunduru yanakabiliwa na changamoto nyingi. Anabainisha kuwa madarasa mengi likiwemo lake hawana vitabu wala miongozo ya namna ya ufundishaji kabisa zaidi ya kila mwalimu anayefundisha kubuni nini afundishe kila uchao.

“…Kwanza licha ya kutokuwa na vifaa vingine hatuna chumba maalumu cha wanafunzi hawa (darasa) kwa sasa tunatumia jengo la darasa ambalo bado linaendelea na ujenzi na hata hivyo jengo hili halijengwi kwa ajili ya wanafunzi wa awali,” anasema mwalimu Christina Komba.Wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Nakayaya, wakiwa katika darasa lao. Wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Nakayaya, wakiwa katika darasa lao.

“Madarasa ya elimu ya awali hayana vitabu, hayana miongozo…huwa tunaanzima au ukipata hela yako wewe binafsi unaenda kununua kitabu kimoja au viwili ili uweze kuwasaidia watoto. Na baadhi ya masomo hayana vitabu kabisa hata ukienda madukani katika Wilaya yetu (Wilaya ya Tunduru) vitabu kama Haiba na Michezo, pamoja na Sanaa hazipo kabisa madukani. Anasema uongozi wa juu wilayani unalitambua hilo.

Batadhari Mkwela ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nanjoka anasema usajili wa wanafunzi wa awali kila mwaka huongezeka japokuwa bajeti ya kuendesha elimu hiyo ni changamoto. “…Darasa la awali linahitaji vitendea kazi lakini havipo, hatuna vifaa kama vitabu vya kutosha, vyenzo za kufundishia, hakuna bajeti hata ya vifaa hivi toka Serikalini, hatuna madawati maalum kwa ajili ya wanafunzi wa awali,” anasema Mkuu huyo wa Shule ya Nanjoka.

Hadija Makamla ni mwalimu wa darasa la awali Shule ya Msingi Majengo. Mwalimu huyu ambaye amehitimu kozi ya kufundisha darasa hilo, anasema anavyo baadhi tu ya vitabu vinavyoitajika katika darasa hilo. Anabainisha kuwa darasa hilo lina jumla ya wanafunzi 48 lakini hutumia darasa la wanafunzi wa kawaida maana hawana darasa lililojengwa maalum kwa wanafunzi wa awali.

“…Ninazo nakala chache kwa ajili ya mwalimu tu ila wanafunzi hawana hata kimoja…lakini kuna masomo mengine sina vitabu kabisa kama vile Sanaa na Haiba ya Michezo sina kabisa hata mimi,” anasema mwalimu Makamla. “…Unajua watoto kwa kiasi kikubwa wanajifunza kwa vitendo, picha na uhalisia, sasa huenda tunavyowapa ni vikubwa zaidi au vidogo sana kwa sababu ya kubuni mada kwa baadhi ya masomo.

Dorothea George ni mwalimu wa darasa la awali shule ya Msingi Nanjoka Wilayani Tunduru. Yeye anasema japokuwa hakuwahi kufanya kozi ya ualimu wa awali kwa sasa amekabidhiwa darasa hilo kulifundisha katika shule yake. Anasema darasa hilo kwa sasa lina wanafunzi 98 ambao wanasomea darasa moja chini ya mwalimu mmoja.

Anasema licha ya darasa hilo kuwa na madawati kadhaa lakini si maalum kwa ajili ya wanafunzi wa awali bali ni ya wanafunzi wa kubwa, hata hivyo bado kuna watoto wanalazimika kukaa chini kwa kile kukosa madawati ya kutosha katika shule hiyo. Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Majengo, Madina Mkali anasema uendeshaji wa darasa la awali shuleni hapo ni wa kusuasua kutokana na changamoto anuai zinazowakabili. Hakuna bajeti inayoingia kuisaidia elimu hiyo, ispokuwa mwaka huu waliletewa madawati kumi kwa ajili ya elimu ya awali.Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Tunduru, Abdul Kazembe akizungumza na mwandishi wa makala haya (hayupo pichani) ofisini kwake hivi karibuni. 
Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Tunduru, Abdul Kazembe akizungumza na mwandishi wa makala haya (hayupo pichani) ofisini kwake hivi karibuni.

“…Uendeshaji elimu ya awali hapa ni wa wastani kwa kweli kutokana na changamoto zinazotukabili, kwanza vifaa vya kuwafundishia watoto hawa ni tatizo na wazazi kwa eneo hili wamekuwa hawana mwamko wa elimu hii kabisa. Kwanza hawachangii michango ya chakula kama inavyotakiwa ili mtoto apate chochote awapo shuleni,” anasema mwalimu Mkali.

Anabainisha kuwa watoto pia wanatakiwa kupata uji wawapo shuleni lakini uchangiaji kwa wazazi nao umekuwa tatizo kubwa. “…Wapo wanaochangia wengine wanagoma tunasukumana hivyo hivyo na mambo yanasonga mbele…lakini kutokana na uchangiaji duni kuna baadhi ya siku wanapata uji na sikunyingine hawanywi kutokana na ugumu wa michango,” anasema mwalimu George.

Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko, Adam Hausi katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya anasema uendeshaji wa elimu ya awali katika shule hiyo ni juhudi binafsi za mwalimu wa darasa hilo. Anasema darasa hilo halina bajeti yoyote kutoka serikalini hivyo hakuna vitabu na vitendea kazi vingine vinavyohitajika.

“…Vitendea kazi ndio tatizo kabisa, ila mwalimu anafundisha kwa jitihada zake na darasa linaendelea. Alafu lina idadi kubwa sana ya wanafunzi (84) na anafundisha peke yake…,” anasema Hausi. Anasema uboreshaji elimu ya msingi ni suala la ushirikiano kati ya Serikali na jamii yenyewe lakini wakati mwingine Serikali inakwamisha juhudi hizo kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo baadhi ya maeneo.

“…Mfano sisi tulijenga madarasa mawili kwa nguvu za wananchi hadi yamekamilika ilipofika suala kuezekwa tokaomba msaada wa Serikali pamoja na kumaliziwa ili yaanze kutumika ilikuwa kazi kweli tulizunguzwa sana hadi tukaanza kuyatumia hivyo hivyo,” alisema.

Bi. Thabita Farara ni Mkazi wa Kata ya Mringoti Mashariki anasema bado mwamko wa elimu ya awali kwa wazazi ni mdogo, maana wazazi wengi wamekuwa wakijiandaa na darasa la kwanza tu kumuandikisha mtoto. Kwa upande wake Asha Komba Mkazi wa Tunduru Stendi anasema yeye anaitambua elimu ya awali na kuikubali lakini ni ile inayotolewa na shule binafsi kama za taasisi. Lakini ile inayotolewa kwenye shule za Serikali ni tatizo kubwa maana hazizingatii ubora wa elimu zaidi ya kuwalundika watoto tu darasani.

“…Mimi naitambua elimu ya awali na watoto wangu wote wamepitia lakini huwa tunawapeleka kwenye chekechea za taasisi mbalimbali kama zinazomilikiwa na makanisa majeshi na zinginezo maana huku ndiyo kidogo mtoto anaandaliwa…kule Serikalini kwanza unakuta darasani wapo kibao alafu muda wote wanacheza tu si kujifunza,” anasema Bi. Komba.

Abdul Kazembe ni Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Tunduru, anasema kwa sasa kila shule ya msingi sera inaelekeza lazima iwe na darasa la awali. Anasema hata katika usajili wa wanafunzi wa darasa la kwanza kwa sasa watoto wa mwanzo kusajiliwa ni wale waliopata elimu ya awali katika shule husika.

“…Kwa hiyo kuna umuhimu wa kila shule kuwa na darasa la awali…changamoto sasa inakuja kwenye vitendea kazi, kwa mwaka 2013 na kurudi nyuma uwepo wa ‘capitation’ ulikuwa pia unaelekeza watoto wa awali wapo mule na hata tunapotoa takwimu za awali tulianza na ‘pre-primary’ (wanafunzi wa awali) hivyo wenyewe wapo, tatizo hapa ni ujaji wa pesa yenyewe ya ‘capitation’ haitimii kama inavyo elekeza, yaani ile wastani ya kwamba kila mtoto apate shilingi 10,000 kwa mwaka hautimii,” anasema.

Anatolea mfano mwaka 2013/14 kiwango cha fedha ambacho kilitakiwa kuja katika halmashauri ya wilaya hiyo ni zaidi ya milioni 366.7. Kiwango hiki ni kile kilichoidhinishwa katika bajeti tu lakini ukirudi kwenye mahitaji halisi ni zaidi ya kiasi kilichoidhinishwa. Anasema kilichokuja ni zaidi ya milioni 196.5 fedha ambayo ni karibia nusu ya kiasi kilichopitishwa kwenye bajeti. Anabainisha hilo ndilo tatizo kubwa kwani hata fedha ambazo zimepitishwa haziji kama ilivyopitishwa kwenye bajeti.

“…Kwa hiyo unaweza kuona kwamba ni ngumu kuigawa fedha hii katika matumizi maana kwanza haitoshi na pili hata kilichotegemewa kuja ni pungufu zaidi tena sana, sasa sijui unaweza kugawa kila shule ipate shilingi ngapi…kwani haitoshelezi,” anasema.

Anasema kwa upande mwingine miundombinu ya madarasa ni changamoto kubwa. Kwa mwaka 2013 idadi ya mahitaji ya madarasa kwa wilaya nzima ilikuwa ni 1,715 lakini ukiangalia vyumba vya madarasa vilivyopo ni kama 900 na kitu na mengine ni ya muda mrefu sana kiasi ambacho yanaelekea kuchakaa jambo ambalo pia yanapungua.

Aidha anaeleza kuwa ukienda kwenye bajeti ya ujenzi wa madarasa mapya milioni 171 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na miundombinu mbalimbali kiasi hiki cha fedha waweza kuta kinauwezo wa kujenga madarasa kama nane tu. Kiasi hicho cha fedha ni pamoja na ujenzi wa nyumba tano za walimu. Na kiasi hicho cha fedha za ujenzi ni pamoja na kumalizia miradi viporo za nyumba za walimu na vyumba vya madarasa. Anasema upungufu wa vyumba vya madarasa eneo hilo ni karibia madarasa 800.

“Sasa kwa ujumla unaweza kuona kuwa miundombinu pale shuleni haitoshelezi, ni jambo la kawaida kuona walimu wakiacha ofisi itumike kama darasa au darasa litumike kama ofisi. Huku kwa awali ni changamoto zaidi maana licha ya upungufu wa vyumba hata wazazi hasa vijijini wanashindwa kuchangia chakula (uji) kwa watoto wao unaweza kukuta wameandikishwa wengi Januari lakini kila muda unavyozidi kwenda watoto wanapungua na unaweza kukuta hadi mwezi Juni darasa linapotea kabisa kwa utoro,” anasema.

Kazembe anabainisha kuwa kuna jumla ya shule za msingi 144 katika wilaya hiyo, huku shule zilizo na vyumba maalumu vya madarasa ya awali zikiwa 16 tu. Anasema shule nyingine zote hazina vyumba vya madarasa ya awali na matokeo yake ama wanatumia madarasa ya msingi kwa kupishana.

Anaongeza kuwa uhamasishaji wa ujenzi wa madarasa ya awali na umuhimu wa elimu hiyo unatolewa kwa walimu, wazazi na kamati za shule kupitia vikao mbalimbali ambapo mara nyingi uongozi uhimiza wazazi kuchangia zaidi nguvu zao katika kukamilisha ujenzi wa madarasa ya awali, utengenezaji wa madawati na upatikanaji wa chakula cha mchana na uji shuleni.

“…lakini tunaangalia sana chakula maana watoto hata kwenye mti wanaweza kukaa wakasoma endapo wanamadawati pale au wamekaa chini kwenye kivuli, japokuwa si mazingira mazuri sana shuleni…lakini wakiwa na chakula hata utoro unapungua,” anasema.

Anasema kwa mwaka 2013 serikali ilikumbuka kuleta fedha kwa ajili ya ununuzi madawati ya wanafunzi wa awali, fedha ambazo tulizigawa na kununua baadhi ya vitabu vya awali na madawati kwenye shule ambazo zinamadarasa hai ya awali. Shule zilizonufaika na mgao huo ni shule za mjini Tunduru tu ambazo nyingi ndizo zenye madarasa hai ya awali. Anasema ili kukabiliana na hali ya upungufu wa walimu wa awali; imepitishwa walimu wa gredi ‘A’ kufundisha madarasa hayo kwa kuwa wao mafunzo yao katika kozi hujumuisha ufundishaji darasa la awali, tangu walioitimu mwaka 2013.

“…sasa wakati mwingine unaweza kukuta mwalimu ni gradi A na kimsingi yeye anao uwezo wa kufundisha darasa la awali, lakini wengine hawakubali hadi aone ana cheti kabisa maalumu cha kufundisha darasa la awali…ukimuuliza huyu atakwambia yeye hana taaluma ya kufundisha awali jambo ambalo si sawa,” anasema Ofisa Elimu huyo wa Msingi.

“..Kwa suala la vitabu kweli hii ni changamoto, hapo nyuma tulikuwa tunanunua vitabu wenyewe wakini kwa sasa TAMISEMI wenyewe moja kwa moja wananunua na kuvileta. Sasa huku kwetu ni nadra sana kuona wazabuni wetu wanaleta vitabu vya awali kwa sababu soko lake ni dogo sana kutokana na idadi ndogo ya uwepo wa elimu hii ya awali eneo husika,” anasema.

Hata hivyo umeona unafuu maeneo ya mjini mzazi anatambua umuhimu wa elimu hivyo anaweza kuchonga dawati kwa ajili ya mtoto wake lakini kwa vijijini hali ni mbaya zaidi. Mzazi ukimwambia achangie dawati anakushangaa na pia haoni umuhimu huo.

“…Nikwambie unajua Wilaya ya Tunduru mzazi mtoto wake akifeli anafurahi sana…tena baadhi wanaona kama ni sherehe, kwanza wakifanya mtihani tu wa la saba barabarani akina mama wanashangilia wanaona wametua mzigo, unaweza kujiuliza wazazi wanaoshangilia inamaana walikuwa wakiona ni adhabu watoto wao kuwa shule? Lakini pia mtoto akisha faulu kwenda shule hapelekwi hadi DC aunde kamati, atembee na hakimu na polisi kukamata wazazi wanaogoma kusomesha watoto watishiwe ndo wanakubali kusomesha…lakini kitendo cha wazazi kukamatwa kushikiliwa kwa kushindwa kuwapeleka watoto shule wamegeuka na kuwarubuni watoto wao wasifaulu,” anasema.

Anabainisha kuwa ni kweli Serikali ina jukumu la elimu, lakini mzazi kwa upande wake anajukumu zaidi, kuangalia mtoto wake anapata elimu gani na ya kiwango gani na kama mzazi hayupo tayari basi haiwezekani na wakati mwingine inakuwa ngumu. Kimsingi jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia watoto wa awali zipo, lakini upatikanaji wa fedha ndio.

Salum Mtutula ni Mbunge wa Tunduru Kusini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbunge huyu katika mahojiano anakiri kuwa elimu ya awali ni muhimu na msingi mzuri wa mtoto kielimu. Anasema mtoto anapopata elimu nzuri ya awali huwa na msingi mzuri kielimu katika masomo yake ya mbele.
“…Ili mtoto apate elimu bora ni lazima apate elimu ya awali inayostahiki…hakiwa na msingi mbaya wa elimu ya awali kuna uwezekano mkubwa way eye kufanya vibaya pia,” anasema Mtutula.

Hata hivyo anaishauri Serikali kuingiza suala hili katika sheria na kanuni zake kuwa kila shule ya msingi inapoanzishwa ianze na darasa la awali kwanza ndipo madarasa mengine yafuate. “…Mimi nitafurahi kama suala hili tutaliweka kwenye sheria au kanuni zetu kuwa kila shule ya msingi inapoanzishwa basi lazima ianze na darasa la awali ndipo madarasa mengine yafuate iwe shule za Serikali au binafsi,” anasema Mbunge Mtutula.
*Imeandaliwa na: www.thehabari.com

No comments: